Monday, January 28, 2013

Maendeleo ya Jengo la Mradi wetu....

Assalam Alaykum.....!! zifuatazo ni picha mbili zenye kutonesha hali halisi ya maendeleo ya jengo letu la mradi wa Jumuiya. Picha zimepigwa tarehe 27, Januari 2013.








Unajionea sehemu kubwa ya ujenzi umekamilika bado katika suala zima la kuweka mambo sawa ili jengo liendane na hadhi ya Waislamu na Jumuiya yetu ya MSATEKU....Tayari tanki la maji lipo tayari.....vyoo alikadhalika....na hata sakafu na mambo mengine ya ndani yamekamilika.

Semina ya Wanafunzi wa Kidato cha Sita (2013).

Assalam alaykum!!!Jumuiya ya MSATEKU kupitia kamati yake ya Taaluma...iliandaa tena semina kwa vijana wa kidato cha Sita katika jiji la Mbeya.Ama hakika hatuna budi kumshukuru Allah kwa Kuwapatia nguvu kamati hii,pia uongozi wa Jumuiya kwa kuwapa rukhsa ya kuifanya semina hii.......Lengo kuu la semina kuwaanda vijana wa kidato cha Sita,hususani vijana wa kiislamu,kujiandaa vema na hatimaye kufaulu mitihani yao itakayofanyika wiki mbili zijazo.Tutakuletea mada moja wapo iliyowasilishwa katika Semina hiyo na baadhi ya picha ya matukio ya siku hiyo ya Jumapili,tarehe 27,Januari,2013.

Head Secretary-MSATEKU


Bismillahir Rahmanir Rahiim:

I'M PROUD TO BE A MUSLIM:
1:) Islam is the religion of peace
 2:) Islam is the religion of peace and justice
3:) Islam is the religion of peace and tolerance
4:) Islam is the religion of peace and prosperity.
YOUR BROTHER: Amry Jaribu, Don’t forget me in your nice prayers THANKS.

Jumapili, tarehe 27 Januari, 2013. Assalam alaykum……
Hatuna budi kumshukuru Allah kwa kutupa nguvu na uzima wa kukutana wote hapa katika msikiti wa jumuiya ya MSATEKU kwa lengo la kuambiana mambo mawili, matatu kuhusiana na MBINU ZA UFAULU KWA MTAHINIWA,MAMBO YA KUFANYWA NA YASIYOTAKIWA KUFANYWA NA MTAHINIWA  NDANI YA CHUMBA CHA MTIHANI.Namuomba Allah awapeni usikivu na mie kunipa nguvu ya kuwasilisha mada zangu kwenu,wanafunzi wa KIDATO CHA SITA na wengineo………..awali ya wote na nitaanza mada yangu kwa  chachu hizi….

 Mtihani ni kipimo cha imani (kidini), uelewa au ufahamu wa mtu juu ya kitu fulani kwa mfano Mwenyezimungu (s.w) ametuandalia mitihani mbali mbali kama maradhi au vifo ili kutupima imani zetu kama tutafaulu au tutafeli. Pia katika mashule yetu imeandaliwa mitihani ili kutupima ufahamu uelewa wetu juu ya yale ambayo tunayasomea.

Katika namna ya kujiandaa na mitihani kupo kwa namna kuu mbili nazo ni; 

(i) Maandalizi ya kivitendo, hapa mtu hujiandaa pale tu anapoingia katika shule kutokana na kufahamu kuwa ipo siku atafanya mitihani na kumaliza shule. Mitihani hiyo ndiyo ambayo itakufanya uweze kufaulu na kwenda katika ngazi ya juu zaidi au kutokwenda. Hivyo basi hatuna budi kujiandaa kwa namna yoyote ile iwayo ili tuweze kufaulu na kuweza kuendelea katika ngazi za juu zaidi na hatimaye kuweza kutimiza yale malengo yetu. 

(ii) Maandalizi ya kiimani, Katika maandalizi haya mtu huanza katika ngazi ya kifamilia, kuanzia pale unapozaliwa hadi kufikia kiwango cha kuweza kujitegemea kwa maisha yako na hatimaye kuwa baba au kuwa mama. 

Hivyo hatuna budi basi kuamini kuwa mitihani nikipimo cha kuamini Qadar (kheri au shari ) zinatokana na Mwenyezimungu (s.w). Hivyo basi hatuna budi kuelewa kuwa tunadhimma ya kutekeleza yale yote ambayo ndiyo sababu ya sisi kufaulu au kufeli katika mitihani hiyo (KIIMANI) Hivyo katika maandalizi haya hatuna budi kuiendea mitihani yetu katika namna ambayo Mwenyezimungu (sw) ataipendelea ambayo ni;

i. kusimama visimamo vya usiku, 

ii. Kuingia katika chumba cha mtihani haliyakuwa tumetia udhu,

 iii. Kuwahi katika eneo la tukio (chumba cha mtihani) ili kuyazoea mazingira ya eneo husika,

 iv. Kumtanguliza Mwenyezimungu kwa kusoma suratul fat-ha(quran)
 na suratul muadhwatain (falaq& nnasi) mwisho ni saratul ikhlas   ni vizuri idadi ya witri ikiwezekana.

v. Kumsabahi Mwenyezimungu kwa nyiradi mbalimbali (fupifupi). 

NAMNA YA KUFELI MITIHANI KWA MAKUSUDI 

1. Usiwe na ratiba ya mitihani pamoja na ya kujisomea.

2. Anza na swali usilolijua ambalo litakuchanganya.

 3. Kutotumia uwezo wako wote katika kulijibu swali ambalo unalijua.

 4. Kufanya swali ambalo huna uelewa nalo kabisa ni akheri usilifanye na uliache kwani utapolifanya utaonyesha udhaifu wako kwa wasahihishaji au ukitaka basi lifanye mwisho baada ya maswali yote unayoyafahamu kuyafanya. 

 5. We hisi kuwa ni vizuri kwa kutokuwa makini na muda, kwani waona kufanya mtihani kwa muda si sehemu ya mtihani.

6. Usiende maktaba kusoma wala kujikumbusha ulivyo soma darasani kwa muda wako wa ziada.

7. Usisome vitabu, wewe soma tu 'summary' za notes na kamusi ili ujue tu maneno magumu ya kuwatishia wengine kuwa wewe ni msomi na lugha ina panda kwa sana.


8. Kesha sana kila siku lala saa tisa usiku au kumi kabisa alfajiri wakati shule unatakiwa kuamka saa moja asubuhi kila siku.

9. Nenda club mara nyingi iwezekanavyo kama vipi kila siku ukiweza.

10. Kuwa mlevi na mwingi wa wanaume/wanawake wakati uko masomoni.


11. Ukipewa mtihani anza kufanya bila kusoma maelekezo kwanza.


12. Usisome wakati unategemea kufaulu mtihani kwa miujiza.

13. Usisikilize walimu wako au walezi/wazazi hususani kipindi mwisho, karibu na mitihani kama hiki.

14. Uwe mwenye kusoma kitu kipya (mada mpya) karibu na mitihani.

15. Uwe mpenda sifa, mjuaji wa kila kitu, majivuno ya kwenu mna pesa kufaulu sio ishu.

16. Mwalimu anapo fundisha usichukue notes kaa tu muangalie kama kideo na ongezea kusinzia ikibidi.Eti anatupotezea muda mitihani imekaribia.

17.Usijali alama unazopata katika mazoezi au mithani ya Majaribio mbalimbali, eti ukisema ‘after all is just a number!!

18.Waambie wenzio 'wametumwa na kijiji kuja kusoma ndio maana wanasoma sana' na wewe kusoma kwako sio ishu sana, after all ukifeli unaweza kuwa konda wa magari ya''baba/ mama, mjomba, shangazi, baba mdogo n.k''

19.Ukiwa katika mtihani wa usifanye yaangalie tu na hisabati soma kama notes usi kokotoe hata moja 'after all ni ugonjwa wa taifa'

20.Wakatishe wenzio tamaa ''kufauru masomo sio kufauru maisha'; ' wasomi mbona wengi halafu wote choka mbaya tu (kusoma sio dili) au mkubwa afeli bhana……..

21. Wewe toa mawaidha badala kujibu swali (Islamic knowledge).

22. Wewe jifanye walijua sana somo husika, hivyo utalifaulu tu (Islamic Knowledge).

MAMBO KUMI(10) YA KUZINGATIA YA WAKATI WA MAANDALIZI YA MITIHANI:

KWANZA: kuzingatia muda, si vema kukurupuka na kukimbizana nao na kujinyima usingizi wakati ratiba ya mtihani ilikuwa inafahamika na  ulikuwa na uwezo wa kujiandaa taratibu kuelekea kwenye siku
ya kutahiniwa kwako.

PILI: Jindae mwenyewe kwa kutafuta na kufanya mitihani iliyopita, huku ukinakili maswali ambayo watunzi wamekuwa wakiyarudia rudia kila mwaka.

Njia hii itakuwezesha kujiandaa kwa kuzingatia shabaha na mahitaji halisi ya maswali yatokayo mara nyingi kwenye mitihani. Hakikisha unapata mitihani ya nyuma ya ngazi uliyopo isiyopungua kumi au zaidi na uifanye huku ukihakikisha hakuna swali hata moja ambalo linakushinda.

Pamoja na ukweli kwamba ubahatishaji wa vitu si njia sahihi sana, lakini umeonekana kuwasaidia wale ambao ubahatishaji wao huambatana na umakini, hivyo mwanafunzi anatakiwa kuwa na tabia ya kubahatisha maswali ambayo anadhani mwalimu wake anaweza kuyatoa kutoka kwenye daftari lake na hivyo kujiandaa.

Ubahatishaji huu, lazima uambatane na kile nilichosema awali, yaani kuwa na kumbukumbu ya mitihani iliyopita. Wanasema watalaamu kuwa ulimwengu una tabia ya kurudia matukio, hivyo hata kwenye maswali kuna tabia hii ya kujirudia rudia.

TATU: Orodhesha maeneo yote ambayo huyaelewi kwenye mtihani hiyo ya nyuma na uyafanyie mazoezi kwa kupata ushauri kwa waalimu wako. Kama kuna mada ambazo hujazielewa kwenye daftari lako hakikisha muda uliojiwekea utatosha kuzielewa.

NNE:  Haifai mwanafunzi kukimbia ma
elekezo ya mwisho yanayotolewa darasani na mwalimu wako, kwani hayo ndiyo yatamuwezesha kufahamu kama umekamilika kwa kutahiniwa au bado kuna eneo linakutatiza.

TANO: Hakikisha kuwa kumbukumbu zako kichwani zinaongezeka kadiri unavyosoma, usiwe mtu wa kusahau sahau ulichosoma na ikiwezekana eneo ambalo unaonekana kulisahau ndilo ulipe kipaumbele cha kujikumbusha, ikibidi hata kila siku.

SITA: Angalia kwa makini alama zako za mitihani ya majaribio, ikiwa umepata alama za chini ujue kuna mahali panahitaji nguvu za ziada, shauriana na mwalimu wako maeneo yote unayokosa au yanayokusumbua kabla ya siku ya mtihani.

SABA: Iliuwe na uhakika wa kufanya vema mtihani wake anatakiwa kuzingatia dondoo zote zilizotolewa kwenye kipengele
cha kuimarisha kumbukumbu kichwani, ambazo zimo ndani ya kitabu hiki.

NANE: Wakati mwingine ni vema ukausikiliza mwili, si vema kuulazimisha kusoma hata kama unaona kuna udhaifu, baadhi ya wanafunzi hukesha wiki mbili mfululizo wakisoma, matokeo yake mwili na akili huchoka na kushindwa kupokea masomo vizuri. Muda wa kupumzika unahitajika.

TISA: Kabla ya mitihani unatakiwa kujiamini kwa kushinda hofu. Eneo hili ni muhimu sana kwani kuna wanafunzi hufeli si kwa
sababu hawakujiandaa, bali hukumbwa na hofu muda mfupi kabla ya kuanza mitihani. Hivyo ni muhimu mwanafunzi akaandaliwa kisaikolojia na waalimu pamoja na wazazi wake jinsi atakavyoweza kufanya mtihani bila hofu.

KUMI: Imani ni hitimisho la mafanikio ya mwanafunzi, haifai kuingia katika kipindi cha mtihani ukiwa na mawazo hasi. Kinachotakiwa ni ari ya ushindi au kwa lugha nyingine ni mawazo chanya. “LAZIMA NIFAULU MTIHANI HUU” Imani hii inaweza kujengwa na mtu kupitia kujiamini mwenyewe au kuamini kwa msaada wa nguvu za imani yake ya dini.

MBINU ZA KUFAULU KABLA  NA BAADA YA KUINGIA CHUMBANI CHA MTIHANI:

Kwanza unapaswa kuzingatia akilini kuwa unakabiliwa na mtihani, hivyo jikumbushe mambo yote uliyoelekezwa na mwalimu wako kuhusu mtihani, pili hakikisha kuwa unafahamu vema ratiba. Ukishaweka uzingativu, anza kupambana na hofu ambayo wengi huwa nayo siku ya mtihani. Jiambie kuwa unajiamini na utafanya vizuri mtihani wako. Epuka kuwaza kuwa mtihani utakuwa mgumu kwako.

Uone mtihani kama kitu cha kawaida na kitu ambacho kinakufanya upeo wako ukue na uelewa wako kuongezeka. Puuza hofu na vitisho vyote ulivyowahi kuambiwa juu ya mtihani.Ukiliweza hili taratibu utaanza kuona kujiamini kwako kunaongezeka.

Pia fahamu kuwa wewe si mtu wa kwanza kufanya mtihani kwani watu wengi walisha wahi kufanya mitihani na wakafaulu. Jiweke katika kundi la watakaofaulu vizuri na jiamini kuwa una uwezo huo. Siku ya mtihani amka mapema na anza kuandaa vifaa vyako vya kufanyia mtihani. Hakikisha una kalamu zaidi ya moja, rula, penseli, Mathematical set (mkebe) wenye vifaa vyote hasa katika masomo yanayohusisha hesabu na kuchora.

Pata kifungua kinywa chepesi, kama ni chai au chochote ulichozoea kula asubuhi. Epuka kula sana asubuhi kwani utaanza kusinzia kwenye chumba cha mtihani.

Kama unaishi mbali na shule,wahi kuondoka ili kuzuia vitu ambavyo vitakufanya uchelewe kwenye chumba cha mtihani kama foleni ya magari au umbali mrefu.
Hakikisha vifaa vyako vyote vimekamilika kabla ya kutoka nyumbani,mfano peni,penceli,mkebe,kitambulisho…..na vinginevyo vinavyohitajika kuingia navyo katika chumba cha mtihani.


Pia hakikisha una saa ili uweze kuutumia vizuri muda uwapo ndani ya chumba cha mtihani.
Wakati unaendelea kujiandaa, unaweza kuendelea kujikumbushia vitu vidogo vidogo katika notisi zako unavyohisi vinaweza kuwemo kwenye mtihani ingawa siyo lazima kama umejiandaa vizuri.


Epuka mazungumzo yoyote yanayohusu mtihani. Kaa mbali na watu ambao wanazungumzia mabaya kuhusu mtihani kwa mfano “ mtihani huu ni mgumu” au “wengi walifeli mwaka jana” kwani kauli kama hizi zitakufanya ushindwe kujiamini.

Kaa kimya muda wote na epuka sehemu zenye kelele. Endelea kujiamini kuhusu ufaulu na jinsi utakavyofurahiwa na wazazi wako baada ya majibu kutoka. Tafuta ushujaa kwa watu waliokusomesha, ingia kwenye mitihani kwa lengo moja tu la kuibuka mshindi na si mshindwa.

Jiamini kuwa ulichokisoma kwa siku zote ulizokuwa shule kinatosha kukufanya ufaulu. Epuka kusoma vitu vipya muda mchache kabla ya kuingiaItulize kabisa akili yako.

Zingatia sana usafi wa mavazi na mwili kwani ukiwa mchafu utakosa utulivu uwapo ndani ya chumba cha mtihani.

NDANI YA CHUMBA CHA MTIHANI
:

Hakikisha umeingia ndani ya chumba cha mtihani nusu saa kabla ya muda wa kuanza mtihani.Kama hamtaruhusiwa kuingia kabla, hakikisha upo jirani na chumba cha mtihani na unaelewa kila kitu kinachoendelea.

Endelea kutuliza akili yako na amini utafaulu kwa moyo mmoja. Tulia kimya ukitafakari namna utakavyoyajibu maswali kwa ufanisi.

Baada ya kuingia chumba cha mtihani na kupewa karatasi ya kujibia na karatasi ya maswali, endelea kutulia ukisubiri kusikia maelekezo kutoka kwa wasimamizi. Usikimbilie kufunua karatasi ya maswali na kuanza kujibu au kusoma kabla haujaruhusiwa kwani hilo ni kosa.

Hakikisha akili yako imetulia na wala usiwe na papara. Jiamini kuwa unaweza. Bila shaka utapewa muda wa kuanza kupitia maswali kabla ya kuanza kufanya mtihani. Utumie muda huo kusoma maelekezo ambayo yako juu ya karatasi (Instructions).

Soma kwa makini maelekezo yote na hakikisha umeyaelewa vizuri na ikiwezekana rudia kusoma kwa mara ya pili. Baada ya Kuhakikisha umeelewa vizuri maelekezo yote, anza kuyasoma maswali kabla ya kuanza kuyajibu. Elewa ni maswali yapi ni lazima kuyajibu (compulsory), fahamu mtihani una maswali mangapi jumla na fahamu kila swali lina maksi ngapi.

Hakikisha umeyasoma maswali yote, la kwanza mpaka la mwisho na weka alama kwenye maswali unayoyafahamu vizuri. Ukishayasoma yote, panga muda utakaoutumia kujibu kwa kila swali kutegemeana na uzito wa swali. Ukishamaliza sasa unaruhusiwa kuanza kuyajibu. Anza na yale unayoyajua vizuri kwani kwa kufanya hivyo utajikuta kujiamini kwako kukizidi kuongezeka.

Epuka kuanza kujibu maswali unayoyaona ni magumu kwako. Anza na yale mepesi kisha ndiyo uendelee na yale magumu.Utajikuta ukiufurahia sana mtihani wako na hofu itaisha kabisa. Hakikisha unafikiria kwa makini kabla ya kujibu swali lolote hata lile unaloliona ni jepesi.

Zingatia kuandika majibu yako kwa mwandiko unaosomeka vizuri ili msahishaji avutiwe na kazi yako. Hakikisha pia umeandika namba ya kila swali ulilolijibu. Hakikisha unajibu maswali kulingana na jinsi ulivyoulizwa. Ukiambiwa jibu kwa herufi (Multiple choice) basi fuata maelekezo. Kama umeambiwa jibu Kweli au si kweli ( True and False) fuata maelekezo kwa makini, usiweke manjonjo sana unaweza kupoteza maksi.

Namna ya Kuyapokea Matokeo:

      Matokea ni zao au chumo ambalo hutokea baada ya kufanyika kwa jambo fulani ,hivyo machumo yaweza kuwa ni kuridhisha au kutoridhisha. Hivyo matokeo ya mitihani yetu yaweza kuwa ni mazuri , ya kati na kati au yasiokuwa mazuri.

              i.            MATOKEO MAZURI:

    Hayo ni matokeo ambayo mtu huyapata yakamuwezesha yeye/wewe kwenda katika ngazi ya juu ambayo anaitarajia/ unatarajia.
       Watu wengi wapatapo matokeo mazuri hupata kiwewe kutokana na furaha waliyonayo na kukurupuka na kushindwa kufanya uamuzi uliosahihi.La umuhimu nikumuomba Mwenyezimungu na kumshukuru na kutafuta ushauri kwa wale walio juu yako ni lipi la kufanya kabla ya kufanya uwamuzi. 

            ii.           Kati Kati:

      Haya ni matokeo ambayo mtu hupata alama/matokeo mazuri lakini kutokana na alama hizo hazikumuwezesha yeye kupata kuisoma kozi ambayo ameitarajia. Mfano mtu ambaye amepata gredi ya tatu (Division iii) na ametaka asome udaktari (medicine) .Ni ngumu kupata kozi hiyo lakini kuna baadhi ya vyuo ambavyo anaweza kupata chuo kutokana na alama hizo. Hivyo basi ni uzuri kutafuta ushauri kupitia wanafunzi/waislam walio vyuoni ili kuweza kumshauri cha kufanya.

            iii.       MABAYA (YASIYORIDHISHA)

       Haya ni matokeo ambayo hayatamuezesha mtu kujiunga, kuingia elimu ya juu (vyuo) katika kiwango cha shaada(degree) maranyingi watu hawa huwa ni wenye kukata tamaa na wengine kuamua kurudia mtihani ili waweze kufaulu hali yakuwa kuna njia nyingine (mbadala) ambazo wanaweza kupitia na kufikia malengo yao mfano ASTASHAHADA (CERTIFICATE), STASHAHADA (DIPLOMA), na hatimae kufikia SHAHADA (DEGREE) na kisha kuendelea ngazi au kiwango cha juu zaidi kielimu.

USHAURI.

Nisingependa kumshauri mtu arudie mtihani kwa maana utafiti umeonyesha kuwa wengi wanaorudia mtihani hawafanyi vizuri.
Lakini kwa wenye kuamua mitihani yawapasa wafanye yafuatayo kwanza:
1.      Kufanya tathmini ya kina sababu zilizopelekea matokeo yake kuwa hivyo
2.      Je sababu hizo zinatatulika kirahisi
3.      Basi atatue matatizo hayo ndio aweze kurudia mtihani
Miongoni mwa sababu zinaweza kuwa;
a) Sababu za ndani/binafsi (internal factor)
b) Sababu za nje (external factors)
   Sababu zote hizi mwisho wa siku huchangia katika kuleta matokeo ama mazuri au mabaya, zinaweza kuwa za kiuchumi, kifamilia, kimazingira, kijamii au kitaasisi (shule).
      Baada ya kutatua hizo sababu tunaweza kukubaliana na wewe katika mawazo yako ya kurudia mtihani wako.

*********  Wabillah Taufiq **********

Brother Mussa Khaini akiwa anatoa mada kuhusiana na mambo ya kujiandaa kisakolojia kwa Mtahiniwa kabla ya Mithani ya kidato cha Sita.



Brother Nassoro nae alikuwa ni kati ya watoa mada kwa wanasemina,hapa akiwa anasisitiza jambo kutokana na mada yake ya "maisha baada ya mitihani"



 


Pichani vijana wa kidato cha sita kutoka shule mbalimbali zamjini mbeya wakifuatilia mada zilizokuwa zinatolewa,huku wakiwa wanachukua nukuu kwa yanayozungumzwa,tayari kwa utekelezaji wa kivitendo.

 Nje maandalizi ya WALI MAUA......uliendelea ili vijana wapate chakula cha mchana mara baada ya Semina.


"Dahhhh.......WALI MAUA tayari, sasa itakuwaje hapa......ebu ona kitu cha njano katika sufuria...... "    ndivyo anvyoonekana akisema ustadh Yusufu(mwenye kanzu)huku bibi harusi mtarajiwa(Zainabu Kalulu) akifurahi.......dada shamila na Ajuna wakifuatilia kinachoagizwa na kiongozi mwenzao.



 
Japo tupo jikoni je tutakula leo jamani.....????? ndiyo tafsiri zinazoenekana kwa picha mbili hapo juu...kwa maustadh wakiwa katika pozi tofauti ili muradi mambo yaende sawa kwa shughuli za jikoni na maandalizi mengine ya nje ya chumba cha semina. 






 Hatimaye paliliwa......!!!! wanasemina na watoa mada wakiwa katika makundi tofauti...walipata chakula cha mchna kwa pamoja.......WALI MAUA wenye Radha ya Pwani uliliwa......Mashaallah......!!!!!
Raha ya mchele sharti uvulie viatu.......na pia maji ya MBEYA SPRING WATER nayo yafuatieeeee......!!!!ni baadhi ya majukumu yaliyofanywa na Maustadh pichani......hakika ilikuwa rahaaaaaaaaa.

"......Rahaaaaa.......ya mchele Brother Jaribu ni sharti na ni lazima ukalie katika majaniiiii.....pia ni lazima sharti kanzu uipandisheeeee....." 
ndivyo anavyoelekea kuyasema Brother Amour na Ridhiwan mara baada ya kufanya kazi ngumu sana ya kuwaleta pamoja vijana wa kidato cha sita na kufanikiwa kwa Semina. 



 Wacha ninawe mie.......!!!!vijana wakiwa wanaosha mikono yao tayari kwa safari ya kurudi makwao.

Friday, January 25, 2013

Kisa chenye Wosia Kwa Dada Zetu:MOLA WAKO MLEZI ATAKUPA MPAKA URIDHIKE:












Baada ya kumaliza masomo yangu ya chuo kikuu nilipata kazi nzuri sana.
Wachumba wakaanza kuja kunichumbia.Lakini hakuna niliye ridhika nae ili awe mshirika wangu wa maisha.
Kisha baada ya hapo nikashughulishwa sana na kazi mpaka nikasahau kabisa masuala ya ndoa.
Mpaka nikafikia umri wa miaka thelathini na nne.Nikaanza kupata shida kutokana na kuchelewa kuolewa.

Siku moja akajitokeza kijana mmoja kunichumbia, na alikuwa akinizidi kiumri kwa miaka miwili.
Hali yake ya kimaisha ilikuwa ni mbaya lakini niliridhika nae juu ya hali hiyo.
Tukaanza maandalizi ya ndoa,akaniomba fotocopy ya kitambulisho changu,nikampatia.
Baada ya siku mbili mama yake akanipigia simu, akanitaka nikutane naye haraka kadri iwezekanavyo.
Nikaelekea nyumbani kwake,ghafra nikashangaa ananitolea ile fatocopy ya kitambulisho changu.
Akaniuliza:Hivi tarehe ya kuzaliwa katika kitambulisho
chako ni sahihi?!
Nikamjibu:Ni sahihi.
Akasema kwa hiyo wewe wakaribia miaka arobaini?!
Nikamwambia mie nina umri wa miaka thelathini na nne.
Akasema:Hakuna tofauti wewe ushavuka miaka therathini,
na matarajio ya kuzaa ni madogo sana,na mie ninataka kuwaona wajukuu.

Mambo hayakutulia mpaka uchumba wetu ukavunjika.Ukapita muda wa miezi sita ambayo ilikuwa ni migumu sana kwangu.Nikaamua nielekee Umra katika nyumba tukufu ya Allah, ili niweze punguza fikra na mawazo.

Nikaelekea katika nyumba tukuf ya Allah(Masjidi al haraam).
Nikawa nikiswali hali ya kuwa ni mwenye kulia nikimuomba Allah na kumshtakia anifanyie wepesi na ajaalie kheri juu ya suala langu la ndoa.
Pindi nilipo maliza kuswali ,nikamuona mwanamke mmoja akisoma Qur ani kwa sauti nzuri.
Alikuwa akiirudia rudia na kuikariri aya isemayo:
(Na fadhila za Mwenyezi Mungu zilizo juu yako ni kubwa sana)
Surat Nisaai:113
Nikajikuta machozi yakinidondoka.Yule mwanamke akanivuta karibu yake,akawa akiirudia rudia kauli
yake Allah: ( Na Mola wako Mlezi atakupa mpaka uridhike) Surat Dhuha:5
Wallahi ilikuwa ni kama vile mara yangu ya kwanza ninaisikia ayah hii, nafsi yangu ikatulia,nikamaliza ibada yangu ya Umra,nikaamua kurudi nyumbani. Karibu yangu katika ndege kulikuwa na kijana wa kiume.
Ndege ikafika uwanjani nikashuka. Nikashangaa kumuona mume wa rafiki yangu akiwa
katika ukumbi wa mapokezi.Nikamuuliza ni nini kilicho kuleta uwanja wa ndege?
Akanijibu ya kwamba anamsubiri jamaa yake ambaye anaingia na ndege inayo ingia muda ule ule nilio ingia mimi.
Haikupita dakika yule rafiki yake akawa ashafika.Kumbe alikuwa ni yule kijana ambaye alikukwa karibu yangu katika siti. Kisha nikaondoka pale nikiwa na baba yangu.
Haukupita muta mrefu baada ya kufika nyumbani kubadilisha mavazi yangu na kupumzika kiasi,rafiki yangu akanipigia simu. Akanieleza ya kwamba rafiki wa mume wake kapendezwa nami na anataka kuja kunichumbia. Nilifurahi sana!nikahisi huenda Allah kanijaalia faraja baada ya tabu ya muda mrefu.
Baada ya siku kadhaa wakaja nyumbani kunichumbia kwa baba yangu. Haukupita muda mrefu mpaka tukawa tushafunga ndoa.

Tukaanza maisha ya ndoa yenye upendo na furaha.
Niliyapata kwa mume wangu yale yote ambayo nafsi yangu ilikuwa
ikiyatamani kuyaona kwa yule atakaye kuwa mshirika wangu wa maisha,
miongoni mwa upendo,huruma na wema
juu ya familia yake na familia yangu.
Isipokuwa miezi ilikuwa ikipita hali ya kuwa
hatuoni alama zozote za ujauzito.
Nikapatwa na mfadhaiko sana juu ya suala hili,
khususani ukichukulia ya kwamba muda huu nilikuwa
nishafikisha umri wa miaka thelathini na sita.
Nikamtaka mume wangu tuelekee hospitali nikapime,
nikikhofia huenda fursa yangu ya kupata watoto ikawa ndio ishapita!
Tukaelekea kwa daktari anayehusika na magonjwa ya
wanawake nikapata vipimo.

Baada ya kuanza kupata majibu ya kipimo cha kwanza kabisa,
daktari akasema:Hakuna haja ya kuendelea na vipimo,hongera dada
unaujauzito!
Tulipatwa na furaha isiyokuwa na kifani.
Ujauzito ukaendelea kukua salama,ingawa nilikuwa nikipata
shida kutokana na ukubwa wa tumbo,kila nilipo mweleza daktari
juu ya tatizo hilo aliniambia nisiwe na khofu
kwani hali hii ni kutokana na kuchelewa kwangu
kupata ujauzito mpaka nimefikia umri wa miaka thelathini na sita.

Sikutaka kupata vipimo ili kujua ujauzito wangu
ni wa mtoto wa aina gani,kwani mtoto wa aina yoyote yule
niliye andikiwa ni kheri kwangu.
Ukafika wakati wa kusubiri kujifungua na nikajifungua salama.
Baada ya kuzindukana, daktari akanijia hali ya kuwa ni mwenye
kutabasamu.Akaniuliza:ulikuwa ukitamani kupata mtoto wa aina gani?
Nikamjibu:Mie nilitamani Allah aniruzuku mtoto pasina ya kujali mototo huyo ni wakiume au wa kike.
Akaniambia:waonaje nikikwambia umejaaliwa kupata
Hasani,Husaini na Fatuma?!
Sikufahamu lolote nikamuuliza:wakusudia nini???
Nikashangazwa pindi alipo nieleza hali ya kuwa akinituliza,
Mwenyezi Mungu mtukufu kanipatia neema ya watoto
watatu! Kana kwamba Allah alijaalia wale watoto nilio tarajia kuwapata
ndani ya umri wangu wote niwapate kwa mara moja,hii ikiwa ni rehema kutoka Kwake!
Nikadondokwa na machozi ya furaha nikasema:
( Na Mola wako Mlezi atakupa mpaka uridhike)Surat Dhuha:5
************************************************
Hivi ndivyo ilivyo mipango ya Allah,usikate tamaa.
Matendo ya Allah juu yetu yote ni kheri,hatuna budi kusubiri
na kuridhika na hukumu yake.Yeye anajua hali za waja wake
na hakuna mwenye huruma juu yetu kulikoni Yeye.
Tumuabudu yeye peke yake tutekeleze amri zake
na tushikamane na dini yake.Ahadi yake ni ya kweli.
Hivi pasina ya mitihani mbali mbali katika maisha
angejulikana vipi yule mwenye imani thabiti na mwenye imani dhaifu?
Angejulikana vipi yule mwenye subira na asiye kuwa na subira?
Ili kila mmoja alipywe kutokana na matendo yake???!
(Hakika wenye subira watalipwa ujira wao bila ya hisabu)
Surat Zzumar:10.
Kwa hiyo suala la kuchelewa kupata mume lisikupelekee kufanya mambo
ya haramu,lisikupelekee huhalalisha ndoa ambazo Allah kaziharamisha,
subiri kuchelewa kupata mume ni moja ya mitihani ya Allah,Nae atakulipa
kutokana na subra yako malipo pasina ya hesabu.Hii ni Ahadi ya Allah
kama tulivyo ona katika aya.Waonaje laiti kama tajiri fulani,mkarimu,
mwadilifu na mpole atakuahidi kukupatia ujira juu ya kazi yako nzuri
uliyo ifanya, je utakuwa na wasi wasi juu ya tajiri huyu mkarimu mwadilifu
na mpole katika kukulipa ujira wako???
Nadhani hatuto tofautiana katika jibu ya kwamba:Hapana.
Sasa vipi ahadi ya Allah ambaye si mwenye kukhalifu ahadi yake,
tajiri wa matajiri,mkarimu wa wakarimu,mwadilifu wa waadilifu,
mmiliki wa kila kitu,atakalo huwa na asilo litaka haliwi???

Dada yangu mpendwa !!!
Vyovyote vile hali itakavyo kuwa usikubali
kuwa mja wa shetani,usikubali kuuza
maisha ya akhera,maisha ambayo neema zake
hakuna macho yaliyo ziona,wala masikio yaliyo
zisikia wala hazijawahi fikiliwa na yeyote,
yaani vyovyote vile utakavyo fikiria juu ya uzuri wa pepo hii ambayo Allah kawaandalia viumbe wake wema,huwezi kupatia.Nursa ya Mwenyezi Mungu ipo karibu nawe.
Usikate tamaa.Kukataa tamaa si katika sifa za waumini