Sifa
njema anastahiki Allah (s.w), rehma na amani zimuuendee mbora wa viumbe mtume
wetu Muhammad (s.a.w.) na Maswahaba zake na wale wote waliopita katika njia
yake hadi siku ya mwisho..AMIN
Ni mwezi wa kufanya biashara na muumba wetu….ameweka mwezi huu
kw kuwa Allah anahuruma ya kupitilza kwetu sisi…makala hii inaelezea nyakati
muhimu za kujipinda sana katika mwezi huu wa Ramadhwaan:
Nyakati Tatu Muhimu Za Kufanya Ibada – Zisikupite Katika
Ramadhaan
Nyakati tatu hizi
ni muhimu sana za kufanya ibada kutokana na fadhila zake kuu. Mwenye kupenda
kuchuma thawabu nyingi asizikose khaswa katika mwezi huu Mtukufu Wa Ramadhaan
ambao ni mwezi wenye malipo maradufu
1-Wakati wa
mwanzo: Baina ya Alfajiri na jua kuchomoza:
Usimulizi
uliothibiti kutoka katika Swahiyh Muslim (564/1) kwamba Mtume (Swalla Allaahu
'alayhi wa aalihi wa sallam) na Maswahaba walikuwa wakibakia macho wakati huo
hadi jua kuchomoza kwani ni wakati mja anapogaiwa rizki yake, na ni wakati
wenye kheri nyingi, unampa siha nzuri ya mwili binaadamu, na kwa ujumla ni
wakati wenye baraka nyingi za kila aina kwani Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa
aalihi wa sallam) aliomba:
((اللهم بارك لأمتي
في بكورها)) الترمذي, أحمد, أبي داود, ابن
ماجه
((Ewe Allaah, wabarikie
Ummah wangu nyakati za asubuhi mapema)) [At-Tirmidhiy, Ahmad, Abu Daawuud, Ibn
Maajah na imethibitishwa kuwa ni Hadiyth Swahiyh na Shaykh Al-Albaaniy]
Usimulizi huu
umetoka kwa Maswahaba kadhaa ambao wameelezea kwamba: "Mtume (Swalla
Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) alipotaka kupeleka kikosi au jeshi
aliwapeleka mwanzo wa asubuhi". Vile vile wamesimulia kwamba:
"Swakhar alikuwa mtu tajiri ambaye alikuwa akipelekea biashara zake mwanzo
wa asubuhi na matokeo yake ilikuwa ni kufuzu katika biashara na kupata faida
kubwa sana".
Wamesimulia
Salafus-Swaalih kwamba Ibn 'Abbaas naye alimkataza mtu kulala nyakati hizo
alipomwambia:
"قُم، أتنام في
الساعة التي تقسَّم فيه الأرزاق؟"
"Inuka! Je,
unalala katika saa ambayo rizki inagaiwa?"
Ikiwa basi wakati
huo ni kama hivyo ilivyoelezwa juu, basi vipi Muislamu auache wakati huu umpite
khaswa katika mwezi huu mtukufu wa Ramdhaan?
Ibnul-Qayyim
(Rahimahu-Allaah) katika kitabu chake 'Zaad Al-Ma'aad' amesema:
"Usingizi wa asubuhi unanyima rizki kwani huo ni wakati ambao Muumba
anaombwa rizki na wakati wa kugaiwa rizki. Hivyo usingizi unanyima rizki
isipokuwa kwa dharura. Usingizi wakati huo pia ni madhara kwa mwili…"
Faida nyingine
kubwa ya kubakia macho ukimdhukuru Allaah wakati huu:
Si chini ya muda
wa saa na nusu utakuwa umepata thawabu za Hajj na ‘Umrah kamilifu:
عن
أنس عن النبي صلى الله عليه وسلم ، أنه قال (( من صلى الفجر في جماعة ثم قعد يذكر
الله حتى تطلع الشمس ثم صلى ركعتين كانت له كأجر حجة وعمرة تامة تامة تامة) ) أخرج
الترمذي صححه الألباني .
Imetoka kwa Anas kwamba Mtume (Swalla Allaahu
'alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: ((Atakayeswali Alfajiri katika Jama'ah
kisha akakaa anamkumbuka Allaah mpaka likachomoza jua kisha akaswali Raka'ah
mbili, atapata ujira kama ujira wa kwenda Hajj na 'Umrah ulio kamili kamili
kamili)) [Imetolewa na At-Tirmidhiy na kaisahihisha Al-Albaaniy]
Pindi ukifanya hivyo kwa mwezi mzima utakuwa
umechuma thawabu za Hajj na ‘Umrah mwezi mzima. Hizo ni fadhila za siku za
kawaida, seuze ukifanya mwezi mtukufu huu wa Ramadhaan? Jitahidi ndugu Muislamu
kadiri uwezavyo kuchuma hizi thawabu kubwa ambazo zingelikukalifu mali, tabu za
safari na mashaka ya kufika Makkah kutekeleza ibada hizo. Lakini kwa Rahma ya
Allaah Ametujaalia tuweze kuzichuma tukiwa majumbani mwetu tena kwa wepesi
kabisa. Wanaume thawabu zitazidi ikiwa watatekeleza wakiwa misikitini. Wanawake
wanazipata fadhila hizo hata wakiswali majumbani mwao. Hata hivyo, pamoja na
ujira wote huu, tusisahau kuwa fadhila hizo hazivunji wala hazifuti fardh ya
kwenda Hajj kwa mwenye uwezo, asije mtu akadhani kufanya hayo kutakuwa
kumetengua wajiibu wake wa kuhiji au kufanya ‘Umrah.
2- Wakati wa
pili: Kabla ya Jua kuzama (Magharibi):
Huu ni wakati
ambao bado Muislamu yuko katika Swawm na du'aa yake anayoiomba hairudi:
قال صلى الله عليه وسلم: ((ثلاثة لا ترد
دعوتهم: الصائم حتى يفطر والإمام العادل والمظلوم)) وروى الترمذي بسند حسن
Mtume (Swalla
Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: (([Watu] watatu du'aa zao
hazirudi; mwenye kufunga hadi afuturu/afutari, Kiongozi muadilifu na
aliyedhulumiwa)) [At-Tirmidhiy kwa isnaad nzuri]
Kwa hiyo ni fursa
ya kuitumia Muislamu aombe du'aa na haja zake wakati huu khaswa pia kwa vile ni
wakati ambao Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala) Amehimiza Atukuzwe kama Anavyosema:
(( وَسَبِّحْ
بِحَمْدِ رَبِّكَ قَبْلَ طُلُوعِ الشَّمْسِ وَقَبْلَ الْغُرُوبِ))
((.. na mtakase
kwa kumsifu Mola wako Mlezi kabla ya kuchomoza jua na kabla ya kuchwa)) [Qaaf:
39]
((وَسَبِّحْ
بِحَمْدِ رَبِّكَ قَبْلَ طُلُوعِ الشَّمْسِ وَقَبْلَ غُرُوبِهَا وَمِنْ آنَاء
اللَّيْلِ فَسَبِّحْ وَأَطْرَافَ النَّهَارِ لَعَلَّكَ تَرْضَى))
((…Na umtakase
Mola wako Mlezi kwa kumsifu kabla ya kuchomoza jua, na kabla halijachwa, na
nyakati za usiku pia umtakase, na ncha za mchana ili upate ya kukuridhisha))
[Twaahaa: 130].
((
وَاسْتَغْفِرْ لِذَنبِكَ وَسَبِّحْ بِحَمْدِ رَبِّكَ بِالْعَشِيِّ وَالْإِبْكَار))
((…Na omba
msamaha kwa dhambi zako, na umtakase Mola wako Mlezi kwa kumhimidi jioni na
asubuhi)) [Ghaafir: 55]
3- Wakati wa
tatu: Suhuur - Kabla ya Alfajiri
Allaah
(Subhaanahu wa Ta'ala) Amewaaahidi Wacha Mungu Pepo kwa sababu sifa mojawapo
yao ni kuomba maghfira kabla ya Alfajiri:
إِنَّ
الْمُتَّقِينَ فِي جَنَّاتٍ وَعُيُون)) ((آخِذِينَ مَا آتَاهُمْ رَبُّهُمْ
إِنَّهُمْ كَانُوا قَبْلَ ذَلِكَ مُحْسِنِينَ)) ((كَانُوا قَلِيلًا مِّنَ
اللَّيْلِ مَا يَهْجَعُونَ)) ((وَبِالْأَسْحَارِ هُمْ يَسْتَغْفِرُون))
((Hakika
Wacha Mungu watakuwa katika Mabustani na chemchem)) ((Wanapokea Aliyowapa Mola
wao Mlezi. Kwa hakika hao walikuwa kabla ya haya wakifanya mema)) ((Walikuwa
wakilala kidogo tu usiku)) ((Na kabla ya Alfajiri wakiomba maghfira))
[Adh-Dhaariyaat: 15-18]
Kisha wamesifiwa
tena kwa sifa hiyo hiyo pamoja na nyinginezo:
((الصَّابِرِينَ
وَالصَّادِقِينَ وَالْقَانِتِينَ وَالْمُنفِقِينَ وَالْمُسْتَغْفِرِينَ
بِالأَسْحَارِ))
((Wanaosubiri,
wanaosema kweli, na watiifu, na wanaotoa sadaka, na wanaoomba maghafira kabla
ya Alfajiri)) [Al-'Imraan: 17]
Muislamu asiache
wakati huo umpite kwani ni wakati muhimu na wenye fadhila na faida kubwa kwa
vile Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala) Huteremka wakati huo kutoka mbingu ya saba
na kuweko mbingu ya ardhi kutukidhia haja zetu:
عن أبي
هريرة رضي الله عنه أن رسول الله
صلى الله عليه وسلم قال: ((ينزل ربنا
تبارك وتعالى كل ليلة إلى السماء الدنيا
حين يبقى ثلث الليل الآخر فيقول:
من يدعوني فأستجيب له؟ من يسألني
فأعطيه؟ من يستغفرني فأغفر له )) البخاري و مسلم
Imetoka kwa Abu Hurayrah (Radhiya Allaahu 'anhu)
kwamba Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: (Allaah
(Subhaanahu wa Ta'ala) Huteremka (kwa namna inavyolingana na utukufu Wake) kila
siku katika mbingu ya dunia (mbingu ya kwanza) inapobakia thuluthi ya mwisho ya
usiku na Husema: Nani ananiomba Nimtakabalie? Nani ana shida Nimtekelezee? Nani
ananiomba maghfirah Nimghufurie?)) [Al-Bukhaariy na Muslim]
Nani miongoni
mwetu asiyemhitaji Mola wake kumkidhia haja zake na kumuondeshea shida zake?
Nani asiyekuwa na madhambi asiyemhitaji Mola wake kumghufuria? Hivyo usiache
wakati huu ukakupita khaswa kwa vile mwezi huu Mtukufu ambao kila jambo
ulifanyalo lina fadhila na thawabu marudufu.
Tunamuomba Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala)
Atuwezeshe kudiriki nyakati hizo tatu na nyingine, tuwe katika ibada katika
mwezi huu wa Ramadhaan na miezi yote mingineyo na Atujaalie kheri na Baraka
nyingi, Atukidhie haja zetu, Atuondoshee shida zetu na Atughufurie madhambi
yetu yote. Aamiyn
Abuu khaythamah
Mussa Abdallah
No comments:
Post a Comment