FALSAFA YA MWEZI MTUKUFU WA RAMADHANI
.
Kwa
Kuhusiana na mwezi huu mtukufu wa Ramadhani, Mimi ninapenda kuwaambieni baadhi
ya mambo yaliyo muhimu kwa sababu sisi ni miongoni mwa wale watu waliobahatika
kupata fursa hii kwa mara nyingine tena hata bila ya kumuomba Allah Subhanahu
wataala. Kwa mara nyingi, mwanadamu hawezi kukadiria kiasi cha fadhila
alizojaaliwa na Mwenyezi Mungu kwa sababu ya kutokujua umuhimu wake, na
vilevile hawezi kushukuru neema hizo wala kufaidika na fursa hizi ambazo
amefunguliwa njia zake. Kwa upande mwingine kanuni za fursa nazo ni za aina
pekee kama vile ilivyooelezwa katika riwaya mbali mbali kuwa fursa zinakuja kama mawingu na kuondoka vivyohivyo. Fursa hizo
hazisubiri wala kumbishia hodi mtu mlangoni mwake mara kwa mara, na hazirejei
tena. Wanadamu maishani mwao kwa mara moja au kwa baadhi ya nyakati huwa
wanabahatika kupata fursa kama hizo, na kwa hivyo
inawabidi wawe wenye kushukuru kwa neema hizo. Na inawabidi kukaribisha neema
hizo, na kuzikumbatia na vilevile kushikamana nazo. Kwa hakika kwa lenyewe,
maana ya fursa na tawfiq inahitaji pia kuangaliwa. Ama kwa wakati huu,
inatubidi sisi tuelewe kwamba mwezi huu mtukufu wa Ramadhani ni miongoni mwa
fursa nyingi kubwa ambazo Allah swt. Ametuzawadia.
Kwa
hakika hili siyo jambo dogo kuwa maisha yetu kwa kipindi cha mwaka mzima
yamepita na tumeweza kuingia kipindi hiki cha mwezi mtukufu wa Ramadhani mwaka
huu. Chcochote kile ambacho Qur’ani tukufu imezungumzia kuhusu mwezi huu
mtukufu wa Ramadhani kwetu sisi tunaelewa vyema na taswira ambayo Qur’ani
tukufu imetuwekea katika akili na fahamu zetu ni kwamba:
“Shahru Ramadhanalladhii anzala fihil Qur’aan Hudalinaasi wabayinatim
minal huda walfurqan.”
Mwezi
huu Mtukufu ni mwezi uliyoteremshwa Qur’ani Tukufu kama mwongozo wa wanadamu. (Surat
Al-Baqarah; 2:185) Hakika katika Mwezi huu mtukufu Qur’ani Tukufu
iliteremshwa kama kuwaongoza wanadamu
Qur’ani
Tukufu inazungumzia kuwa mwezi huu ni wa kuteremshwa Qur’ani tukufu. Na
katika riwaya inapatikana kuwa mwezi huu mtukufu wa Ramadhani unaitwa Rabiul
Qulub, yaani ni mwezi wa machipuo kwa ajili ya mioyo. Vile mchipuo unavyokuja
ardhini, ndivo hivyo hivyo mioyo yetu inavyokuwa katika hali ya mchipuo.
Ni Kipindi au msimu wa mchipuko siyo kwa majina tu ya kubadilika kwa
kubadilika usiku na mchana. Kwa hakika wenyewe tunaona na kushuhudia kuwa
katika msimu huo hali ya ardhi inakuwa katika sura tofauti kabisa na
misismu mingine.
Katika
hali hii tunaona ghafla kwa kudra za Allah Subhanahu Wataala kuwa ardhi ambayo
ilikuwa ni ngumu, kavu, tasa, iliyogeuka kuwa jangwa, ikawa ya mchanga,
ilikuwa ya mawe na ambayo haikuwa na maji, sasa inageuka kuwa ardhi laini
ambapo tunaona majani na mimea na maua
vinachipua.
Katika
mmojawapo ya miujiza ni kwamba hakuna mtu ambaye anatifua au kulima
katika ardhi hiyo lakini zile mbegu zilizokuwa zimefukiwa ambazo zilikuwa
zimeshakufa tunaona zinapata uhai na kuchipua. Sisi sote tumeona vile majani na
mimea inavyochipua kutoka ardhini na inaota na kutoa maua na kutoa mbegu na baada ya hapo tunaona
miche na miti hiyo inakauka na huku mbegu zake zinakuwa zimefukiwa kwenye
ardhi. Kwa kipindi chote cha mwaka mzima kwa vipindi mbali mbali vya kiangazi
kipupwe n.k. mbegu inakuwa imebakia imejificha ndani ya ardhi na inapofika
msimu wa kuchipua inajichipua na ndiyo kumaanisha kuwa mbegu hiyo inakuwa
imehifadhika katika hali yake ya kuwa imekufa ndani mwa ardhi. Kwa
hivyo unapowadia wakati wa kuchipua mbegu hiyo ambayo ilikuwa imekufa kwa
kipindi chote hicho inaanaza kuota na kutoa majani na hivyo tunaona ardhi
inakuwa kijani. Kwa amri za Allah Subhanahu Wataala ardhi inageuka kuwa
laini. Na hivyo kuwa na uwezo wa kuipokea kwenye udongo wake ile mbegu iliyopo
na kuipa uwezo wa kupitia hatua mbalimbali na hadi kufikia kuwa rangi ya kijani
kwa kuipatia uhai. Na kwa amri za Allah inapotoa majani inatokezea nje ya
ardhi, na hapo inakuwa katika mmea ambao unatoa maua na vilevile kufikia hatua ya kutoa
matunda. Kwa hakika mandhari hii inakuwa ni nzuri sana na ya kuvutia! Matunda yanavyokuwa
matamu tunayaelewa na manukato ya matunda hayo yanavyokuwa mazuri tunayaelewa.
Kwa kifupi tumeona kuwadia kwa msimu wa mchipuo wa mbegu iliyokuwa imekufa
kutokea ardhi ambayo nayo ilikuwa imekufa, sasa inaanza kuchipua na hapo ndio
tunaona muujiza mkubwa wa Allah Subhanahu Wataala ukiwa dhahir na bayana mbele
ya mwanadamu.
Imeelezwa
katika riwaya mbali mbali kuwa mwezi mtukufu wa Ramadhani ni mchipuo wa mioyo
na vile vile mchipuo wa Qur’ani tukufu. Hii inamaanisha kwamba moyo ambao
tunaodhania kuwa uko katika vifua vyetu sivyo hivyo, si moyo ule ulionyuma ya
mapafu, bali ni moyo ule ambao ni nafsi zetu. Na ambao kwa hakika ndiyo
moyo wa hisia wa mwanadamu. Hata hivyo moyo huu wa nafsi, unapitia katika
vipindi mbalimbali. Vipindi vya machipuo, kiangazi, masika nk. Bila shaka
wengi tutakuwa tumeshaona vile ardhi inavyoonekana katika kipindi cha baridi,
wakati ambapo hewa baridi ipo na unakuta maji yanakuwa yemeganda na barafu
inadondoka. Na katika hali hii vitu laini vinaganda na kuwa vigumu na
vivyohivyo ndivyo moyo wa mwanadamu unakuwa hivyo. Kuna baadhi ya nyakati
katika maisha ya mwanadamu ambapo moyo wake unakuwa umeganda kama
vile barafu inavyoganda. Hivyo katika hali hiyo kumkumbuka Allah Subahanahu
Wataala kunakuwa ni kugumu sana kwa moyo kama huo. Ndio maana baadhi ya nyoyo zinakuwa zimekufa kama miche na mimea inavyokufa katika nyakati mbalimbali
katika mwaka. Na hivyo moyo kama huo haukubali
kuongozwa. Ili kutaka moyo huo uwe katika hali
nzuri na ya kuweza kuchipua na kuzaa majani na matunda mazuri basi moyo huo wa
mwandamu ambao unasemwa kuwa Kalbul-Mu’min ashurihaman, na hivyo ndiyo
maana Allah Subhanahu Wataala ameuweka msimu huu wa mwezi mtukufu wa Ramadhani
ili nyoyo zetu ziweze kuchipua. Kuja kwa mwezi mtukufu wa Ramadhani pasi na
kufanya yoyote mioyo yetu inakuwa laini. Tumeona siku moja imepita na
hata siku ya leo imetupita na hali ya siku iliyopita yaani jana na hali ya siku
tuliyopo leo ni tofauti. Ingawaje jua na mwezi vinachomoza na kuzama kama
kawaiada na usiku na mchana inakuwa sawa lakini leo tunakuwa na hisia yenye
nguvu na ya aina pekee. Leo tunakuwa na mtazamo ulio wa kitayari,
matayarisho tofauti kabisa na yale tuliyokuwanayo siku iliyopita. Na tunaona
kuwa nyoyo zetu zinakuwa tayari kupokea jambo fulani na vilevile zinatafuta
jambo fulani.
Nuzul
ya Qur’ani tukufu si jambo la kufikiria au kudhania au kama
vile tunavyofikiria sisi kwa kawaida. Iwapo kutakuwa na majaaliwa Inshallah
tutalizungumzia swala hili kwa mapana zaidi katika nyakati nyinginezo. Kwa
hakika sisi tunavyolifikiria suala hili la Nuzul ni kwa kile tunachokiona,
yaani kwa kitu chenyewe na kuteremka kwake kidhahiri, kama
vile kitu kilichopo juu ya paa la nyumba yetu kikija chini au tone la mvua
linalodondoka kutokea mawinguni, ndio hapo tunaposema kitu fulani
kimeteremka yaani kimekuja chini. Sisi tunachukulia kuteremka kama
vile kitu kinatoka juu kuja chini kwa mfano kunapokuwa na ile lift katika jengo
inapoteremka kutoka juu kuja chini tunasema hiyo imeteremka. Kwa hakika fikra kama hii haiwezekani kuzungumziwa kwa ajili ya Qur’ani
tukufu. Qur’ani haijateremka katika sura kama
hii tunavyoielewa, yaani katika sura fulani au ilikuwa katika mbingu ya saba
sasa ikaja chini kwani mbingu ni juu na ardhi ni chini ndio maana tukasema
inateremka, sivyo hivyo. Kwa hakika sivyo hivyo kabisa, kwa hakika Qur’ani
tukufu ni nuru, mwongozo na vile vile ni neno la Allah Subhanahu Wataala. Kamwe
haikuwa katika sura ya kitu fulani kabla au baada yake. Kama
kuna mahala ambapo ni nafasi ya Qur’ani tukufu, basi si katika sura ya
kitu fulani au katika hali fulani na nafasi yake ni katika nyoyo zetu. Moyo wa
mwanadamu ndio nafasi ya Qur’ani tukufu.
Maana
ya kuteremka ni kwamba Qur’ani ilikuwa katika hali ambayo mwongozo huu, hidaya
hii ya Mola Wetu ilikuwa katika hali ambayo sisi hatuwezi kuifikia. Na ilikuwa
ni nje ya uwezo wa uelewa wetu. Qur’ani tukufu ilikuwa katika ‘Lawhi
Mahafudh’. Lawhi Mahafudh siyo jina la kitu au chombo fulani kama vile tunavyoona fremu za mbao au fremu
zilizotengenezwa kwa mawe. Kamwe hatuwezi kusema ni kitu kinachoshikika. Lawhi
Mahafudh ni mahala au hadhi. Katika kuumbwa kwa ulimwengu mzima ni mahala pamoja
na Qur’ani nafasi yake ndio hiyo ambapo sisi daraja letu ni la chini kabisa kama vile Qur’ani tukufu inavoelezea “
“Asfala
Safilini.” (Sura ya 95: Aya 5)
Sasa
wakati Qur’ani tukufu ilipokuwa katika hali iliyoifadhiwa kwa hiyo haikuwa
wepesi kwetu sisi kuelewa kwani sisi tukiwa katika daraja la Asfala Safilin.
Sasa kile ninachowaambieni mimi kuwa Qur’ani haikuwezekana kueleweka,
haimaanishi kuwa Qur’ani tukufu ilikuwa ni jambo moja lililogumu kabisa nje ya
uwezo wetu, au Qur’ani ilikuwa na maajabu yasiyoeleweka au kulikuwa na matatizo
ndani yake, laa, bali Qur’ani daima imekuwa ndio mwongozo wetu na ndio
iliyokuwa ikituongoza katika kila jambo na daima imekuwa ikituita sisi katika
kutuongoza na daima imekuwa jambo moja lililo wazi na lililo bayana na
lililokuwa limefunguka vizuri kwa kueleweka kwa ukamilifu. Lakini swala
lililopo hapa ni kwamba uwezo wa wale waliotaka kuielewa umekuwa na mipaka
yake, nafasi zao zimekuwa ni za chini kabisa, uelewa wao pia ni mdogo sana hivyo hawawezi
kuielewa Qur’ani tukufu kwa ukamilifu. Kwa mfano, iwapo kutatolewa mhadhara wa
kitaaluma fulani wa hali ya juu kwa mtoto mdogo basi itamaanisha kuwa
unazungumzia jambo moja lililo na mafumbo mengi taabu na lisilo wazi kueleweka
kwa mtoto huyo. Ingawaje wewe unalolizungumzia liko wazi kabisa bayana lakini
kwa upande wa pili msikilizaji wako ni mtoto kwani yeye anao upeo mdogo wa
kuelewa. Wewe jambo unalolizungumzia ni la hali ya juu kabisa wakati yule
anayekusikiliza anao upeo mdogo sana
wa kuelewa. Vile vile baadhi ya nyakati inaelezwa kuwa wakati mtu anapozungumza
jambo lenye elimu ya hali ya juu basi miongoni mwa wale wasilikilizaji wanasema
kuwa jambo unalolizungumzia ni la hali ya juu sana ambalo liko nje ya uwezo wetu wa kuelewa
hivyo tunakuomba kidogo urahisishe lugha yako ili watu waweze kukuelewa vyema.
Ndivyo
hivyo hivyo ilivyo maana ya Nuzul, yaana kwamba hadi katika hali ya
sasa hivi ipo katika hali ambayo inaweza kueleweka vyema kabisa kwa wale wenye
upeo mdogo wa kuelewa. Qur’ani tukufu imejaribu kuelezea kila jambo kiasi
kwamba kila mtu anaweza kulielewa vyema na kwa hivyo ndio maana inaelezwa kama nuzul (kuteremka).
Kwa
hakika Qur’ani imekuwa katika hali ya upeo mkubwa kabisa wa juu wa kueleweka,
kama haingekuwa katika hali liyopo ya sasa hivi basi ingelikuwa ngumu sana kuielewa. Na hii
ndio maana ya nuzul ya Qur’ani tukufu, yaani kuwepo katika hali ambayo tunaweza
kuielewa vyema au tukawa na uwezo au upeo wa kuielewa hiyo. Na pale Qur’ani
inapokuwa katika hali ya kuweza kueleweka, basi kwa ulimi wetu tu hatuwezi kuielewa
Qur’ani tukufu, au kwa kuisikiliza tu hatuwezi kuielewa Qur’ani tukukufu. Kwa
hakika mahala ambapo Allah Subhanahu Wataala ametujalia sisi kuielewa Qur’ani
tukufu ni katika kalb yaani moyo wetu. Lakini katika kalb hii, misimu
mingi inapitia na mavuno ya aina nyingi yanapitia humo, na sura mbali mbali. Na
baadhi ya nyakati moyo huu unakuwa mgumu kabisa kama vile inavyosema pale, “kal
Hijara au ashadu kaswatan” baadhi ya nyakati inakuwa kama
jiwe, na hata kuzidi ugumu wa jiwe. Baadhi ya nyakati moyo huu unakuwa, “Bal
Alahah Kulubu Atfaluha” yaani ikimaanisha baadhi ya nyakati nyoyo zinakuwa
kama zimefungwa kwa kufuli, na baadhi ya
nyakati moyo wetu unakuwa na machafu au uchafu.
Kwa
mujibu wa maelezo ya Qur’ani tukufu, ”Rain ala Kulubihim”, yaani baadhi
ya tabaka za uchafu zinakuwa zipo juu ya nyoyo zetu. Nyoyo zao zinakuwa
zimefungwa kwa mihuri na Allah Subhanahu Wataala ”Khatamalahu Alakulubihim,”
Nyoyo zilizopigwa mihuri. Yaani ni kwamba, baadhi ya mioyo ni mawe, na baadhi
ya mioyo ni migumu kuliko hata mawe, baadhi ya mioyo inakuwa imefungwa, na
baadhi ya mioyo inakuwa imepigwa mihuri kabisa, na baadhi ya mioyo inakuwa
imeishaanza kuwa na uchafu, na baadhi ya mioyo inakuwa na tabaka za maovu mbali
mbali. Sasa kwa kutaka nyoyo hizi ziwe zimejihusisha na Qur’ani tukufu, ili
kuzileta nyoyo hizi karibu na Qur’ani tukufu, Allah Subhanahu Wataala ndio
ametujalia neema hii kubwa ya mwezi huu mtukufu wa Ramadhani. Bila ya sisi
kusema, kwa kutambua tu haja zetu, Allah Subhanahu Wataala ametujalia muhula huu.
Mwezi huu mtukufu wa Ramadhani ni mwezi wa kuchipua kwa mioyo. Hii inamaanisha
kwamba mioyo ambayo ilikwisha kuwa migumu, migumu kuliko hata mawe au mioyo ile
ambayo imekwisha fungwa na kupigwa mihuri, basi mioyo yote hiyo katika mwezi
huu mtukufu wa Ramadhani inalainika. Huu ni msimu wa kuchipua na katika
kila hali ya ardhi inakuwa laini. Lakini iwapo ardhi hii itawekwa vile ilivyo
bila kuzalisha chochote wala kupanda mbegu yoyote au kumwagia maji au kwa
kujali basi daima itabakia ardhi iliyokufa kama
vile itakavyokuwa imetangulia. Msimu wa kuchipua utakuja na utakwenda lakini
ardhi hiyo itabakia ngumu na yenye mawe tupu. Kwa hivyo kuna haja kwetu sisi
kuifanya ardhi hii iweze kulainika, inatubidi tuitayarishe tupande mbegu
tuimwagilie maji na kupanda kitu chochote katika ardhi hiyo. Ndipo hapo ardhi
hiyo itakuwa ina rutuba na yenye kuzaa matunda. Kwa hakika ardhi hii ni ngumu
kabisa na kwa upande mwingine ni msimu wenye maajabu, na msimu wa
machipuo, mbegu yoyote utakayoipanda ndani yake itaota yaani itazaa matunda. Na
kwa maana hii Allah Subhanahu Wataala ndipo alipouzungumzia mwezi huu mtukufu
wa Ramadhani kama ni mwezi wa nuzul ya Qur’ani
tukufu.
Kwa
hakika swaum ndio mojawapo ya nguzo muhimu ya mwezi huu mtukufu wa Ramadhani.
Ukuu na hali ya mwezi mtukufu wa Ramadhani si kwa sababu ya kufunga swaumu,
bali utukufu na ukuu wa mwezi mtukufu wa Ramadhani ni kwa kutokana na Qur’ani
tukufu. Kwa hakika swaum inakuja katika nguzo mojawapo. Ni utaratibu wa mwezi
huu mtukufu wa Ramadhani kwamba tufunge swaum katika mwezi huu. Na mtu
yeyote ambaye hafungi swaum katika mwezi huu mtukufu wa Ramadhani basi mtu huyo
hana adabu nzuri. Na vile vile haimaanishi kuwa mtu yeyote anayefunga katika
mwezi huu mtukufu wa Ramadhani ataweza kubarikiwa baraka zote za Qur’ani tukufu,
au kujipatia baraka zote za mwezi mtukufu wa Ramadhani kwa kufunga swaum moja
tu! Kwa hakika swaum inaifanya mioyo yetu kuwa milaini. Na vile vile swaum
inatoharisha nafsi zetu kwa uelewa bora wa Qur’ani tukufu na kuweza kukubaliwa
Hidaya kwa urahisi.
Baadhi
ya nyakati sisi tunasikia, na vile vile tunatamka senteso hii kwa ndimi zetu
wenyewe, na utakuwa umesikia kwa watu wengi, na unapowauliza je kwa nini
haukuja katika darsa za masomo ya Qur’ani, darsa za tafsiir na sherehe ya
Qur’ani, masomo ya Qur’ani, je kwa nini hakuna darasa ya kutoa masomo ya
Qur’ani? Ukasema hivyo, wao watajibu – kwa sababu sisi tunafunga swaum. Kwa
hiyo mtu anapokuwa katika hali ya swaum anakuwa hayuko imara sawasawa, yaani
anakuwa hana nguvu, dhaifu, hawezi kusimama katika hali ya kuwa na swaum. Sasa
unaona vile madhumuni ya swaum yanavyokuwa yameuliwa hapa. Allah Subhanahu
Wataala ameifanya Swaumu ili kuweza kuelewa Qur’ani. Kufunga swaum kwetu sisi
imekuwa ni kikwazo cha kuelewa Qur’ani. Je kwa nini wewe hauisomi Qur’ani? Je
Kwa nini hutimizi wajibu wa ibada zingine? Je kwa nini? Majibu ya maswali haya
yote atakwambia kwamba yuko katika hali ya swaum. Je, Swaum inakuwa kikwazo kwa
kupata Hidaya? Allah Subhanahu Wataa Amefaradhisha swaum ili kwamba
katika hali ya swaum sisi tuweze kuelewa vyema zaidi na kuwafanya wengineo
waelewe vizuri zaidi. Kwa hakika sisi tunavyochukulia kuwa swaum ni kikwazo
katika kuielewa Qur’ani kwa hakika ni kisingizio tu. Kwa hakika hii ni
fursa moja ya hali ya juu kabisa na umuhimu wake ni kupita uwezo wa vile
tunavyoweza kufikria au kudhania katika akili zetu.
Fursa
hii tumepewa na Allah Subhanahu Wataala bila ya sisi kuiomba Kwake, bali hata
bila ya kuitaka kwa kupitia njia za kuomba. Kwa hiyo inatubidi sisi
tuitayarishe mioyo yetu iwe laini mbele ya Allah Subhanahu Wataala na tuseme,
”Ewe Allah Subhanahu Watalaa mbegu yoyote Wewe unayoipendelea, panda katika
mioyo yetu hii iliyo lainika na mimi ninauwakilisha moyo wangu huu laini ukiwa kama ndiyo ardhi laini kwako Wewe.” Na kwa hakika Allah
Subhanahu Wataala atapandikiza mbegu ya hidaya katika sura ya Qur’ani tukufu.
Kwa hakika ni muhimu sana
kuisoma hivyo, na kupata kuielewa kwake vilevile ni muhimu mno kwetu sisi. Na
vilevile ni muhimu kwetu sisi kupitisha wakati wetu wa mchana na usiku pamoja na
Qur’ani tukufu. Na ni muhimu kwetu kujihusisha na Qur’ani tukufu na vilevile
tuwe Waislamu maharam kwa Qur’ani tukufu, maharam ni wale walio halalika na
wala tusiwe na-maharam wasiohalalika katika kutokuielewa Qur’ani.
Yaani
tusiwe watu na-maharam kwa Qur’ani tukufu. bali inatubidi tuwe watu
maharam kwa Qur’ani tukufu. Msemo huu wa maharamiati, (uhalalifu
), ni nzuri na unaoeleweka kwa urahisi. Kwa hakika sisi tumezoea kusikia
Maharam na na-maharam kwa wanaume na wanawake tu, lakini maharamiati ina wigo
mpana zaidi kuliko huu. Wakati unapokwenda kuhiji (Hajj), na wakati unapokuwa
umevaa Ihram basi wewe unakuwa mahrimu, basi wewe unakuwa umeingia katika haram
ya Allah Subhanahu wataala, na hapo ndipo unakuwa maharam. Muhurim (yule
anayevaa Ihramu) anakuwa maharim wa Allah Subhanahu Wataala na hapo ndipo
anasema, ”labbayk” (nimekuja nimeitikia wito wako), na wakati
anaposikia jambo anasema Labbayk. Hapo huyo anakuwa ameingia katika kuta nne,
anakuwa ameingia katika haram, na yeye sasa ni Muhirimiaji na hivyo mahrim, na
yeye sasa anakuwa ni balozi wa siri za miongozo ya kiroho ya Allah Subhanahu
Wataala hivyo ndivyo inavyotubidi sisi tuwe mahrim kwa Qur’ani tukufu. Sisi
tusichukulie Qur’ani tukufu kama na-maharam, na wala tusiwe na mwelekeo kama na-maharam pamoja na Qur’ani tukufu. Tusiishi
na Qur’ani kama wageni nayo.
Kubali
Qur’ani tukufu na jambo hili litakuwa ni bora kabisa kwetu kama
iwapo tunapata fursa hiyo. Wewe umejionea mwenyewe, kuwa mimea na miche
inayoota katika kipindi cha mchipuo na mavuno yake yanayofuatia na hali ya
ukijani unaokuwa juu ya ardhi, unabakia kwa kipindi cha mwaka mzima. Hata
katika kipindi cha kiangazi baadhi ya ukijani unakuwa bado ukionekana, baadhi
ya matunda pia yakiwepo na hata maua
pia yanaonekana. Maua haya si maua
ya kipindi cha kiangazi, maua
haya yanakuwa yanatokana na kipindi kile cha mchipuo ambapo bado yanakuwa
yanahifadhika hadi katika kipindi kile cha kiangazi, na hata yanakuwa
yanahifadhika katika kipindi cha baridi. Na maua ya msimu huo wa mchipuo yanakuwa katika
msimu mwingine pia. Wale wanaokuwa wamelala katika kipindi cha mchipuo basi
vipindi vya misimu mingine inakuwa ni misimu yao pia. Na wale wanaokuwa macho katika
kipindi cha mchipuo, basi msimu huo wa mchipuo unakuwa bado uko katika misimu
mingine inayofuatia.
Jambo
hili liko katika uwezo wetu, na iwapo tutataka sisi kufanya msimu huo na misimu
yote ikawa ni misimu ya mchipuo, basi itabidi tuelewe thamani ya mwezi mtukufu
wa Ramadhani ili tuweze kufaidika na baraka zake zote katika misimu yote.
Tunamuomba Allah Subhanahu Wataala atujalie fursa katika mwezi huu mtukufu wa
Ramadhani kwa kutilia maanani thamani na ubora wa kipindi hiki; na Insha’allah
kwa uwezo wa Allah Subhanahu Wataala sisi sote tutajitumbukiza katika hidaya ya
Qur’ani tukufu.
Wabilahi
taaufiki.
Tamati,
Bil-kheir.
No comments:
Post a Comment