Sunday, October 7, 2012

MAWAIDHA YA ADABU NA TABIA NJEMA.....



ASSALAM ALAYKUM........
 
Ndugu zangu katika imani leo tunajikumbusha tena na kupeana mawaidha ya adabu na tabia njema,ni imani yangu utafuatilia na kuzingatia,ukiwa na maoni tunaomba uyaandike hapo chini,karibu sana......NI mawaidha tunayoayapata kutoka katika blog mbalimbali za kiislamu ili nasi tupitie na kujua yaliyomo katika mawaidha hayo,yametolewa na..........


Muhammad Faraj Salem Al Saiy

Utangulizi

Mwenyezi Mungu ametufunza adabu za namna nyingi ili ziwe pambo letu Waislam zikitupamba katika matendo yetu, maneno yetu, na pia zikitupamba ndani ya nafsi zetu.
Mapambo ya ndani ya nafsi ni Tabia njema. Na Adabu, ni yale maneno na matendo mema yanayozidhihirisha.

Neno Adabu, asili yake linatokana na neno ‘Maaduba’, na maana yake ni kualikwa chakula au kuitwa. Na neno ‘Adabu’, limetoholewa kutoka katika neno hilo ‘Maaduba’, kwa sababu watu ‘Wanaitwa’ katika kuzifuata tabia njema na katika kuwa na khuluka njema.
Khuluka njema ni msingi madhubuti wa Umma. Ni kuendelea kwa Umma. Ni tumaini la Umma. Ni uhai wa Umma.
Umma ukirudishwa nyuma kwa sababu zozote zile za kilimwengu kisha ukapoteza tabia zake njema na khuluqa zake, si rahisi tena kunyanyuka. Lakini Umma hata ukirudi nyuma namna gani, ikiwa bado umeshikamana na khuluqa njema, basi tumaini la kunyanyuka tena linabaki. Na hii ni kwa sababu Umma wowote ukiacha tabia zake njema na kujifanya kama karagosi kwa kuonyesha kila fani ya kuiga, na jeuri na utovu wa adabu, basi tamaa ya kunyanyuka tena inapotea.
Mshairi alisema:
“Hakika ya umma wowote ule ukitaka kubaki, basi lazima wawe na tabia njema. Tabia njema zao zikitoweka, basi na wao watatoweka.”

Umma wa Kiislamu ni Umma uliolelewa kwa Adabu na Tabia njema tokea Mtume wetu Muhammad (Swalla Llahu alayhi wa sallam) alipoanza kuwalingania watu katika dini hii tukufu.
Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Llahu alayhi wa sallam) alikuwa akisema:
بُعِثْتُ لأتمِّمَ مَكَارِمَ الأَخْلاَقِ
“Kwa hakika nimeletwa kuja kukamilisha (kufundisha) tabia njema”.

Huyu ni Mtume wetu mtukufu (Swalla Llahu alayhi wa sallam) ambaye Mola wake alimsifia na kumwambia:
وإنك لعلى خلق عظيم
 “Na bila shaka una tabia njema kabisa”
Al Qalam – 4

Muislamu anatakiwa awe mwenye adabu na mwenye heshima akiwaheshimu wakubwa wake na wadodo wake.
Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Llahu alayhi wa sallam) amesema:
<ليس منا من لم يرحم صغيرنا، ويعرف شرف كبيرنا>
Hayupo pamoja nasi asiyewahurumia wadogo wetu na asiyeijuwa heshima ya wakubwa wetu.
Attirmidhy na Abu Daud

Na katika riwaya nyingine, Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Llahu alayhi wa sallam) amesema kumuambia Ummu Salamah (Radhiya Llahu anha):
يا أم سلمة ذهب حسن الخلق بخير الدنيا والآخرة
Ewe Ummu Salamah, Tabia njema imechukuwa kheri zote za dunia na akhera.
Attabarani

Muislamu asiyekuwa na adabu anaudhuru Uislamu badala ya kuupa nguvu. Mamilioni ya watu waliingia katika dini hii tukufu kwa kuvutiwa na Adabu na Tabia njema za Masahaba (Radhiya Llahu anhum) waliozifungua nchi zao hizo, pamoja na kuvutiwa na Adabu na Tabia njema za wale waliokuja baada yao.
Mataifa makubwa kama vile Indonesia kwa mfano, mamilioni ya watu wake waliingia katika dini hii kutokana na tabia njema za wafanya biashara wa Kiislam waliokwenda huko. Walikuwa wakiuona uaminifu wao, ukweli wao, ucha Mungu wao. Ilikuwa mara tu unapofika wakati wa Swala, walikuwa wakiwaona namna gani wafanya biashara hao wakiacha kazi zao na kuelekea mwahali maalum kwa ajili ya kufanya Ibada zao.
Imam Malik anasema:
“Umma huu hauwezi kutengenea isipokuwa kwa kufuata mwenendo wa wenzao waliowatangulia”.
Kuwatii wazee wawili
Kuwatii wazee wawili ni miongoni mwa Adabu zilizotiliwa mkazo sana na kusisitizwa katika Qurani na katika mafundisho ya Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Llahu alayhi wa sallam).
Mwenyezi Mungu ametuamrisha tuwatii na kuwafanyia wema wazee wetu, na akazifanya haki za wazee - baba na mama - kuwa katika daraja la pili baada ya haki Zake Subhaanahu wa Taala. Mwenyezi Mungu amewajaalia wazee kuwa ni sababu ya kuwepo kwetu hapa duniani, na kwa ajili hiyo wakapata tabu sana juu yetu.
Hasa Mama, aliyembeba mwanawe tumboni miezi tisa, akamzaa, kisha akahangaika naye na kutaabika naye, tabu juu ya tabu. Tabu ya kubeba, tabu ya kuzaa, tabu ya kulea, kunyonyesha pamoja na kukesha na kuhangaika naye kila mtoto anapolia au kuugua.
Kwa ajili hiyo Mwenyezi Mungu Ametuamrisha kuwakirimu wazee wetu wawili hao, kuwatumikia kuwainamishia bawa la unyenyekevu, pamoja na kuwaombea dua ili Mwenyezi Mungu awarehemu kama walivyotulea huku wakiturehemu tulipokuwa watoto.
Mwenyezi Mungu Anasema:
وَقَضَى رَبُّكَ أَلاَّ تَعْبُدُواْ إِلاَّ إِيَّاهُ وَبِالْوَالِدَيْنِ إِحْسَانًا إِمَّا يَبْلُغَنَّ عِندَكَ الْكِبَرَ أَحَدُهُمَا أَوْ كِلاَهُمَا فَلاَ تَقُل لَّهُمَآ أُفٍّ وَلاَ تَنْهَرْهُمَا وَقُل لَّهُمَا قَوْلاً كَرِيمًا 23 وَاخْفِضْ لَهُمَا جَنَاحَ الذُّلِّ مِنَ الرَّحْمَةِ وَقُل رَّبِّ ارْحَمْهُمَا كَمَا رَبَّيَانِي صَغِيرًا 24

 “Na Mola wako Mlezi ameamrisha kuwa; Msimuabudu yeyote ila Yeye tu, na wazazi wawili muwatendee wema. Mmoja wao akifikia uzee, naye yuko kwako, au wote wawili, basi usimwambie hata: Ah! Wala usiwakemee. Na sema nao kwa msemo wa hishima.
Na uwainamishie bawa la unyenyekevu kwa kuwaonea huruma. Na useme: Mola wanguMlezi! Warehemu kama walivyo nilea utotoni.”
Al israa- Bani Israil 23-24

Na Anasema:
وَوَصَّيْنَا الْإِنسَانَ بِوَالِدَيْهِ حَمَلَتْهُ أُمُّهُ وَهْنًا عَلَى وَهْنٍ وَفِصَالُهُ فِي عَامَيْنِ أَنِ اشْكُرْ لِي وَلِوَالِدَيْكَ إِلَيَّ الْمَصِيرُ
“Na tumemuusia mtu kwa wazazi wake wawili. Mama yake ameichukua mimba yake kwa udhaifu juu ya udhaifu, na kumwachisha ziwa baada ya miaka miwili. (Tumemuusia):Nishukuru Mimi na wazazi wako. Na kwangu Mimi ndiyo marudio.”
Luqman 14

Mafundisho ya Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Llahu alayhi wa sallam) yanakubaliana na mafundisho ya Qurani.
Alipoulizwa juu ya matendo anayoyapenda zaidi Mwenyezi Mungu kupita yote, Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Llahu alayhi wa sallam) alisema:
Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Llahu alayhi wa sallam) alisema:
"الصلاة على وقتها ثم بر الوالدين ثم الجهاد في سبيل اللّه"
"Swala ndani ya wakati wake, kisha kuwafanyia wema wazee wawili kisha jihadi katika njia ya Mwenyezi Mungu."
Fathi l Bari (Sharhi ya Sahihul Bukhari)

Aliiweka amali hii ya kuwafanyia wema wazee wawili kuwa ni ya pili ikiitangulia hata Jihadi katika njia ya Mwenyezi Mungu.

Na alipokuwa akizitaja amali ovu, akaitaja amali ya kuwaasi wazee wawili kuwa ni ya pili baada kumshirikisha Mwenyezi Mungu. Akasema:
قال رسول الله صلى الله عليه وسلم: (ألا أنبئكم بأكبر الكبائر). قلنا: بلى يا رسول الله، قال: (الإشراك بالله، وعقوق الوالدين - وكان متكئاً فجلس فقال - ألا وقول الزور، وشهادة الزور، ألا وقول الزور، وشهادة الزور). فما زال يقولها، حتى قلت: لا يسكت.
Amesema Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Llahu alayhi wa sallam):
“Nikuambieni ni amali zipi zilizo ovu kupita zote?”
Tukasema:
“Tuambie ewe Mtume wa Mwenyezi Mungu”
Akasema:
“Kumshirikisha Mwenyezi Mungu na kuwaasi wazee wawili,”
Alikuwa ameegemea, akakaa vizuri, kisha akasema:
“Na kusema uongo, na kutoa ushahidi wa uongo…”
Akawa anayakariri maneno hayo mpaka tukasema (nyoyoni);
“Yareti angenyamaza”
Bukhari na Muslim

Pakitokea mgongano baina ya haki ya Mwenyezi Mungu na haki ya wazee, kwa mfano mzee awe ni mshirikina akimuamrisha mwanawe naye awe kama yeye katika ushirikina huo, au katika kumuasi Mwenyezi Mungu kwa jambo lolote lile, basi hapo haijuzu kumtii mzee, kwa sababu haki ya Mwenyezi Mungu ni kubwa zaidi na tukufu zaidi. Lakini wakati huo huo kuasi au kumshirikisha Mwenyezi Mungu kwao, kusikuzuwie kuwatendea mema na kusikufanye ukawa unawapiga pande.
Mwenyezi Mungu anasema:
وَإِن جَاهَدَاكَ عَلى أَن تُشْرِكَ بِي مَا لَيْسَ لَكَ بِهِ عِلْمٌ فَلَا تُطِعْهُمَا وَصَاحِبْهُمَا فِي الدُّنْيَا مَعْرُوفًا وَاتَّبِعْ سَبِيلَ مَنْ أَنَابَ إِلَيَّ ثُمَّ إِلَيَّ مَرْجِعُكُمْ فَأُنَبِّئُكُم بِمَا كُنتُمْ تَعْمَلُونَ
“Na pindi wakikushikilia kunishirikisha na ambayo huna ilimu nayo, basi usiwat'ii. Lakini kaa nao kwa wema duniani, nawe ishike njia ya anayeelekea kwangu. Kisha marejeo yenu ni kwangu Mimi, na Mimi nitakuambieni mliyokuwa mkiyatenda.”
Luqman -15
Ndugu wa Nasaba ni wale ulohusiana nao, jamaa zako, ikiwa ni katika wanaoweza kukurithi au wasioweza, unaoweza kuoana nao au usioweza, lakini upo uhusiano wa nasaba baina yenu.
Mwenyezi Mungu Ametutahadharisha juu ya hatari ya kuwapiga pande ndugu wa Nasaba Akasema:
أَيُّهَا النَّاسُ اتَّقُواْ رَبَّكُمُ الَّذِي خَلَقَكُم مِّن نَّفْسٍ وَاحِدَةٍ وَخَلَقَ مِنْهَا زَوْجَهَا وَبَثَّ مِنْهُمَا رِجَالاً كَثِيرًا وَنِسَاء وَاتَّقُواْ اللّهَ الَّذِي تَسَاءلُونَ بِهِ وَالأَرْحَامَ إِنَّ اللّهَ كَانَ عَلَيْكُمْ رَقِيبًا
“Enyi watu! Mcheni Mola wenu Mlezi aliyekuumbeni kutokana na nafsi moja, na akamuumba mkewe kutoka nafsi ile ile. Na akaeneza kutokana na wawili hao wanaume na wanawake wengi. Na tahadharini na Mwenyezi Mungu ambaye kwaye mnaombana, na jamaa zenu. Hakika Mwenyezi Mungu ni Mwenye kuwaangalieni.”
Annisaa - 1
Hapa Mwenyezi Mungu anatutahadharisha tusije tukamuasi, na pia anatutahadharisha juu ya Jamaa zetu, tusije tukawapiga pande na kuachana nao.
Mwenyezi Mungu pia ametutaka tushikamane na kuendeana nao.
Mwenyezi Mungu anasema:
وَإِذْ أَخَذْنَا مِيثَاقَ بَنِي إِسْرَائِيلَ لاَ تَعْبُدُونَ إِلاَّ اللّهَ وَبِالْوَالِدَيْنِ إِحْسَاناً وَذِي الْقُرْبَى وَالْيَتَامَى وَالْمَسَاكِينِ وَقُولُواْ لِلنَّاسِ حُسْناً وَأَقِيمُواْ الصَّلاَةَ وَآتُواْ الزَّكَاةَ ثُمَّ تَوَلَّيْتُمْ إِلاَّ قَلِيلاً مِّنكُمْ وَأَنتُم مِّعْرِضُونَ
“Na tulipofunga agano na Wana wa Israili: Hamtamuabudu yeyote ila Mwenyezi Mungu; na muwafanyie wema wazazi na jamaa na mayatima na masikini, na semeni na watu kwa wema,na shikeni Swala, na toeni Zaka. Kisha mkageuka isipo kuwa wachache tu katika nyinyi; na nyinyi (pia) mnapuuza.”
Al Baqarah - 83

Na Akasema:
وَأُوْلُواْ الأَرْحَامِ بَعْضُهُمْ أَوْلَى بِبَعْضٍ
“Na ndugu wa nasaba wanastahikiana wenyewe kwa wenyewe”
Al Anfal – 75
Na Akasema:
فَآتِ ذَا الْقُرْبَى حَقَّهُ وَالْمِسْكِينَ وَابْنَ السَّبِيلِ ذَلِكَ خَيْرٌ لِّلَّذِينَ يُرِيدُونَ وَجْهَ اللَّهِ وَأُوْلَئِكَ هُمُ الْمُفْلِحُونَ
“Basi mpe jamaa haki yake na masikini na msafiri (aliyeharibikiwa). Hayo ni bora kwa wale wanaotaka radhi ya Mwenyezi Mungu; na hao ndio watakaofuzu”.
Ar Rum – 38

(Neno ‘Rahim’ maana yake ni ‘undugu wa nasaba’)
Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Llahu alayhi wa sallam) amesema:
“Mwenyezi Mungu amelitoa (au amelitohoa) jina la ‘Rahim’ kutoka katika jina lake ‘Al Rahiym’, kisha akasema:
“Atakayekuunga nitamuunga na atakayekukata nitamkata”.
Na hii inamaanisha kuwa Mwenyezi Mungu atamkata (kwa kutomrehemu) yule atakayeukata uhusiano na jamaa zake, na atawaunga (kwa kuwarehemu) wale watakaouendeleza uhusiano huo.

Mtu anaweza kuona kuwa; katika kutembeleana kwa ajili ya kuunganisha uhusiano na ndugu wa nasaba pesa nyingi zinatumika na wakati mwingi unapotea. Lakini Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Llahu alayhi wa sallam) ametufundisha kinyume na hivyo.
Katika hadithi ilisiyomuliwa na Anas bin Malik (Radhiya Llahu anhu), Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Llahu alayhi wa sallam) amesema:
“Anayependa atandaziwe riziki (aongezewe riziki yake), basi aendeleze uhusiano wake na ndugu zake wa nasaba (jamaa zake alohusiana nao)”.
Bukhari
Na katika Hadith al Qudusiy, Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Llahu alayhi wa sallam) amesema:
“Mwenyezi Mungu ameiambia Rahim; ‘Je utaridhika iwapo nitamuunga atakayekuunga na nitamkata atakayekukata?”
Rahim ikasema:
“Ndiyo”
Mwenyezi Mungu Akasema:
“Basi hiyo ni haki yako”
Bukhari

Kuuendeleza uhusiano huu kunakuwa kwa kupendana, kunasihiana, kufanyiana wema na uadilifu, kurudishiana haki zilizopotea, kuwasaidia wale wenye shida kati yao, kujua hali zao, kusameheana katika makosa yanayotokea baina yao mara kwa mara, kuombeana dua, na kwa ujumla kujaribu kuwafanyia kila la kheri na kuwaepusha na kila shari kwa uwezo wote.
Iwapo katika ndugu, yupo au wapo wasiopenda kurudisha uhusiano na ndugu kwa sababu ndugu yake au jamaa yake huyo anapindukia mipaka katika kumuasi Mwenyezi Mungu, na baada ya kujaribu kila njia katika kunasihi kwa kutumia njia mbali mbali za hekima kujaribu kumweka sawa ndugu huyo bila mafanikio, basi hapana ubaya kuepukana na mtu au watu wa aina hiyo, wakati huo huo tukiendelea kuwaombea dua, huenda Mwenyezi Mungu akawahidi na kuwaongoza katika haki.
Mwenyezi Mungu anasema:
وَاعْبُدُواْ اللّهَ وَلاَ تُشْرِكُواْ بِهِ شَيْئًا وَبِالْوَالِدَيْنِ إِحْسَانًا وَبِذِي الْقُرْبَى وَالْيَتَامَى وَالْمَسَاكِينِ وَالْجَارِ ذِي الْقُرْبَى وَالْجَارِ الْجُنُبِ وَالصَّاحِبِ بِالجَنبِ وَابْنِ السَّبِيلِ وَمَا مَلَكَتْ أَيْمَانُكُمْ إِنَّ اللّهَ لاَ يُحِبُّ مَن كَانَ مُخْتَالاً فَخُورًا
“Muabuduni Mwenyezi Mungu wala msimshirikishe na chochote. Na wafanyieni wema wazazi wawili na jamaa na mayatima na masikini na jirani wa karibu na jirani wa mbali, na rafiki wa ubavuni na mpita njia, na walio milikiwa na mikono yenu ya kulia. Hakika Mwenyezi Mungu hawapendi wenye kiburi wanao jifakhiri”.
Annisaa – 36
Na katika hadithi iliyotolewa na Bukhari, Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Llahu alayhi wa sallam) amesema:
“Jibril alikuwa akiendelea kuniusia juu ya Jirani, hata nilidhania atapewa haki ya kunirithi”
Kumfanyia wema jirani, ni kwa kutokumuudhi au kumkera.
Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Llahu alayhi wa sallam) amesema:
“Wallahi si Muislam Wallahi si Muislam”,
Wakamuuliza:
“Nani huyo ewe Mtume wa Mwenyezi Mungu?”
Akasema:
“Ambaye jirani yake haiepuki shari yake”

Katika wema pia, ni kumfanyia jirani ihsani kiasi cha uwezo wako kwa kumsaidia pale anapohitajia msaada wao, kwa kumjulia hali yake, kumpelekea zawadi, yote hayo kiasi cha uwezo.
Mwenyezi Mungu anasema:

يَسْأَلُونَكَ مَاذَا يُنفِقُونَ قُلْ مَا أَنفَقْتُم مِّنْ خَيْرٍ فَلِلْوَالِدَيْنِ وَالأَقْرَبِينَ وَالْيَتَامَى وَالْمَسَاكِينِ وَابْنِ السَّبِيلِ وَمَا تَفْعَلُواْ مِنْ خَيْرٍ فَإِنَّ اللّهَ بِهِ عَلِيمٌ
“Wanakuuliza watoe nini? Sema: Kheri mnayo itoa ni kwa ajili ya wazazi na jamaa na mayatima na masikini na wasafiri. Na kheri yoyote mnayo ifanya Mwenyezi Mungu anaijua”.
Al Baqarah - 215

Na akasema:

وَإِذَا حَضَرَ الْقِسْمَةَ أُوْلُواْ الْقُرْبَى وَالْيَتَامَى وَالْمَسَاكِينُ فَارْزُقُوهُم مِّنْهُ وَقُولُواْ لَهُمْ قَوْلاً مَّعْرُوفًا
“Na wakati wa kugawanya wakihudhuria jamaa na mayatima na masikini, wapeni katika hayo mali ya urithi, na semeni nao maneno mema”.
An Nisaa - 8

Na akasema:

فَآتِ ذَا الْقُرْبَى حَقَّهُ وَالْمِسْكِينَ وَابْنَ السَّبِيلِ ذَلِكَ خَيْرٌ لِّلَّذِينَ يُرِيدُونَ وَجْهَ اللَّهِ وَأُوْلَئِكَ هُمُ الْمُفْلِحُونَ
“Basi mpe jamaa haki yake, na masikini, na msafiri. Hayo ni kheri kwa watakao radhi ya Mwenyezi Mungu. Na hao ndio wenye kufanikiwa”.
Ar Rum - 38
Na katika hadithi, Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Llahu alayhi wa sallam) amesema:
“Mwenye kujishughulisha kuwasaidia Vizuka na Masikini ni mfano wa anayepigana Jihadi katika njia ya Mwenyezi Mungu, au mfano wa mwenye kufunga nyakati za mchana na kuswali nyakati za usiku”.
Bukhari
Na katika hadithi nyingine Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Llahu alayhi wa sallam) amesema:
“Mimi na mwenye kumlea yatima tutakuwa (pamoja) Peponi kama hivi.” Akaashiria kwa kidole cha shahada na cha kati.
Bukhari
Mwenyezi kiburi hupata maradhi mengi yakiwemo kudharau, kusengenya nk. Na hii ni kwa sababu mtu wa aina hii siku zote hujiona kuwa yeye amekamilika, na kwa ajili hiyo huanza kuwatia wenzake kila aina ya ila, wakati ukweli wa mambo ni kwamba yeye ndiye mwenye ila, na kwa ajili hiyo utamuona anajaribu kutafuta ila za wenzake pamoja na makosa yao na kuwaonyesha watu makosa hayo, ili ajionyeshe kuwa yeye amekamilika.
Mtu wa aina hii hupenda kuwadharau wenzake na kuwacheka pale wanapokosea.
Haya yote yameharimishwa. Na Mwenyezi Mungu ametujulisha kuwa mwenye kudharauliwa huenda akawa ni bora kuliko mwenye kudharau, na ujinga wa mwisho ni mtu kumdharau yule aliye bora kuliko yeye.
Mwenyezi Mungu Anasema:
يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا لَا يَسْخَرْ قَومٌ مِّن قَوْمٍ عَسَى أَن يَكُونُوا خَيْرًا مِّنْهُمْ وَلَا نِسَاء مِّن نِّسَاء عَسَى أَن يَكُنَّ خَيْرًا مِّنْهُنَّ
“Enyi mlio amini! Wanaume wasiwadharau wanaume wenzao, wala wanawake wasiwadharau wanawake wenzao. Huenda hao wakawa bora kuliko wao.”
Al Hujurat - 11

Na katika jambo baya la dharau ni kule kuwavunjia watu heshima na kuwaita kwa majina ya kejeli.
Mwenyezi Mungu Anasema:
وَلا تَلْمِزُوا أَنفُسَكُمْ وَلا تَنَابَزُوا بِالاَلْقَابِ بِئْسَ الاِسْمُ الْفُسُوقُ بَعْدَ الايمَانِ وَمَن لَّمْ يَتُبْ فَأُوْلَئِكَ هُمُ الظَّالِمُونَ
“Wala msivunjiane hishima, wala msiitane kwa majina ya kejeli. Ni uovu kutumia jina baya baada ya kwisha amini. Na wasio tubu, hao ndio wenye kudhulumu”.
Al Hujurat - 11

Kuwasengenya watu, na maana yake ni kutafuta makosa yao na upungufu wao, na kuyazungumza kwa wengine.
Waislamu wanatakiwa wawe wenye kupendana mfano wa mwili mmoja, kila mmoja amsitiri mwenzake na sio kumfedhehesha.
Mwenyezi Mungu ِAnasema:
وَلا يَغْتَب بَّعْضُكُم بَعْضًا
“Wala msisengenyane nyinyi kwa nyinyi."
Al Hujurat - 12

Kwa hivyo Muislam anapomsengenya Muislam mwenzake au kumwita kwa jina ovu, anakuwa kama amejifanyia mwenyewe, na hii ni kwa sababu Muislam ni ndugu wa Muislam na Umma wa Kiislam ni Umma mmoja.
Katika mambo aliyoharamisha Mwenyezi Mungu, ni kujiamulia mambo kwa dhana tupu, kwa sababu dhana inaharibu uhusiano baina ya watu na kuwafanya watoe uamuzi kinyume na haki.

Mwenyezi Mungu ِAnasema:
يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا اجْتَنِبُوا كَثِيرًا مِّنَ الظَّنِّ إِنَّ بَعْضَ الظَّنِّ إِثْمٌ
“Enyi mlio amini! Jiepusheni na dhana nyingi, kwani baadhi ya dhana ni dhambi”.
Al Hujurat - 12

Mwenyezi Mungu ametukataza pia kupelelezana kutaka kujua siri za watu au kuona na kusikia yale ambayo wenyewe hawapendi wengine wayasikie.
Mwenyezi Mungu ِAnasema:
وَلا تَجَسَّسُوا
“Wala msipelelezane”.
Al Hujurat - 12
Katika kulifasiri neno ‘Kusengeya’ (Ghiyba), Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Llahu alayhi wa sallam) aliwauliza Masahaba (Radhiya Llahu anhu):
"Mnajua nini maana ya kusengenya (Ghiyba)? "
Wakasema: "MwenyeziMungu na Mtume wake wanajua zaidi".
Akasema: "(Kusengenya) ni kuzungumza juu ya nduguyo (Muislam, akiwa hayupo) yale anayoyachukia".
Akaulizwa: "Je! ikiwa (ila) ninayoizungumzia anayo kweli?"
Akasema: "Ikiwa anayo kweli, basi huko ndiko kusengenya, na ikiwa si kweli, basi hayo ni madhambi makubwa zaidi (kwa kumsingizia uongo)”.
Muslim
Mwenyezi Mungu ametuwekea sheria na mafundisho mbali mbali katika mwenendo wetu na adabu zetu, na Muislam anatakiwa ayafuate. Miongoni mwa mafundisho hayo ni;
Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Llahu alayhi wa sallam) amesema:
“Mwenye kumuamini Mwenyezi Mungu na Siku ya Kiama, amkirimu mgeni wake.”
Bukhari na Muslim
Katika mafundisho ya kiislamu ni kuomba ruhusa kabla ya kuingia majumbani mwa watu.
Mwenyezi Mungu anasema:
يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا لا تَدْخُلُوا بُيُوتًا غَيْرَ بُيُوتِكُمْ حَتَّى تَسْتَأْنِسُوا وَتُسَلِّمُوا عَلَى أَهْلِهَا ذَلِكُمْ خَيْرٌ لَّكُمْ لَعَلَّكُمْ تَذَكَّرُونَ
“Enyi mlio amini! Msiingie nyumba zisio nyumba zenu mpaka mwombe ruhusa, na mwatolee salamu wenyewe. Hayo ni bora kwenu mpate kukumbuka”.
An Nur – 27
Mwenyezi Mungu anasema:
وَإِذَا حُيِّيْتُم بِتَحِيَّةٍ فَحَيُّواْ بِأَحْسَنَ مِنْهَا أَوْ رُدُّوهَا إِنَّ اللّهَ كَانَ عَلَى كُلِّ شَيْءٍ حَسِيبًا
“Na mnapo amkiwa kwa maamkio yoyote, basi nanyi itikieni kwa yaliyo bora kuliko hayo, au rejesheni hayo hayo. Hakika Mwenyezi Mungu ni Mwenye kuhisabu kila kitu”.
An Nisaa - 86

Na Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Llahu alayhi wa sallam) amesema:
“Haki ya Muislamu kwa mwenzake ni mambo matano;
1.   Kumtolea salaam,
2.   Kumtembelea anapoumwa,
3.   Kuhudhuria mazishi yake,
4.   Kuitikia wito anapokualika, na
5.   Kumwombea ndua anapokwenda chafya.
Bukhari na Muslim

Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Llahu alayhi wa sallam) pia ametufundisha namna ya kutoa salam, akasema:
“Aliyepanda (gari, mnyama nk.) anamsalimia anayekwenda kwa miguu, (na) anayekwenda anamsalimia aliyekaa, watoto wawasalimie wakubwa na wachache wawasalimie wengi”.
Bukhari

Na akasema:
“Umtolee salamu unayemjua na usiyemjua”
Bukhari
Katika dini yetu tumefundishwa kusema; ‘Bismillahi’ kabla ya kula, na kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kusema; ‘Alhamdulillah’ baada ya kula, na pia tumefundishwa kula kwa mkono wa kulia.
Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Llahu alayhi wa sallam) alipomuona mtoto mdogo akila chakula ndani ya sinia , mara anakula kilicho chini yake na mara anakula kilicho mbali, akamwambia:
“Ewe kijana! Sema Bismillah, kula kwa mkono wa kulia na kula kilicho karibu yako’
Bukhari na Muslim

Tumefundishwa pia kuwa mtu anapokwenda chafya aseme: ‘Alhamdulillah’, na yule atakayemsikia (akisema Alhamdulillah) amwambie; ‘Yarhamuka Llah’, (Mwenyezi Mungu akurehemu). Kisha yule aliyepiga chafya anamjibu mwenzake kwa kumwambia; “Yahdiykumu Llahu wa yuslih baalakum”.(Mwenyezi Mungu akuhidi na astawishe hali yako).
Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Llahu alayhi wa sallam) amesema:
"إذَا عَطَسَ أحَدُكُمْ فَلْيَقُل: الحَمْدُ لِلَّهِ، وَلْيَقُلْ لَهُ أخُوهُ أوْ صَاحبُهُ: يَرْحَمُكَ اللَّهُ، فإذَا قالَ لَهُ: يَرْحَمُكَ اللَّهُ، فَلْيَقُلْ: يَهْدِيكُمُ اللَّهُ وَيُصْلِحُ بالَكُمْ"
“Mmoja wenu akienda chafya aseme: ’Alhamdulillah’ na amjibu ndugu yake na rafiki yake (kwa kumwambia;) ‘Yarhamuka Llah’, na akimwambia; ‘Yarhamuka Llah’ amjibu kwa kumwambia: ‘Yahdiykumu Llahu wa yuslih baalakum”.
Bukhari
Katika mafundisho ya Kiislam pia tumekatazwa kunon’gona watu wawili ikiwa yupo wa tatu pamoja nao.
Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Llahu alayhi wa sallam) amesema:
“Mnapokuwa watatu, wawili wasinon’gone wakamuacha wa tatu wao, mpaka mchanganyike na watu (muwe wengi) kwa sababu (kutenda) hivyo, kutamhuzunisha (wa tatu wenu)”.
Bukhari na Muslim
Dini yetu imetuamrisha na kupendekeza kuwazuru wagonjwa.
Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Llahu alayhi wa sallam) amesema:
“Muislam anapomzuru ndugu yake Muislam, anakuwa ndani ya bustani za Peponi mpaka atakaporudi.”
Muslim
Ni vizuri pia mtu anapomtembelea mgonjwa na kabla ya kuondoka, asimame kuliani pake kisha aombe dua ifuatayo mara saba:
أسألُ اللَّهَ العَظِيمَ رَبّ العَرْشِ العَظِيمِ أنْ يَشْفِيكَ
“Namuomba Mola mtukufu Mola wa Arshi tukufu, akuafu”
Attirmidhy
Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Llahu alayhi wa sallam) ametukataza kula au kunywa tukiwa tumesimama wima.
Amesema Anas (Radhiya Llahu anhu):
“Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Llahu alayhi wa sallam) ametukataza mtu kunywa akiwa amesima wima”. Anasema Qatada: ‘Tukamuuliza Anas; ‘Na kula je?’ Akasema; “Vibaya zaidi.”
Akimaanisha ‘kula wima’.
Muslim
Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Llahu alayhi wa sallam) ameharamisha mwanamume kuvaa dhahabu na vitambaa vya hariri.
Katika hadithi nyingi zilizomo katika Bukhari na Muslim na vitabu vingine sahihi kutoka kwa Masahaba mbali mbali (Radhiya Llahu anhum) wamesema:
“Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Llahu alayhi wa sallam) ametukataza kuvaa dhahabu na hariri, na (ametukataza pia) kunywa ndani ya vyombo vya dhahabu na vya fedha, na akasema: “Vyombo hivi ni vyao hapa duniani na vyenu huko akhera”
Bukhari na Muslim
Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Llahu alayhi wa sallam) pia ametufundisha namna ya kuwalea watoto, kuwahurumia na kuwabusu.
Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Llahu alayhi wa sallam) alikuwa akiwabusu Al Hassan na Al Hussein (Radhiya Llahu anhum), na alimkataza yule aliyesema kuwa ana watoto kumi na hajapata kumbusu yeyote kati yao hata siku moja. Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Llahu alayhi wa sallam) alimwambia:
“Asiyekuwa na huruma, hatohurumiwa.”
Bukhari
Rehma ya Muislam si kwa ajili kwa wanadamu peke yao, bali tumeamrishwa kuwahurumia hata wanyama.
Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Llahu alayhi wa sallam) alitujulisha juu ya yule aliyekuwa na kiu, na baada ya kunywa maji kisimani akamuona mbwa akihangaika mbele ya kisima, akajisemea moyoni mwake:
“Bila shaka mbwa huyu ana kiu kikubwa”. Akachota maji kisimani na kumnywesha. Mwenyezi Mungu akamghufiria madhambi yake yote.
Masahaba (Radhiya Llahu anhu) waliposikia hayo wakamuuliza:
“Ewe Mtume wa Mwenyezi Mungu, hata katika wanyama tunapata thawabu?”
Akasema:
“Katika kila kiumbe kilicho hai mnapata thawabu (mkikifanyia wema na kukihurumia).
Bukhari

Upole
Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Llahu alayhi wa sallam) ametufundisha kuwa wapole na wavumilivu katika kutatua matatizo yetu. Alimfundisha Bibi Aisha (Radhiya Llahu anhu) hayo pale Bibi Aisha alipowatukana Mayahudi na kuwalani. Akamwambia:
“Taratibu ewe Aisha, Mwenyezi Mungu anapenda upole katika kila kitu”
Bukhari
Kisa chenyewe kilikuwa hivi:
Liliingia kundi la Mayahudi kwa Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Llahu alayhi wa sallam) na badala ya kumtolea salaam kwa kumuambia "ASSALAAM alaykum, wakamuambia:
“ASSAAM aleikum”, na maana yake NI; “Mauti yawe juu yenu.”
Walisema hivyo wakidhania kuwa Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Llahu alayhi wa sallam) hatotambua. Lakini Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Llahu alayhi wa sallam) akawajibu:
“Wa alaikum”. Bila ya kuongeza neno lolote, na maana yake; “Na juu yenu pia”.
Bibi Aisha (Radhiya Llahu anha) aliyekuwa amekaa pamoja na Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Llahu alayhi wa sallam) wakati ule akawajibu kwa ghadhabu:
‘Alaykumu assaam wa Llaana’
“Mauti yawe juu yenu pamoja na laana”
Ndipo Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Llahu alayhi wa sallam) alipomwambia:
“Taratibu ewe Aisha, Mwenyezi Mungu anapenda upole katika kila kitu.”
Anasema Bibi Aisha (Radhiya Llahu anha):
“Nikamwambia: "Hukuwasikia walivyosema?”
Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Llahu alayhi wa sallam) akanijibu:
“Nimesikia, ndio maana nikawajibu ‘Wa aleikum”
Na maana yake “Na juu yenu”
Mwenyezi Mungu ametuamrisha tusaidiane wenyewe kwa wenyewe kwa wema na kwa uchaMungu, akasema:
وَتَعَاوَنُواْ عَلَى الْبرِّ وَالتَّقْوَى وَلاَ تَعَاوَنُواْ عَلَى الإِثْمِ وَالْعُدْوَانِ
“Na saidianeni katika wema na uchamungu. Wala msisaidiane katika dhambi na uadui”.
Al Maidah – 2
Na Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Llahu alayhi wa sallam) amefananisha kushikamana kwa Waislam kuwa sawa na kushikamana kwa mwili mmoja, na akafananisha kushikamana huko kuwa ni sawa na kushikamana kwa majengo.
Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Llahu alayhi wa sallam) amesema:
“Waislam katika kuhurumiana kwao na kupendana kwao na kupendeleana kwao ni mfano wa mwili mmoja, kinaposikitika kiungo (chochote kwa kuumwa), basi mwili wote unashirikiana katika kukesha na kupata homa”.
Bukhari na Muslim
Na katika hadithi nyingine amesema:
“Waislam ni mfano wa majengo, yameshikamana na kuzuwiana yenyewe kwa yenyewe (yasianguke)”.
Bukhari
Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Llahu alayhi wa sallam) ametuhadharisha juu ya tabia mbaya sana ya 'Namiyma', nayo ni mtu kuchukua maneno ya huku na kuyapeleka kule kwa nia ya kufitinisha.
Siku moja Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Llahu alayhi wa sallam) alipopita karibu na kaburi, aliwajulisha Masahaba (Radhiya Llahu anhum) kuwa mwenye kaburi lile anaadhibishwa kwa sababu alikuwa akiishi baina ya wenzake akiwa na tabia hiyo ovu.
Uislam unatufundisha pia ubora wa kusaidia watu na kukidhi haja zao.
Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Llahu alayhi wa sallam) amesema:
“Anayejishughulisha na kuwasaidia ndugu zake, na Mwenyezi Mungu atamsaidia. Na atakayemuondolea Muislam mwenzake dhiki yake, basi Mwenyezi Mungu atamuondolea dhiki katika dhiki zake za Siku ya Kiama. Na atakayemsitiri Muislam na Mwenyezi Mungu atamsitiri Siku ya Kiama”.
Muslim
Tabia, ni ule mwenendo alio nao mwanadamu ndani ya nafsi yake. Mwenendo ambao si rahisi mtu kuweza kuubadilisha, kwa sababu chimbuko lake ni ndani ya nafsi yake, na hatimaye unageuka mwenendo huo kuwa ni sehemu ya dhati yake asiyoweza kuachana nayo.
Baadhi ya maulama wa elimu ya nafsi wanasema kuwa Tabia ya mtu ni mfano wa picha yake ikikuelezea ni nani yeye, na anaweza kujulikana mtu undani wake kutokana na tabia zake.
Bila shaka tabia ziko ovu na ziko njema.

Katika lugha ya kiarabu neno ‘Khalqu’ maana yake “Umbile” na neno “Khuluqu” maana yake “Tabia”. La mwanzo kwa kutumia ‘a’ ‘Khalqu’ na linatujulisha juu ya umbile la nje la kiumbe. Ama la pili kwa herufi ‘u’ ‘Khuluqu’ linatujulisha juu ya umbile la ndani la kiumbe.
Kwa hivyo neno ‘Khalqu’ (Umbile), linamaanisha sura inayo onekana ya kiumbe na neno ‘Khuluqu’ ambalo kwa kiswahili tunaita ‘Khuluka’ na maana yake ni tabia, linatujulisha juu ya zile tabia ambazo si kitu cha kuonekana kwa jicho, bali zimo ndani ya nafsi yake mwanadamu.
Kama tulivyoandika hapo mwanzo kuwa Tabia ziko aina mbili; Njema na Ovu.
Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Llahu alayhi wa sallam) alimuambia Ash'aj Abdul Qais (Radhiya Llahu anhu):
“Una mambo mawili ambayo Mwenyezi Mungu anayapenda; Upole na Kutokuwa na pupa”.
Ahmed – Annasai – na Bukhari katika Adabul mufrad (Fathu l Bari)
Miongoni mwa tabia njema, ni Kusema kweli, Uaminifu, Ukarimu, Kutimiza Ahadi, Ushujaa na Subira. Bila shaka mwenye tabia hizi anastahiki kukirimiwa na kupewa kila sifa anayostahiki.
Miongoni mwa Tabia ovu ni; Kusema Uwongo, Khiana, Uwoga, na Kusengenya.
Mwenye tabia hizi, bila shaka anastahiki kila lawama.
Mwenyezi Mungu ametuwekea sheria inayowaita (inayowalingania) watu katika Tabia njema na kuwakataza Tabia ovu, ili nafsi zipate kutahirika na kutakasika na ili watu waweze kuishi vizuri baina yao.
Kwa ajili hii, utaona kuwa mafundisho mengi ya dini yamezungumzia maudhui haya na hayakuacha kumpa sifa anazostahiki kila mwenye tabia njema. Inatosha kauli yake Suhanahu wa Taala alipomsifia Mtume wake kwa kumwambia:
وَإِنَّكَ لَعَلى خُلُقٍ عَظِيمٍ
“Na bila shaka una tabia njema kabisa”.
Suratul Qalam - 4

Mwenyezi Mungu akatutaka pia tuzikimbilie Rehema Zake na Pepo Yake aliyowatayarishia wacha Mungu katika waja wake wenye sifa hiyo ya Tabia njema.
Mwenyezi Mungu ِِAnasema:
وَسَارِعُواْ إِلَى مَغْفِرَةٍ مِّن رَّبِّكُمْ وَجَنَّةٍ عَرْضُهَا السَّمَاوَاتُ وَالأَرْضُ أُعِدَّتْ لِلْمُتَّقِينَ. الَّذِينَ يُنفِقُونَ فِي السَّرَّاء وَالضَّرَّاء وَالْكَاظِمِينَ الْغَيْظَ وَالْعَافِينَ عَنِ النَّاسِ وَاللّهُ يُحِبُّ الْمُحْسِنِينَ
“Na yakimbilieni maghfira ya Mola wenu Mlezi, na Pepo ambayo upana wake tu ni sawa na upana wa mbingu na ardhi, iliyo wekwa tayari kwa wachamungu.
Ambao hutoa wanapo kuwa na wasaa na wanapo kuwa na dhiki, na wanajizuia
ghadhabu, na wasamehevu kwa watu; na Mwenyezi Mungu huwapenda wafanyao wema.”
Aal Imran – 133-134
Na katika aya ifuatayo, Mwenyezi amewasifia wenye kutimiza ahadi, wavumilivu wakati wa shida, wakati wa madhara na wakati wa vita, kuwa ni watu wenye Tabia njema.
Mwenyezi Mungu Anasema:

لَّيْسَ الْبِرَّ أَن تُوَلُّواْ وُجُوهَكُمْ قِبَلَ الْمَشْرِقِ وَالْمَغْرِبِ وَلَـكِنَّ الْبِرَّ مَنْ آمَنَ بِاللّهِ وَالْيَوْمِ الآخِرِ وَالْمَلآئِكَةِ وَالْكِتَابِ وَالنَّبِيِّينَ وَآتَى الْمَالَ عَلَى حُبِّهِ ذَوِي الْقُرْبَى وَالْيَتَامَى وَالْمَسَاكِينَ وَابْنَ السَّبِيلِ وَالسَّآئِلِينَ وَفِي الرِّقَابِ وَأَقَامَ الصَّلاةَ وَآتَى الزَّكَاةَ وَالْمُوفُونَ بِعَهْدِهِمْ إِذَا عَاهَدُواْ وَالصَّابِرِينَ فِي الْبَأْسَاء والضَّرَّاء وَحِينَ الْبَأْسِ أُولَـئِكَ الَّذِينَ صَدَقُوا
“Sio wema kuwa mnaelekeza nyuso zenu upande wa Mashariki na Magharibi. Bali wema ni wa anaye muamini Mwenyezi Mungu na Siku ya Mwisho na Malaika na Kitabu na Manabii, na anawapa mali kwa kupenda kwake, jamaa na mayatima na masikini na wasafiri, na waombao, na katika ugombozi, na akawa anashika Sala, na akatoa Zaka, na wanao timiza ahadi yao wanapo ahidi, na wanao vumilia katika shidana dhara na wakati wa vita; hao ndio walio sadikisha, hao ndio wajilindao.”
Al Baqarah – 177

Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Llahu alayhi wa sallam) pia ametufundisha mengi juu ya umuhimu wa kuwa na Tabia njema.
Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Llahu alayhi wa sallam) amesema:
“Wema (kutenda mema) ni (katika) Tabia njema”.
Muslim

Na akasema:
“Mbora wenu ni yule mwenye Tabia njema zaidi”.
Bukhari

Na akasema:
“Kwa hakika, Muislam mkamilifu wa Imani ni yule mwenye Tabia njema kupita wenzake”
Attirmidhiy na Al Hakim

Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Llahu alayhi wa sallam) pia ametujulisha kuwa Tabia njema ndiyo yenye uzito zaidi juu ya mizani Siku ya Kiama.
Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Llahu alayhi wa sallam) amesema:
“Hakuna chenye uzito zaidi juu ya mizani kuliko Tabia njema”
Bukhari, Abu Daud, Attirmidhiy na imesahihishwa na Ibni Hibban

Tabia njema pia ni katika sababu kubwa za kuingizwa katika Pepo ya Mwenyezi Mungu.
Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Llahu alayhi wa sallam) alipoulizwa juu amali gani zinazowaingiza watu zaidi Peponi akasema:
“Ucha Mungu na Tabia njema”
Attirmidhiy na Ibni Hibban (Bukhari katika Fathi l Bari)

Na akasema:
“Katika wale ninaowapenda sana miongoni mwenu na watakaokuwa karibu nami Siku ya Kiama, ni wale wenye Tabia njema, na katika wale ninaowachukia na watakaokuwa mbali zaidi nami, ni wale wenye kusema maneno mengi yasiyo na maana na wenye kuzungumza kwa kujinata (huku akiukaza ulimi na kuuregeza na kujifanya kuwa yeye ni mfasihi kuliko wenzake) na wenye kuzungumza kwa kiburi.”
Attirmidhiy

Bila shaka mwenye Tabia na mwenendo mwema pamoja na maneno mazuri yasiyo na kiburi, ni mwenye kupendeka zaidi mbele ya wenzake.
Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Llahu alayhi wa sallam) amesema:
“Hamtopendwa na watu kwa ajili ya mali zenu, bali mtapendwa kwa ajili ya ukunjufu wa nyuso zenu na Tabia zenu njema”.
Al Bazzaar
Tumesoma hapo mwanzo kuwa Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Llahu alayhi wa sallam) ni mfano bora wa kufuatwa katika Tabia njema, hata Mola wake Subhaanahu wa Taala Akamuambia:
وَإِنَّكَ لَعَلى خُلُقٍ عَظِيمٍ
“Na bila shaka una tabia njema kabisa”.
Suratul Qalam - 4

Masahaba wake (Radhiya Llahu anhum) na adui zake, wote walikubaliana juu ya Tabia zake njema. Hajawahi hata siku moja yeyote katika adui zake kumtuhumu Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Llahu alayhi wa sallam) kuhusu jambo hili, bali Tabia zake njema zilijulikana kila pembe ya dunia.
Anas bin Malik (Radhiya Llahu anhu) alimtumikia Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Llahu alayhi wa sallam) miaka kumi, na alikuwa hambanduki kila anapokwenda, na kwa ajili hiyo bila shaka alikuwa akimjua vizuri sana Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Llahu alayhi wa sallam).
Tumsikilize nini anasema juu ya Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Llahu alayhi wa sallam):
Anasema Anas (Radhiya Llahu anhu):
“Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Llahu alayhi wa sallam) alikuwa mbora wa viumbe, mkarimu kupita wote na alikuwa shujaa kupita wote”.
Anaendelea kusema:
“Nimemtumikia Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Llahu alayhi wa sallam) miaka kumi, wallahi hajapata hata siku moja kuniambia:”Ah!”, na wala hajapata kuniambia kuhusu jambo lolote nililofanya: ”Kwa nini umefanya," au "bora ungefanya hivi”.
Muslim
Mwenyezi Mungu Subhanahu wa Taala kama alivyozisifia Tabia njema, pia amezilaumu Tabia ovu pamoja na wenye tabia hizo.
Mwenyezi Mungu ِِِAnasema:
وَلا تُطِعْ كُلَّ حَلافٍ مَّهِينٍ. هَمَّازٍ مَّشَّاء بِنَمِيمٍ. مَنَّاعٍ لِّلْخَيْرِ مُعْتَدٍ أَثِيمٍ
“Wala usimt'ii kila mwingi wa kuapa wa kudharauliwa.
Mtapitapi, apitaye akifitini. Mwenye kuzuia kheri, dhaalimu, mwingi wa madhambi.
Mkavu, na juu ya hayo, mshari, amejipachika tu.”
Al Qalam – 10 - 13

Katika kumkataza mwanawe tabia mbovu, Luqmaan mwenye hekima alisema:

وَلا تُصَعِّرْ خَدَّكَ لِلنَّاسِ ولا تَمْشِ فِي الْأَرْضِ مَرَحًا إِنَّ اللَّهَ لا يُحِبُّ كُلَّ مُخْتَالٍ فَخُورٍ
“Wala usiwabeuwe watu, wala usitembee katika nchi kwa maringo. Hakika Mwenyezi Mungu hampendi kila anaye jivuna na kujifakhirisha.”
Luqman – 18
Baadhi ya wataalam wanasema kuwa; Tabia ni mizizi iliyo ndani ya nafsi ya mtu. Ni kitu alichoumbwa nacho, na kwamba haiwezekani mtu kujirekebisha au hata kujaribu kuzibadilisha tabia zake. Baadhi ya watu wakapata kisingizio kutokana na msemo huu, wakaona uzito kujitahidi katika kuzirekebisha tabia zao.
Lakini ukweli ni kwamba zipo katika Tabia njema ambazo mtu ameumbwa nazo ndani ya nafsi yake. Na mtu anapojaaliwa na kitu kama hicho, amshukuru Mwenyezi Mungu aliyempa fadhila hizo.
Wakati huo huo zipo tabia njema ambazo mtu huzipata kwa kujaribu na kujitahidi, kama tulivyoona katika ile hadithi ya Al Ash'aj wakati Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Llahu alayhi wa sallam) alipomwambia:
“Una mambo mawili ambayo Mwenyezi Mungu anayapenda; Upole na Kutokuwa na pupa”.
Al Ash'aj, akamuuliza Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Llahu alayhi wa sallam):
“Ninazo (tabia hizo) tokea mwanzo (nimezaliwa nayo) au nimezipata baadaye?”
Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Llahu alayhi wa sallam) akamjibu:
“Tokea mwanzo”
Akasema:
“Namshukuru Mwenyezi Mungu aliyeniumba na tabia mbili anazozipenda”.
Ahmed – Annasai – na Bukhari katika Adabul mufrad (Fathu l Bari).
Katika kuisherehesha hadithi hii, anasema Ibni Hajar Al Asqalani, mmoja wa Maulamaa wakubwa wa Kiislam:
“Kutokana na jawabu ya Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Llahu alayhi wa sallam), tunaelewa kuwa zipo katika Tabia mtu ameumbwa nazo, na zipo zile ambazo mtu anaweza kuzipata au kujifunza”.
Fathi l Bari

Zipo dalili nyingi zinazothibitisha kuwa mtu anaweza kuzipata au kujifunza.Tabia njema:

Kwanza:-
Tunaona kwa mfano mtu mwoga, kutokana na kupewa mafunzo mengi na jitihada nyingi anageuka kuwa shujaa. Na pia tunaona mara nyingine mtu mwongo, kwa mafunzo na malezi bora, anageuka kuwa ni msema kweli. Kama vile tulivyoona wagomvi na watu waovu, baada ya kumjua Mola wao na kuongezeka imani yao, wanageuka kuwa ni watu wema, na wakati huo huo tunaona watu wema wanapochanganyika na watu waovu kwa muda mrefu, wao nao wanageuka kuwa watu waovu.

Pili:-
Tumeona pia mara nyingi wanyama wanapopata mafunzo, hubadilisha Tabia zao. Tumeona kwa mfano paka anapopata mafunzo maalum, huishi pamoja na mapanya, na mbwa anaishi na paka, na pia tumeona kima wanapopata mafunzo maalum huweza kufanya mambo mengi ya kiajabu. Ikiwa mwenendo wa wanyama unaweza kubadilika, basi uwezo wa mwanadamu ni mkubwa zaidi.
Tatu:-
Mweyezi Mungu katika sehemu nyingi ametutaka tuzibadilishe tabia zetu na kuwa na Tabia njema.
Mwenyezi Mungu ِِAnasema:
يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُواْ اتَّقُواْ اللّهَ وَكُونُواْ مَعَ الصَّادِقِينَ
“Enyi mlio amini! Mcheni Mwenyezi Mungu, na kuweni pamoja na wakweli.”
At Tawba – 119

Na Akasema:
وَاصْبِرْ وَمَا صَبْرُكَ إِلاَّ بِاللّهِ وَلاَ تَحْزَنْ عَلَيْهِمْ وَلاَ تَكُ فِي ضَيْقٍ مِّمَّا يَمْكُرُونَ
“Na subiri. Na kusubiri kwako kusiwe ila kwa sababu ya Mwenyezi Mungu tu. Wala usiwahuzunikie; wala usiwe katika dhiki kwa hila wanazo zifanya.”
An Nahl-127

Na Akasema:
وَأَنفِقُواْ فِي سَبِيلِ اللّهِ وَلاَ تُلْقُواْ بِأَيْدِيكُمْ إِلَى التَّهْلُكَةِ وَأَحْسِنُوَاْ إِنَّ اللّهَ يُحِبُّ الْمُحْسِنِينَ
“Na toeni katika njia ya Mwenyezi Mungu, wala msijitie kwa mikono yenu katika maangamizo. Na fanyeni wema. Hakika Mwenyezi Mungu huwapenda wafanyao wema.”
Al Baqarah - 195

Ingelikuwa Tabia za mtu haziwezi kubadilika, basi amri za Mwenyezi Mungu pale anapotutaka tubadilishe Tabia zetu na kuzifanya ziwe njema zitakuwa hazileti maana. Na kila mwenye akili timamu anatambua kuwa Mwenyezi Mungu haamrishi jambo lisilo na maana wala haamrishi yale tusiyoyaweza.
Mwenyezi Mungu Anasema:
لاَ يُكَلِّفُ اللّهُ نَفْسًا إِلاَّ وُسْعَهَا لَهَا مَا كَسَبَتْ وَعَلَيْهَا مَا اكْتَسَبَتْ رَبَّنَا لاَ تُؤَاخِذْنَا إِن نَّسِينَا أَوْ أَخْطَأْنَا رَبَّنَا وَلاَ تَحْمِلْ عَلَيْنَا إِصْرًا كَمَا حَمَلْتَهُ عَلَى الَّذِينَ مِن قَبْلِنَا رَبَّنَا وَلاَ تُحَمِّلْنَا مَا لاَ طَاقَةَ لَنَا بِهِ وَاعْفُ عَنَّا وَاغْفِرْ لَنَا وَارْحَمْنَآ أَنتَ مَوْلاَنَا فَانصُرْنَا عَلَى الْقَوْمِ الْكَافِرِينَ
“Mwenyezi Mungu haikalifishi nafsi yoyote ila kwa kadiri iwezavyo. Faida ya iliyo yachuma ni yake, na khasara ya iliyo yachuma ni juu yake pia. (Ombeni:)Mola wetu Mlezi! Usituchukulie tukisahau au tukikosea. Mola wetu Mlezi! Usitubebeshe mzigo kama ulio wabebesha wale walio kuwa kabla yetu. Mola wetu Mlezi Usitutwike tusiyo yaweza, na utusamehe, na utughufirie, na uturehemu. Wewe ndiye Mlinzi wetu. Basi tupe ushindi tuwashinde kaumu ya makafiri.”
Al Baqarah - 286

Nne:-
Katika hadithi sahihi, Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Llahu alayhi wa sallam) amesema:
“Hakika ya elimu (mtu huipata) kwa kujifunza, na upole (mtu hujifunza) kwa kuwa mpole na mtu anapoitafuta kheri ataipata, na anayejiepusha na shari, huepushwa nayo.”
Al Khatib, kutoka kwa Abi Huraira
Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Llahu alayhi wa sallam) pia alikuwa akimuomba Mwenyezi Mungu amuongoze katika Tabia njema.
Katika dua ya kufungulia sala alikuwa akiomba kwa kusema:
واهدني لأحسن الأخلاق لا يهدي لأحسنها إلا أنت واصرف عني سيئها لا يصرف عني سيئها إلا أنت
Na maana yake ni;
“Na uniongoze katika Tabia njema, hapana aongozae katika Tabia njema isipokuwa Wewe. Na uniepushe na Tabia mbaya, hapana anaye epusha nazo isipokuwa Wewe.”
Muslim, Attirmdhy Annasai na wengine
Mmoja katika maulamaa wa India aitwae Muhammad Yaaqub Al Fairuz Abadiy amezigawa Tabia njema katika sehemu nne zifuatazo;
1.           Subira
2.           Wema
3.           Ushujaa
4.           Uadilifu

1.           Mwenye Subira kwa kawaida huwa mstahamilivu. Hupenda kuwaondolea wenzake udhia, huwa mwenye huruma, mpole, na kwa kawaida mweye Subira hawi na tabia ya pupa na uamuzi wa haraka.
2      Mtu Mwema daima hujiepusha na utovu wa adabu na uovu katika vitendo na matamshi, na pia huwa mwingi wa haya. Na tabia hii ya kuona haya ni nguzo muhimu sana katika mambo ya kheri.
Wema pia humuepusha mtu na matendo machafu, ubakhili, uwongo, kusengenya na kufitinisha watu kwa kuchukua maneno ya huku na kuyapeleka kule.
3      Mtu Shujaa kwa kawaida hujiheshimu. Hapendi kuwakosea wenzake kama vile yeye alivyokuwa hapendi kukosewa. Shujaa pia huwa na tabia ya kuwatakia wenzake kheri, hata kama yeye atakosa, na huwa na uwezo wa kuzuwia ghadhabu zake na kwa kawaida huwa mpole.

Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Llahu alayhi wa sallam) amesema:
“Ushujaa si kwa uhodari wa kupigana mieleka, bali ushujaa ni mtu anayeimiliki nafsi yake wakati wa ghadhabu”.
Huu ndio ushujaa, nao ni ufalme na hawezi kuumiliki ufalme huo isipokuwa Shujaa peke yake.
4      Uadilifu, kama alivyosema Feiruz Abadi; Humfanya mwenye tabia hiyo kuweza kufanya mambo yake yote kwa Uadilifu, kati na kati bila ya kupindukia mipaka katika kutoa wala katika kuzuwia nk.
Ukweli ndiyo njia ya ushindi na mafanikio, na uwongo ndiyo njia ya kushindwa na upotofu. Hivi ndivyo dini yetu inavyotufundisha na hivi ndivyo ilivyothibiti katika maisha yetu na matendo yetu ya siku zote.
Kama yupo mwenye kudhania kinyume cha hayo, basi amekosea. Akiwepo anayedhania kuwa uwongo ndio utakaomuokoa, na ukweli utamuangamiza, basi huyo bado hajaijua vizuri haki na yuko mbali nayo kabisa.
Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Llahu alayhi wa sallam) ametufundisha hayo katika hadithi iliyosimuliwa na Abdillahi bin Masaood (Radhiya Llahu anhu).
Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Llahu alayhi wa sallam) amesema:
“Shikamaneni na ukweli, kwa sababu ukweli unaongoza katika wema, na wema kwa hakika unaongoza katika Pepo, na mtu anaposema kweli na akawa anajilazimisha (kila anaposema) kusema kweli, mpaka ataandikwa kwa MwenyeziMungu kuwa ni Msemakweli. Na jiepusheni na uwongo, kwa sababu uwongo kwa hakika unaongoza katika maovu, na maovu kwa hakika yanaongoza katika Moto. Na mtu anaposema uwongo, na akawa anajilazimisha (kila anaposema) kusema uwongo, mpaka ataandikwa kwa Mwenyezi Mungu kuwa kuwa ni Muongo”.
Bukhari na Muslim

Zifuatazo ni sifa walizopewa waliosadiki na kuamini kikweli:
Mwenyezi Mungu ِAnasema:
مِنَ الْمُؤْمِنِينَ رِجَالٌ صَدَقُوا مَا عَاهَدُوا اللَّهَ عَلَيْهِ فَمِنْهُم مَّن قَضَى نَحْبَهُ وَمِنْهُم مَّن يَنتَظِرُ وَمَا بَدَّلُوا تَبْدِيلا
“Miongoni mwa Waumini wapo watu walio timiza waliyo ahidiana na Mwenyezi Mungu.Baadhi yao wamekwisha kufa, na baadhi wanangojea, wala hawakubadilisha (ahadi) hata kidogo.”
Al Ahzab – 23

Wale waliokadhibisha na kutoa ahadi za uwongo, Mwenyezi Mungu Amesema juu yao:
وَمِنْهُم مَّنْ عَاهَدَ اللّهَ لَئِنْ آتَانَا مِن فَضْلِهِ لَنَصَّدَّقَنَّ وَلَنَكُونَنَّ مِنَ الصَّالِحِينَ. فَلَمَّا آتَاهُم مِّن فَضْلِهِ بَخِلُواْ بِهِ وَتَوَلَّواْ وَّهُم مُّعْرِضُونَ. فَأَعْقَبَهُمْ نِفَاقًا فِي قُلُوبِهِمْ إِلَى يَوْمِ يَلْقَوْنَهُ بِمَا أَخْلَفُواْ اللّهَ مَا وَعَدُوهُ وَبِمَا كَانُواْ يَكْذِبُونَ
“Na miongoni mwao wapo walio muahidi Mwenyezi Mungu kwa kusema: Akitupa katika fadhila yake hapana shaka tutatoa sadaka, na tutakuwa katika watendao mema.
Alipo wapa katika fadhila yake wakaifanyia ubakhili na wakageuka, na huku
Wakipuuza, basi akawalipa unafiki kuutia nyoyoni mwao mpaka Siku watapo kutana naye, kwa sababu ya kuwa walimkhalifu Mwenyezi Mungu katika yale waliyo muahidi, na kwa sababu ya kusema kwao uwongo.”
At Tawba – 75-77

'Ukweli', kama unavyotakiwa katika mazungumzo na katika kutimiza ahadi, pia unatakiwa katika matendo. Kwa sababu mtu anapoahidi kutenda jambo, kwa mfano anapomuahidi Mwenyezi Mungu kutoa sadaka atakapojaaliwa kupata pesa, basi wakati unapowadia lazima aitimize ahadi hiyo. Na siku zote mtu anatakiwa ajitahidi katika kuudhihirisha ukweli katika kauli zake na matendo yake, ili matendo hayo yadhihirishe yale yaliyo ndani ya nafsi yake.
Msema kweli siku zote hupendeza mbele ya watu. Wanamuaminisha hata mali zao. Ushahidi wake unakubaliwa na unakuwa na uzito mbele ya wenzake. Kinyume na muongo ambaye watu hawamsadiki, na ushahidi wake haukubaliwi, na watu hawamuamini katika mali zao.
Atakayejichunguza akaijua asili yake aliyoumbiwa na Mwenyezi Mungu, akauchunguza ulimwengu aliyezaliwa na kukuwa ndani yake, kisha akamjua Mola wake mtukufu aliyemuumba yeye na aliyeumba ulimwengu wote, itambidi aondoe majivuno yake, na amsitahi Mola wake mtukufu. Kustahi huko, kutaonekana matunda yake katika kauli zake anazotamka na katika matendo yake.
Tumsikilize Mwenyezi Mungu Akituelezea juu ya waja wake wasiokuwa na majivuno.
Mwenyezi Mungu Anasema:
وَعِبَادُ الرَّحْمَنِ الَّذِينَ يَمْشُونَ عَلَى الاَرْضِ هَوْنًا وَإِذَا خَاطَبَهُمُ الْجَاهِلُونَ قَالُوا سَلامًا
“Na waja wa Arrahman (Mwingi wa Rehema) ni wale wanao tembea ulimwenguni kwa staha, na wajinga wakiwasemeza hujibu: Salama!”.
Al Furqan - 63

Kiburi kinatokana na ujinga wa mtu asiyeijuwa kadiri yake na asiyeijuwa kadiri ya Mola wake aliyemuumba. Kwa sababu kila kitu hapa duniani ni cha kupita, hakina thamani yoyote na hakistahiki mtu kutakabari kwa ajili yake.
Pesa zitaondoka, ufalme utaondoka, uzuri utatoweka na uhai haudumu milele. Hapana atakayebaki isipokuwa Mwenyezi Mungu peke yake.
Mwenyezi Mungu Anasema:
كُلُّ مَنْ عَلَيْهَا فَانٍ. وَيَبْقَى وَجْهُ رَبِّكَ ذُو الْجَلالِ وَالإكْرَامِ
“Kila kilioko juu yake kitatoweka.”
Na atabakia Mwenyewe Mola wako Mlezi Mwenye utukufu na ukarimu.”
Ar Rahman – 26 – 27

Kwa hivyo mwenye kiburi anajipachika cheo asichostahiki. Anashindana na Mola wake katika moja wapo ya sifa Zake, na Mwenyezi Mungu haridhiki na jambo hilo.
Katika Hadithul Qudusiy, Mwenyezi Mungu anasema:
“Kiburi ni (mfano wa) vazi langu la chini, na utukufu ni (mfano wa) vazi langu la juu atakaye (jaribu) kuninya’nganya moja kati ya hizo, nitamtupa Motoni na wala sijali.”
Muslim
Mwenye kiburi hawezi kufaidika na wenye kuilingania haki, kwa sababu kiburi chake kinamzuwia asiweze kuikubali haki, na matokeo yake hupata hasara kubwa.
Mwenyezi Mungu anasema:
سَأَصْرِفُ عَنْ آيَاتِيَ الَّذِينَ يَتَكَبَّرُونَ فِي الأَرْضِ بِغَيْرِ الْحَقِّ وَإِن يَرَوْاْ كُلَّ آيَةٍ لاَّ يُؤْمِنُواْ بِهَا وَإِن يَرَوْاْ سَبِيلَ الرُّشْدِ لاَ يَتَّخِذُوهُ سَبِيلاً وَإِن يَرَوْاْ سَبِيلَ الْغَيِّ يَتَّخِذُوهُ سَبِيلاً ذَلِكَ بِأَنَّهُمْ كَذَّبُواْ بِآيَاتِنَا وَكَانُواْ عَنْهَا غَافِلِينَ
“Nitawatenga na Ishara zangu wale wanao fanya kiburi katika nchi bila ya haki. Na wao wakiona kila Ishara hawaiamini. Wakiiona njia ya uwongofu hawaishiki kuwa ndiyo njia; lakini wakiiona njia ya upotofu wanaishika kuwa ndiyo njia. Hayo ni kwa sababu wamezikanusha Ishara zetu, na wameghafilika nazo.”
Al Aaraf- 146

Na mwenye kiburi hupata hasara ya nafsi yake, kwa sababu yeyote mwenye sifa ya kuwa na kiburi, Mwenyezi Mungu humdhalilisha.
Mwenyezi Mungu Anasema:
إِنَّ الَّذِينَ يَسْتَكْبِرُونَ عَنْ عِبَادَتِي سَيَدْخُلُونَ جَهَنَّمَ دَاخِرِينَ
“Kwa hakika wale ambao wanajivuna na kuniabudu Mimi wataingia Jahannamu wadhalilike”.
Ghafir (Al Muuminun) – 60

Mwenyezi Mungu anamdhalilisha mwenye kiburi, lakini wakati huo huo asiye na kiburi Mwenyezi Mungu humtukuza na kumkirimu.
Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Llahu alayhi wa sallam) anasema:
“Mwenyezi Mungu humuongezea utukufu mja wake anayesamehe, na mtu anapoondowa kiburi chake mbele ya Mwenyezi Mungu, basi Mwenyezi Mungu humnyanyua”.
Muslim

Al Fudhail bin Abbas amemuelezea asiye na kiburi kuwa na sifa zifuatazo;
“Mwenye kuikubali haki na kuifuata. Hata ukiisikia kutoka kwa asiyekuwa na elimu, (haki) lazima uikubali”.
Kitabu ‘Tahadhiyb mauidhatul Muuminin’

Lakini kiburi ni kinyume na hivyo. Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Llahu alayhi wa sallam) amesema:
“Kiburi ni kuipinga haki na kuwadharau watu”.
Muslim
Wafuasi wa dini zote wanajulikana kwa sifa zao maalum. Sifa ambazo wasiokuwa wao hawana. Kwa mfano Mayahudi wanajulikana kuwa wana sifa ya khofu, Manasara, wana sifa ya kupenda. Ama Waislamu, wao wana sifa ya aina yao peke yao, nayo ni mchanganyiko wa khofu na kupenda, nayo ni kuona haya.
Katika kitabu chake Imam Malik kiitwacho Al Muwata- a anasema:
Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Llahu alayhi wa sallam) amesema:
“Kila dini ina khuluqa zake, na khuluqa za Uislamu ni kuona haya”.
Khuluqa njema inamuongoza mtu katika kufanya amali njema, lakini khuluqa mbaya inamuongoza mtu katika maovu. Kwa hivyo anayemsitahi Mwenyezi Mungu, hupenda kumtii, na kuepukana na kumuasi pamoja na kumuabudu kama anavyopaswa kuabudiwa.
Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Llahu alayhi wa sallam) amesema:
“Msitahini Mwenyezi Mungu kama anavyopaswa kustahiwa”
Attirmidhy
Na akasema:
“Kuona haya hakuleti (kingine) isipokuwa kheri tupu”.
Bukhari na Muslim

Na kuona haya ni dalili ya kuwa na imani.
Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Llahu alayhi wa sallam) amesema:
“Imani ina sehemu sabini na zaidi. Sehemu ya juu kabisa ni kauli ya ‘La ilaaha illa Llah’ na ya chini ni kuondoa udhia barabarani, na kuona haya ni sehemu katika sehemu za imani”.
Bukhari na Muslim

Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Llahu alayhi wa sallam) siku moja alipokuwa akipita njiani, alimsikia mtu akimnasihi ndugu yake apunguze kuona haya, Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Llahu alayhi wa sallam) akamwambia:
“Mwache, kwani kuona haya ni dalili ya kuwa na imani”.
Bukhari na Muslim

Ikiwa kuona haya kunamsaidia mtu katika matendo ya kheri, kwa hivyo kutokuwa na haya kunaondoa vile vikwazo vinavyomfanya mtu asitende maovu na kumfanya ateleze na kuanza kuyatenda maovu hayo.
Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Llahu alayhi wa sallam) amesema:
“Katika maneno yaliyonukuliwa kutoka kwa Mitume iliyotangulia; (ni haya yafuatayo): “Ikiwa huna haya, basi tenda utakalo”.
Bukhari

Juu ya kuwa kuona haya ni jambo la kheri, lakini haya hizo zisimpeleke mtu akaacha kufanya matendo mema, kukakataza maovu na kuuliza katika mambo ya dini yale asiyoyaelewa.
Ummu Salama (Radhiya Llahu anha) amesema kumwambia mumewe Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Llahu alayhi wa sallam):
“Ewe Mtume wa Mwenyezi Mungu, hakika Mwenyezi Mungu Hatutaki tuone haya katika (kuijua) haki, je! Mwanamke anapoota anatakiwa kukoga?”
Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Llahu alayhi wa sallam) akasema: “Ndiyo, atakapoyaona maji”
Bukhari
Kupendelea, nako ni mtu kumpendelea kheri mwenzake kuliko nafsi yake. Na hii ni daraja kubwa isiyoweza kufikiwa isipokuwa na watu wenye daraja kubwa. Masahaba (Radhiya Llahu anhum) walizifikia daraja hizo, na Mwenyezi Mungu ameshuhudia hayo pale Aliposema:
وَيُؤْثِرُونَ عَلَى أَنفُسِهِمْ وَلَوْ كَانَ بِهِمْ خَصَاصَةٌ
“Bali wanawapendelea kuliko nafsi zao, ingawa wao wenyewe ni wahitaji.”
Hashr – 9

Abu Huraira (Radhiya Llahu anhu) amesimulia kuwa; mgeni mmoja aliyetoka safari ya mbali alimwendea Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Llahu alayhi wa sallam) na kumwambia:
“Mimi nimechoka sana”.
Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Llahu alayhi wa sallam) (alitaka kumkirimu yeye mwenyewe, lakini) hakuwa na chochote nyumbani kwake cha kuweza kumkirimu mgeni yule. Akawauliza Sahaba zake (Radhiya Llahu anhum):
“Nani atakayemkirimu mgeni huyu usiku wa leo?”
Mmoja katika watu wa Madina akasema:
“Mimi, ewe Mtume wa Mwenyezi Mungu”.
Akamchukua na kwenda naye mpaka nyumbani kwake na kumwambia mkewe:
“Tumkirimu, huyu ni mgeni wa Mtume wa Mwenyezi Mungu”.
Katika riwaya nyingine, imepokelewa kuwa alisema kumuuliza mkewe:
“Kuna chakula chochote nyumbani?”
Mkewe akajibu:
“Hakuna chochote isipokuwa chakula cha watoto wetu tu”.
Akasema:
“Wababaishe kwa chochote kile, na njaa itakapowashika sana wakataka kula chakula chao cha usiku, jaribu kuwalaza, watakapoingia wageni wetu nyumbani, zima taa, kisha tujifanye kama na sisi tunakula nao.”
Wakawakaribisha, wageni wakala, na wao wakalala na njaa yao.
Asubuhi yake alipokwenda kwa Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Llahu alayhi wa sallam), Mtume akamwambia:
“Mwenyezi Mungu amefurahishwa na yale mliyowatendea wageni wenu usiku wa jana”.
Bukhari na Muslim

Tabia njema zilioje na nafsi njema zilioje, kwa hakika watu hawa walikuwa na ukarimu usio na kifani.

Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Llahu alayhi wa sallam) aliwapa sifa za aina ya pekee watu wa kabila la Al Ash'ariy, na hili ni kabila la Sahaba maarufu Abi Musa Al Ash ary (Radhiya Llahu anhu).
Akasema:
“Watu wa kabila la Al Ash'ary wanapokuwa safarini sehemu za mbali kwa ajili ya kupigana Jihadi, watu wao walioko Madina chakula cha watoto kikipungua, basi hukusanya kile walichonacho katika kitambaa kimoja, kisha wakagawana sawa sawa baina yao. Kwa hivyo wao ni wenzangu na mimi mwenziwao”.
Bukhari na Muslim
Atakayesoma juu ya mwenendo wa Waislam na kudurusu sira zao, akaona namna gani walivyokuwa wakikirimiana, atatambua maana ya kauli yake Subhanahu wa taala ِAliposema:
وَالَّذِينَ تَبَوَّؤُوا الدَّارَ وَالايمَانَ مِن قَبْلِهِمْ يُحِبُّونَ مَنْ هَاجَرَ إِلَيْهِمْ ولا يَجِدُونَ فِي صُدُورِهِمْ حَاجَةً مِّمَّا أُوتُوا وَيُؤْثِرُونَ عَلَى أَنفُسِهِمْ وَلَوْ كَانَ بِهِمْ خَصَاصَةٌ وَمَن يُوقَ شُحَّ نَفْسِهِ فَأُوْلَئِكَ هُمُ الْمُفْلِحُونَ
“Na walio na maskani zao na Imani yao kabla yao, wanawapenda walio hamia kwao, wala hawaoni choyo katika vifua vyao kwa walivyo pewa (Wahajiri), bali wanawapendelea kuliko nafsi zao, ingawa wao wenyewe ni wahitaji. Na mwenye kuepushwa uchoyo wa nafsi yake, basi hao ndio wenye kufanikiwa."
H’ashr – 9
Likiwepo kundi la watu wasiokuwa na mwamana wala ahadi, basi watu wa aina hii hawawezi hata kidogo kuaminiana wenyewe kwa wenyewe, na hali zao zinakuwa mfano wa wanyama. Hawajali kitu isipokuwa kupata wanachokitaka hata kama kupata kwao huko kutasababisha maafa kwa wenzao.
Kwa ajili hiyo Mwenyezi Mungu ametuteremshia aya nyingi zinazotuhimiza juu ya kuwajibika kurudisha amana za watu na kutimiza ahadi.
Mwenyezi Mungu ِAnasema:
يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُواْ لاَ تَخُونُواْ اللّهَ وَالرَّسُولَ وَتَخُونُواْ أَمَانَاتِكُمْ وَأَنتُمْ تَعْلَمُونَ
“Enyi mlio amini! Msimfanyie khiana Mwenyezi Mungu na Mtume, wala msikhini amana zenu, nanyi mnajua.”
Al Anfal – 27

Na Akasema:
إِنَّ اللّهَ يَأْمُرُكُمْ أَن تُؤدُّواْ الأَمَانَاتِ إِلَى أَهْلِهَا
“Hakika Mwenyezi Mungu anakuamrisheni mzirudishe amana kwa wenyewe”.
An Nisaa – 58

Na Anasema:
وَأَوْفُواْ بِالْعَهْدِ إِنَّ الْعَهْدَ كَانَ مَسْؤُولاً
“Na timizeni ahadi. Kwa hakika ahadi itasailiwa.”
Al Israa (Bani Israil) – 34

Na Akasema:
وَأَوْفُواْ بِعَهْدِ اللّهِ إِذَا عَاهَدتُّمْ
“Na timizeni ahadi ya Mwenyezi Mungu mnapo ahidi”.
An Nahl – 91

Na Akasema:
يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُواْ أَوْفُواْ بِالْعُقُودِ
“Enyi mlio amini! Timizeni ahadi.”
Al Maidah – 1
Na Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Llahu alayhi wa sallam) kaviingiza vitendo vya kusema uwongo, kuvunja ahadi na kuikhini amana katika dalili za Unafiki.
Katika hadithi iliyosimuliwa na Abu Huraira, Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Llahu alayhi wa sallam) amesema:
“Alama za mnafiki ni tatu; Akizungumza husema uwongo, akiahidi hatimizi na akiaminiwa hufanya khiana.”
Bukhari na Muslim

Na kutoka kwa Abdillahi bin Amru bin Al Aas; kuwa Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Llahu alayhi wa sallam) amesema:
“Tabia nne, yeyote aliyekuwa nazo (tabia hizi) anakuwa mnafiki halisi. Na aliyekuwa na moja kati ya tabia hizo, amekuwa na moja wapo ya tabia za unafiki mpaka aiache (tabia hiyo); Anapoaminiwa hufanya hiana, anapozungumza husema uwongo, anapoahidi huenda kinyume, na anapochukizwa huvuka mipaka (katika ghadhabu).”
Bukhari na Muslim
Mwenyezi Mungu amewasifia wenye kujiepusha na ubakhili.
Mwenyezi Mungu Anasema:
وَمَن يُوقَ شُحَّ نَفْسِهِ فَأُوْلَئِكَ هُمُ الْمُفْلِحُونَ
“Na wenye kuepushwa na ubakhili wa nafsi zao, hao ndio wenye kufaulu.”
At Taghabun – 16

Na wale waliojidanganya nafsi zao kwa kuona kuwa katika ubakhili mna kheri, Mwenyezi Mungu anawaonya juu ya adhabu kali inayowangojea.
Mwenyezi Mungu ِAnasema:
وَلاَ يَحْسَبَنَّ الَّذِينَ يَبْخَلُونَ بِمَا آتَاهُمُ اللّهُ مِن فَضْلِهِ هُوَ خَيْرًا لَّهُمْ بَلْ هُوَ شَرٌّ لَّهُمْ سَيُطَوَّقُونَ مَا بَخِلُواْ بِهِ يَوْمَ الْقِيَامَةِ وَلِلّهِ مِيرَاثُ السَّمَاوَاتِ وَالأَرْضِ وَاللّهُ بِمَا تَعْمَلُونَ خَبِيرٌ
“Wala wasione wale ambao wanafanya ubakhili katika yale aliyowapa Mwenyezi Mungu katika fadhila Zake kuwa ni bora kwao (kufanya ubakhili huko). La!, ni vibaya kwao. Watafungwa kongwa (madude ya kunasa shingoni) za yale waliyoyafanyia ubakhili – Siku ya Kiama”.
Aali Imran – 180

Na ِAkasema:
وَالَّذِينَ يَكْنِزُونَ الذَّهَبَ وَالْفِضَّةَ وَلاَ يُنفِقُونَهَا فِي سَبِيلِ اللّهِ فَبَشِّرْهُم بِعَذَابٍ أَلِيمٍ. يَوْمَ يُحْمَى عَلَيْهَا فِي نَارِ جَهَنَّمَ فَتُكْوَى بِهَا جِبَاهُهُمْ وَجُنوبُهُمْ وَظُهُورُهُمْ هَـذَا مَا كَنَزْتُمْ لأَنفُسِكُمْ فَذُوقُواْ مَا كُنتُمْ تَكْنِزُونَ
“Na wanao kusanya dhahabu na fedha, wala hawazitumii katika Njia ya Mwenyezi Mungu, wabashirie khabari ya adhabu iliyo chungu.
Siku zitapo tiwa moto katika Moto wa Jahannamu, na kwazo vikachomwa vipaji vya nyuso zao na mbavu zao na migongo yao, wakaambiwa: Haya ndiyo mlio jilimbikia nafsi zenu, basi onjeni mliyo kuwa mkilimbika.”
At Tawba – 34 – 35

Na ubakhili unaangamiza jamii, kwani kwa ajili yake (ubakhili), damu nyingi zilimwagika, na heshima zilivunjwa.
Imepokelewa kutoka kwa Imam Muslim kuwa Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Llahu alayhi wa sallam) amesema:
“Uogopeni ‘Jiepusheni’ na ubakhili, kwa sababu ubakhili uliwaangamiza wale waliokuwepo kabla yenu, uliwafanya wamwage damu zao na wakubali heshima za wanawake zao zivunjike”.
Kwa kawaida mwanadamu huipenda sana mali yake. Kwa ajili hiyo Mwenyezi Mungu ametuletea aya nyingi zikituelezea juu ya thawabu pamoja na ujira mkubwa watakaoupata wale watakaozitoa mali zao katika njia anazozipenda Mwenyezi Mungu na kuridhika nazo.
Mwenyezi Mungu Anasema:
مَّن ذَا الَّذِي يُقْرِضُ اللّهَ قَرْضًا حَسَنًا فَيُضَاعِفَهُ لَهُ أَضْعَافًا كَثِيرَةً وَاللّهُ يَقْبِضُ وَيَبْسُطُ وَإِلَيْهِ تُرْجَعُونَ
“Ni nani atakeyemkatia Mwenyezi Mungu sehemu bora (ya mali yake kwa kuwapa masikini na kutoa katika mambo mengine ya kheri) ili Mwenyezi Mungu amzidishie mzidisho mwingi na Mwenyezi Mungu ndiye anayezuwia na ndiye anayetowa na Kwake (nyote) mtarejeshwa.”
Al Baqarah – 245

Na Akasema:
وَسَارِعُواْ إِلَى مَغْفِرَةٍ مِّن رَّبِّكُمْ وَجَنَّةٍ عَرْضُهَا السَّمَاوَاتُ وَالأَرْضُ أُعِدَّتْ لِلْمُتَّقِينَ. الَّذِينَ يُنفِقُونَ فِي السَّرَّاء وَالضَّرَّاء وَالْكَاظِمِينَ الْغَيْظَ وَالْعَافِينَ عَنِ النَّاسِ وَاللّهُ يُحِبُّ الْمُحْسِنِينَ
“Na yakimbilieni maghfira ya Mola wenu Mlezi, na Pepo ambayo upana wake ni sawa na mbingu na ardhi, iliyo wekwa tayari kwa wachamngu.
Ambao hutoa wanapo kuwa na wasaa na wanapo kuwa na dhiki, na wanajizuia
ghadhabu, na wasamehevu kwa watu; na Mwenyezi Mungu huwapenda wafanyao wema.”
Aali Imran – 133 – 134

Na Akasema:
فَأَمَّا مَن أَعْطَى وَاتَّقَى. وَصَدَّقَ بِالْحُسْنَى. فَسَنُيَسِّرُهُ لِلْيُسْرَى
“Ama mwenye kutoa na akamcha Mungu. Na akaliwafiki lilio jema. Tutamsahilishia yawe mepesi.”
Al Layl – 5 – 7
Mtu hasidi ni mtu mouvu sana anayeudhika na kuumia moyoni pake kila wenzake wanapofurahi na kila wenzake wanapopata mafanikio au wanaponeemeka. Kila anapomuona mtu amepata neema, basi hutamani neema hiyo imuondokee na imjie yeye. Na huenda hata akajitahidi katika kufanya baadhi ya vitimbi ili aipate yeye neema hiyo.
Mtu hasidi si rahisi kupona kutokana na maradhi yake hayo, ndiyo sababu Mwenyezi Mungu akatutaka tujikinge Kwake kutokana na shari ya hasidi anapohusudu.
Mwenyezi Mungu ِAnasema:
قُلْ أَعُوذُ بِرَبِّ الْفَلَقِ 1 مِن شَرِّ مَا خَلَقَ 2 وَمِن شَرِّ غَاسِقٍ إِذَا وَقَبَ 3 وَمِن شَرِّ النَّفَّاثَاتِ فِي الْعُقَدِ 4 وَمِن شَرِّ حَاسِدٍ إِذَا حَسَدَ 5
1.   “Sema: Najikinga kwa Mola Mlezi wa mapambazuko,
2.   Na shari ya alivyo viumba,
3.   Na shari ya giza la usiku liingiapo,
4.   Na shari ya wanao pulizia mafundoni,
5.   Na shari ya hasidi anapo husudu.”
Al Falaq

Uhasidi ni dhambi ya mwanzo aliyoasiwa Mwenyezi Mungu, kwa sababu kilichomfanya Ibilisi akatae kumsujudia Adam ni husda. aliposema:
قَالَ أَنَاْ خَيْرٌ مِّنْهُ خَلَقْتَنِي مِن نَّارٍ وَخَلَقْتَهُ مِن طِينٍ
“Mimi ni bora kuliko yeye. Umeniumba kwa moto, naye umemuumba kwa udongo.“
Al Aaraf – 12

Mayahudi nao walimkanusha Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Llahu alayhi wa sallam) kwa sababu ya uhasidi wao. Kisha hawakutoshelezwa na hayo, wakafanya kila aina ya vitimbi wapate kuwatoa Waislam katika dini yao.
Mwenyezi Mungu Anasema:
وَدَّ كَثِيرٌ مِّنْ أَهْلِ الْكِتَابِ لَوْ يَرُدُّونَكُم مِّن بَعْدِ إِيمَانِكُمْ كُفَّاراً حَسَدًا مِّنْ عِندِ أَنفُسِهِم
“Wengi miongoni mwa watu wa Kitabu wanatamani lau wange kurudisheni nyinyi muwe makafiri baada ya kuamini kwenu, kwa ajili ya uhasidi uliomo ndani ya nafsi zao.”
Al Baqarah – 109

Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Llahu alayhi wa sallam) ameutahadharisha Umma wake juu ya kitakacho sababisha kufarikiana wao kwa wao na kujenga chuki baina yao. Yaliyo msitari wa mbele kabisa katika yanayosababisha hayo ni husda.
Katika Sahih Muslim, kutoka kwa Abu Huraira (Radhiya Llahu anhu) kuwa Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Llahu alayhi wa sallam) amesema:
“Msioneane husda wala msifanyiane hiana, wala msichukiane, wala msiendeane kinyume, wala mtu asiuze kile alichokwisha muuzia mwenzake na kuweni (enyi) waja wa Mwenyezi Mungu ndugu”.
Si katika uhasidi mtu kutamani kupata neema aliyopata mwenzake kwa nia nzuri, bali huko kunaitwa ‘kutamani’, tofauti na kuhusudu.
Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Llahu alayhi wa sallam) amesema:
“Hairuhusiwi husuda isipokuwa katika mambo mawili;
Mtu, Mwenyezi Mungu amempa mali, akawa anaitowa katika njia ya Mwenyezi Mungu usiku na mchana, na mtu Mwenyezi Mungu amempa Qurani, (amehifadhi vizuri Qurani), anaamka usiku na kuswali pamoja na mchana huku akiisoma.”

Mwanadamu akizichunguza neema za Mola wake alizomneemesha nazo, kisha akamtizama yule aliye duni yake akihangaika na dunia, lazima itamuondoka husda aliyo nayo na ataanza kushukuru.
Wasalaamun ala l Mursaliyna wa l hamdu li Llahi rabbi l aalamiyn