Tuesday, February 26, 2013

Msiba Mkubwa kwa jamii ya wasomi wa baadae.



 TAARIFA YA MTOKEO YA KIDATO CHA NNE 2012 HAYA HAPA 

Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Dk. Shukuru Kawambwa (MB) leo ametangaza rasmi matokeo ya Mitihani ya Kidato cha Nne, maarifa-QT.
TAARIFA YA MATOKEO YA MITIHANI YA MAARIFA (QT) NA KIDATO CHA NNE (CSEE)
ILIYOFANYIKA OKTOBA 2012

1.0    UTANGULIZI

Mitihani ya Kidato cha Nne (CSEE) na Maarifa (QT) kwa mwaka 2012 ilifanyika nchini kote kuanzia tarehe 8-25 Oktoba 2012.  Napenda kuchukua nafasi hii kutangaza rasmi matokeo ya mitihani hiyo kama ifuatavyo :
2.0    MTIHANI WA MAARIFA (QT)

2.1           Usajili na Mahudhurio
Katika Mtihani wa Maarifa 2012 watahiniwa waliosajiliwa ni 21,310 ambapo wasichana walikuwa ni 13,134 na wavulana ni 8,176.
Jumla ya watahiniwa 17,137 sawa na asilimia 80.42 ya waliosajiliwa wamefanya Mtihani.
2.2          Matokeo ya Mtihani wa Maarifa (QT)
Watahiniwa 5,984 kati ya 17,137 waliofanya mtihani wamefaulu Mtihani wa Maarifa (QT).

3.0    MTIHANI WA KIDATO CHA NNE (CSEE) 2012

Jumla ya vituo 5,058 vilitumika katika kufanya Mtihani wa Kidato cha Nne 2012 ambapo vituo 4,155 vilikuwa vya watahiniwa wa shule na vituo 903 vilikuwa ni vya watahiniwa wa kujitegemea.

3.1          Usajili na Mahudhurio ya Watahiniwa

(a)          Watahiniwa Wote
Jumla ya watahiniwa 480,036 walisajiliwa kufanya Mtihani wa Kidato cha Nne 2012 wakiwemo wasichana 217,583 sawa na asilimia 45.33 na wavulana 262,453 sawa na asilimia 54.67.  Watahiniwa waliofanya mtihani wa Kidato cha Nne 2012  ni 456,137 sawa na asilimia 95.44. Watahiniwa 21,820 sawa na asilimia 4.55 ya watahiniwa wote waliosajiliwa hawakufanya mtihani.

(b)            Watahiniwa wa Shule
Watahiniwa wa shule waliosajiliwa ni 411,230 wakiwemo wasichana 182,978 sawa na asilimia 44.50 na wavulana 228,252 sawa na asilimia 55.50.  Watahiniwa wa shule waliofanya mtihani walikuwa 397,136 sawa na asilimia 96.57. Aidha, watahiniwa 14,090 sawa na asilimia 3.43 hawakufanya mtihani kutokana na sababu mbalimbali zikiwemo utoro,  ugonjwa na vifo.

(c)             Watahiniwa wa Kujitegemea
Watahiniwa wa kujitegemea waliosajiliwa walikuwa ni 68,806 wakiwemo wasichana 34,605 sawa na asilimia 50.29 na wavulana 34,201 sawa na asilimia 49.71. Watahiniwa 61,001 wakiwemo wasichana 30,917 na wavulana 30,084  wamefanya mtihani wakati watahiniwa 7,730 sawa na asilimia 11.23  hawakufanya mtihani.

4.0        MATOKEO YA MTIHANI WA KIDATO CHA NNE

(a)                 Watahiniwa wa Shule
Jumla ya watahiniwa wa shule 126,847 kati ya watahiniwa 397,136 waliofanya Mtihani wa Kidato cha Nne 2012 wamefaulu. Wasichana waliofaulu ni 46,161 na wavulana ni 80,686.

(b)                Watahiniwa wa Kujitegemea
Idadi ya watahiniwa wa kujitegemea waliofaulu mtihani ni 16,112 kati ya watahiniwa 61,001 waliofanya mtihani.  Wasichana waliofaulu ni 6,751 na wavulana ni 9,361. 

5.0                 UBORA WA UFAULU KWA MADARAJA NA JINSI
Ubora wa ufaulu kwa kuangalia madaraja waliyopata watahiniwa wa shule unaonesha kuwa jumla ya watahiniwa 23,520 wamefaulu katika madaraja I – III ambapo kati yao wasichana ni 7,178 na wavulana ni 16,342.
Mchanganuo wa ufaulu kwa kila Daraja kwa jinsi kwa Watahiniwa wa Shule mwaka 2012 ni kama ifuatavyo:
Daraja
Idadi ya Wavulana                Idadi ya  Wasichana    Jumla
I           1,073                       568                                 1,641
II          4,456                     1,997                               6,453
III        10,813                   4,613                               15,426
I-III      16,342                   7,178                               23,520
IV        64,344                  38,983                             103,327
0         120,664                120,239                            240,903

6.0        SHULE ISHIRINI ZILIZOFANYA VIZURI ZAIDI KATIKA KUNDI LA SHULE ZENYE
            WATAHINIWA 40 AU ZAIDI

Ubora wa ufaulu wa shule umepangwa kwa kutumia kigezo cha “Grade Point Average” (GPA) kuanzia A = 1 hadi F = 5.  Shule zenye watahiniwa 40 na zaidi ziko 3,391. Shule ya kwanza hadi ya ishirini zimeainishwa kwenye Jedwali lifuatalo :
NAFASI           JINA LA SHULE         IDADI YA WATAHINIWA       MKOA
1                      ST. FRANCIS GIRLS                  90                              MBEYA
2                      MARIAN BOYS S.S                    75                              PWANI
3                      FEZA BOYS S.S                          69                              DAR ES SALAAM
4                     MARIAN GIRLS S.S                    88                              PWANI
5                     ROSMINI  S S                               78                               TANGA
6                    CANOSSA S.S                               66                               DAR ES SALAAM
7                    JUDE MOSHONO S S                   51                              ARUSHA
8                    ST. MARY’S  MAZINDE JUU        83                             TANGA
9                   ANWARITE GIRLS S S                   49                              KILIMANJARO
10                KIFUNGILO  GIRLS S S                 86                              TANGA
11                  FEZA GIRLS                                   49                              DAR ES SALAAM
12                  KANDOTO SAYANSI GIRLS SS  124                            KILIMANJARO
13                 DON BOSCO SEMINARY SS         43                              IRINGA
14               ST.JOSEPH MILLENIUM                 133                            DAR ES SALAAM
15              ST.JOSEPH’S ITERAMBOGO SS       64                              KIGOMA
16              ST.JAMES SEMINARY SS                  44                             KILIMANJARO
17             MZUMBE SS                                       104                            MOROGORO
18            KIBAHA SS                                          108                             PWANI
19             NYEGEZI SEMINARY SS                    68                             MWANZA
20             TENGERU BOYS SS                             76                             ARUSHA

7.0        SHULE KUMI AMBAZO HAZIKUFANYA VIZURI ZAIDI KATIKA KUNDI LA SHULE ZENYE WATAHINIWA 40 AU ZAIDI
NAFASI           JINA LA SHULE         IDADI YA WATAHINIWA    MKOA
1                     MIBUYUNI S.S                                 40                       LINDI
2                     NDAME  S.S                                     41                       UNGUJA
3                     MAMNDIMKONGO S.S                63                        PWANI
4                     CHITEKETE S.S                              57                        MTWARA
5                     MAENDELEO S.S                         103                        DAR ES SALAAM
6                     KWAMNDOLWA S.S                     89                         TANGA
7                      UNGULU S.S                                 62                         MOROGORO
8                      KIKALE S.S                                   60                         PWANI
9                      NKUMBA S.S                              152                         TANGA
10                   TONGONI S.S                                56                         TANGA


8.0           TATHMINI YA UFAULU WA WATAHINIWA WA MTIHANI WA KIDATO CHA NNE
               MWAKA 2012 

8.1         Tathmini ya awali iliyofanyika kuhusu ufaulu wa watahiniwa katika shule mbalimbali
               inaonesha kuwa shule zilizofanya vizuri zaidi ni zile ambazo zina mahitaji yote ya msingi
               ikiwemo walimu wa kutosha, miundombinu na vifaa vya kufundishia na kujifunzia.  Aidha,
               shule zenye ufaulu wa chini ni zile ambazo zina changamoto mbalimbali ikiwa ni pamoja na:

(i)                 Baadhi ya shule za vijijini hazina kabisa walimu wa masomo ya Sayansi na Hisabati na pia zina upungufu mkubwa wa walimu wa masomo mengine;

(ii)               Kutokuwepo kwa maabara kwa shule zenye mikondo ya sayansi na pia kutokuwepo kwa
 maktaba kwa ajili ya kujisomea; na Upungufu mkubwa wa vitabu vya kiada na ziada. Katika baadhi ya shule uwiano wa kitabu kwa mwanafunzi ni 1:10.

8.2            Mkakati wa Serikali ni kuendelea kupunguza changamoto hizo kila mwaka ikiwa ni pamoja
              na kufanya mambo yafuatayo:

(i)                      Kuajiri walimu kila mwaka ili kuondoa upungufu uliopo katika shule zetu. Mwaka
 2011/2012 Serikali iliajiri walimu wa sekodari 13,246 na mwaka huu wa fedha 2012/2013 imeajiri walimu 12,973 ambao wamepangwa katika shule zenye upungufu mkubwa wa walimu. Ajira ya walimu wapya mwaka huu umetuwezesha kuwa na wastani wa walimu 2-3 kwa shule.  Hali hii itaendelea kuboreka kadri tunavyoendela kuajiri walimu.

(ii)                    Kuboresha miundombinu iliyoko katika shule zetu ikiwa ni pamoja na kujenga nyumba za walimu, madarasa na maabara. Mwaka 2012/2013 Serikali imepanga kuboresha miundombinu katika shule 264 zilizopo katika mazingira magumu ikiwemo miundombinu ya maabara na nyumba za walimu.

(iii)                  Kuendelea kutoa ruzuku ya Tsh 25,000 kwa mwanafunzi kwa mwaka, ambapo asilimia 50 ya fedha hizo ni kwa ajili ya ununuzi wa vifaa vya kufundishia na kujifunzia ili kuziwezesha shule kununua vitabu pamoja na vifaa vingine muhimu kitaaluma.

(iv)           Wizara kuendelea kuzishauri Halmashauri kuweka mgawanyo mzuri wa walimu waliopo
               baina ya shule na shule.

(v)            Wizara itaendelea kuimarisha Idara ya Ukaguzi wa Shule pamoja na kuwawezesha
                Waratibu Elimu Kata na Wakuu wa Shule kufanya ukaguzi wa ndani katika Shule za
                Sekondari zilizo katika maeneo yao.

9.0           MATOKEO YA MITIHANI YALIYOZUIWA

               Baraza la Mitihani la Tanzania limezuia kutoa matokeo ya:
(a)           Watahiniwa 28,582 wa Shule ambao hawajalipa ada ya Mtihani hadi watakapolipa ada
                wanayodaiwa pamoja na faini; na ikiwa hawatalipa katika kipindi cha miaka miwili (02)            
              toka matokeo kutangazwa, matokeo yao yatafutwa.

(b)           Watahiniwa 65 wa kujitegemea na 71 waliofanya Mtihani wa Maarifa (QT) mwaka 2012
               bila ya kulipa ada ya Mtihani hadi watakapolipa ada pamoja na faini. Ikiwa hawatalipa ada
              hiyo katika kipindi cha miaka miwili (02) toka matokeo kutangazwa, matokeo yao yatafutwa.

10.0             MATOKEO YA MITIHANI  YALIYOFUTWA

10.1              Matokeo Yaliyofutwa Kwa Sababu ya Udanganyifu
              Jumla ya watahiniwa 789 wamefutiwa matokeo yao yote ya mtihani kwa mujibu wa kifungu
             Na.52(b) cha Kanuni za Mitihani baada ya kubainika kuwa walifanya udanganyifu katika
            mitihani ya Oktoba 2012. Kati yao, watahiniwa wa shule ni 624 na watahiniwa wa kujitegema
           ni 148 na watahiniwa wa Mtihani wa Maarifa (QT) ni 17.

Aina ya udanganyifu uliobainika na idadi ya watahiniwa husika ni kama ifuatavyo:

S/N      AINA YA UDANGANYIFU   IDADI YA WATAHINIWA
(i)        Watahiniwa kubainika kuwa na skripti zenye miandiko tofauti au kuwa na miandiko tofauti
            katika skripti ya somo moja au zaidi ya moja. 04

(ii)       Watahiniwa kukamatwa na wasimamizi ndani ya chumba cha mtihani wakiwa na ‘notes.’     170

(iii)      Watahiniwa kubainika kuwa na mfanano usio wa kawaida wa majibu.           590

(iv)      Watu kukamatwa wakiwafanyia watahiniwa wengine mtihani ‘impersonation”.         04

(v)       Watahiniwa kukamatwa na simu ndani ya chumba cha mtihani.         06


(vi)      Watahiniwa kukamatwa na wasimamizi wakibadilisha karatasi za maswali au skripti kwa
           lengo la kufanya udanganyifu. 15

            JUMLA            789

10.2     Matokeo Yaliyofutwa Kwa Sababu ya Watahiniwa Kuandika Matusi Katika Skripti Zao

(i)                    Jumla ya watahiniwa 24 waliandika matusi kwenye skripti zao za masomo mbalimbali.
             Kitendo hicho ni kosa kwa mujibu wa kifungu 5(13) cha Kanuni za Mitihani
             kinachosomeka:

“Written responses to any examination question which carry words, drawings or pictures connected to sex or abusive language in such a way that it becomes offensive shall consitute an examination offence and a candidate who commits such an offence shall be punished by the Council.”
Kutokana na kosa hilo Baraza la Mitihani limefuta matokeo  yao yote kwa mujibu wa Kifungu cha 6(2)(a) cha Kanuni za Mitihani kinachosomeka: 
“A candidate found to have committed an examination offence shall – (a) have his examination results nullified”

(ii)         Kitendo cha kuandika matusi kwenye karatasi za majibu (skripti) kinaonesha utovu wa nidhamu wa hali ya juu. Serikali haitaweza kuwavumilia hata kidogo watahiniwa wa aina hiyo. Hivyo, Serikali itaangalia hatua zaidi za kisheria za kuchukua dhidi ya watahiniwa wote walioandika matusi.
Kwa mujibu wa kifungu Na. 6(2)(b) cha Kanuni za Mitihani, watahiniwa wote waliobainika kufanya udanganyifu katika mitihani au kuandika matusi katika skripti zao hawataruhusiwa kufanya mitihani inayoendeshwa na Baraza la Mitihani la Tanzania  kwa kipindi cha mwaka mmoja (01) kuanzia tarehe ya kutangazwa kwa matokeo.

           

Siku ya Dua ya Pamoja kwa ajili ya U.E

As.alaykum!!!tarehe 15-02-2013,Jumuiya ya MSATEKU ilitekeleza taratibu zake ya kukutanishana pamoja kwa ajili kikao cha pamoja kwa ajili ya kupewa taarifa mbalimbali za maendeleo ya Jumuiya kwisha kuomba dua ya pomoja kwa ajili ya maandalizi ya mitihani ya U.E......zifuatazo ni baadhi picha za tukio hili.Tunaomba radhi kwa picha hizo kukosa ubora wa muonekano.

 Baadhi ya maustadh wa MSATEKU wakifuatilia kwa makini taarifa za awali pamoja na ratiba ya Agenda.
 Vijana walikuwa wanyenyekevu kwa kusikiliza Qu`aran tukufu.
 Qu`aran ilisoma kabla ya ufunguzi rasmi wa agenda mbalimbali.

 Amirat Dada Nevizad Kituka alikuwepo na anaonekana yupo makini kufuatilia yanayojili kutoka meza kuu.
 Meza kuu....Kutoka kulia ni katibu msaidizi Brother Kagomba(mwenye makaratasi),anaemfuatia ni Brother Amry Jaribu(Katibu mkuu) akifuatiwa na mwalimu mlezi brother Alawi Mikidadi,Amir wa jumuiya Brother Abdul Salami,Brother Husseni (naibu Amir Uchumi) na mwishoni ni Amir wa Da`awa Brother Seseme.
 Maukhut wakifuatilia kikao hicho.
 Amir wa Habari (mwenye miwani)akifuatilia kwa makini kikao.

Sunday, February 10, 2013

Maandalizi ya U.E

Assalam alaykum!!!Tarehe 10,February,2013.Idara ya Taaluma ilaandaa SEMINA ya kujiandaa na mitihani ya U.E kwa vijana wa Mwaka wa Kwanza (I) , lengo la semina ni kujaribu kupambana na khofu na pia kupelekea matokeo mazuri kwa vijana hao. Mada mbili ziliwasilishwa ya kwanza ilikuwa Namna ya kujiandaa Kisaikolijia na Nini cha kufanya ili ufanye vizuri katika mitihani? Zifuatazo ni baadhi ya picha zenye tukio hilo.

 Viongozi wa Idara ya Taaluma pamoja na viongozi wa juu wa Jumuiya....Kutoka kushoto ni naibu Amir idara ya Elimu brother Ridhiwan,anaefuata ni Brother Amur(Amir wa Idara ya Elimu na Naibu Amir mkoa Tamsya-Mbeya),anaefuata ni Amir wa Jumuiya (MSATEKU) brother Abdul Salami na anaeongea ni Brother Seseme(Amir idara ya Da`awa) na pembeni ni brother Suilemani(Mkuu wa maktaba ya MSATEKU na mjumbe idara ya elimu)
 Vijana wa mwaka wa kwanza wakifuatilia maelekezo kutoka meza kuu (haipo pichani)
Maustadh wa Mwaka wa Kwanza wakifuatilia kwa makini semina hiyo,leo asubuhi.

Thursday, February 7, 2013

Valentine Day na Hukumu Ya Kuisherehekea









Brother Amry Jaribu (H/S MSATEKU)



                                                                                                         









Valentine Day (Siku Ya Wapendanao) Na Hukumu Ya Kuisherehekea

BismiLLaah wa AlhamduliLLaah was-Swalaatu was Salaamu ‘alaa Muhammad wa ‘alaa ‘Aalihi wa Aswhaabihil Kiraam, wa Ba’ad,
Allaah سبحانه وتعالى Ametuchagulia dini ya Kiislamu ambayo ndio dini ya haki na Hatokubali dini yoyote nyingine kama Anavyosema: 

((وَمَن يَبْتَغِ غَيْرَ الإِسْلاَمِ دِينًا فَلَن يُقْبَلَ مِنْهُ وَهُوَ فِي الآخِرَةِ مِنَ الْخَاسِرِينَ)
 
((Na anayetafuta dini isiyo kuwa Uislamu haitakubaliwa kwake. Naye Akhera atakuwa katika wenye kukhasirika)) [Al-'Imraan:85]
Na Mtume صلى الله عليه وآله وسلم ametuambia kuwa kutakua na makundi katika ummah wake ambao watawafuata maadui wa Allaah سبحانه وتعالى katika desturi na mila zao kama ifuatavyo:
((ستتبعون سنن من كان قبلكم شبراً بشبر وذراعاً بذراع حتى لو دخلوا جحر ضب لدخلتموه)) قالوا: أتراهم اليهود والنصارى؟ قال: ((فمن إذن؟)) البخاري ومسلم

((Mtafuata nyendo  za wale waliokuja  kabla yenu  hatua kwa hatua mpaka itafika hadi wakiingia katika shimo la kenge, na nyinyi mtaingia pia)) Wakasema (Maswahaba):  Ewe Mtume! Je, unamaanisha Mayahudi na Manaswara?  Akasema: ((Hivyo nani basi mwengine?)) Al-Bukhariy na Muslim

Maneno hayo aliyoyasema Mtume صلى الله عليه وآله وسلم  hakika yamesadikika kwani tunaona jinsi gani Waislamu siku hizi wanavyoigiza mila, desturi na tabia za makafiri na kuzisherehekea kama mfano siku hii inayoitwa ‘Valentine day’ (Siku ya Wapendanao). 
Na baya zaidi na la kusikitisha sana ni kwamba sherehe hizi zinaenezwa katika njia mbali mbali za mawasiliano kama kutumiana kadi, barua pepe (e-mail), salamu katika simu za mkono. Hakika fitna hii humfanya Muislamu aharibu ‘Aqiydah (Iymaan) yake kwa kudhani kuwa anafanya jambo la kawaida na hali ni jambo lisilo katika sheria ya dini yetu bali ni shirki kubwa na upotofu wa kufuata wanayoamini makafiri.
   

Historia Ya Sherehe Ya Siku Ya Valentine
Sherehe hii ya wapendanao ni sherehe ya wapagani  wa Kirumi wakati dini yao ya upagani ilikuwa ni dini iliyotapakaa kwa Warumi karne zaidi ya kumi na saba zilizopita.  Na fikra zao ilikuwa ni kuelezea hisia ya ‘mapenzi ya kiroho’
Kulikuwa na visasili (uongo) zilizohusishwa na sherehe hii ya upagani ya Warumi ambao umeendelea kutoka warithi wa Kikiristo. Miongoni mwa uongo huo ni kuamini kwao Warumi kuwa Romulus, aliyevumbua Rome, alinyonyeshwa siku moja na mbwa mwitu mwanamke, hivyo akampa nguvu na hikma. 
Warumi walikuwa wakisherehekea tukio hili katikati ya Februari kila mwaka kwa kufanya sherehe kubwa. Na mojawapo ya tambiko katika sherehe hii ni kuchinja mbwa au mbuzi. Vijana wawili wenye nguvu hujipaka damu ya mbwa au ya mbuzi katika miili yao, kisha huiosha damu hiyo kwa maziwa. Baada ya hapo, watu hufanya gwaride wakiwa vijana hawa wawilii wako mbele wakiongoza gwaride iliyokuwa ikitembea barabarani. Vijana hao wawili walikuwa wakichukua vipande vya ngozi ambavyo waliwapigia watu wanaowavuka. Wanawake wa kirumi walikuwa wakipokea mapigo hayo wakiamini kuwa yatawahifadhi na kutibu utasa.


Kuungamana Baina Mtakatifu Valentine (Saint Valentine) Na Sherehe Hii
Mtakatifu Valentine (Saint Valentine) ni jina waliopewa mashujaa wawili wakongwe waliokufa ambao ni wana wa kanisa la kikiristo. Inasemekena kwamba walikuwa ni wawili au mmoja tu. Huyo mmoja alikufa Rome kutokana na mateso ya kiongozi wa Kigothi aliyeitwa Claudius. Kanisa la Saint Valentine lilijengwa kwa ajili ya kudumisha kumbukumbu yake. 
Warumi walipoingia ukristo, wakaendelea kusherehekea sikukuu ya wapendanao (valentine day) lakini wakabadilisha kutoka fikra ya upagani ya ‘mapenzi ya kiroho’ (spiritual love) na kuleta fikra nyingine iliyojulikana kama ni ‘mapenzi ya mashujaa’ yaliyowakilishwa na Saint Valentine ambaye aliuliwa kwa ajili ya kutetea mapenzi na amani. Vile vile ikajulikana ni sikukuu ya wapenzi, na Saint Valentine alifanywa kuwa ni mlezi wa mapenzi ya mtakatifu. 
Miongoni mwa imani yao inayoambatana na sherehe hii ni kwamba majina ya wasichana waliofika umri wa kuolewa yaliandikwa katika vikaratasi vidogo vilivyokunjwa mviringo kisha vikawekwa katika chombo juu ya meza. Kisha wavulana waliotaka kuoa waliitwa na kila mmoja huchagua karatasi moja ikiwa na jina la msichana. Kisha hujiambatanisha naye huyo msichana aliyempata kutokana na kura hiyo aliyochagua kwa muda wa mwaka ili wajuane vizuri kisha tena hufunga ndoa, au kama hawakuelewana hurudia tena kufanya kura inapofika siku hiyo mwaka unaofatia.   
Vile vile imesemekana kwamba chanzo cha sikukuu hii, ni kwamba warumi walipokuwa wakristo baada ya ukristo kutapakaa, Mfalme wa Kirumi Claudius II alitoa hukumu katika karne ya tatu kwamba askari wasioe kwa sababu kuoa kwao kutawashughulisha na vita walivyokuwa wakipigana. Hukumu hiyo ilipingwa na Saint Valentine ambaye alianzisha kuozesha maaskari kwa siri. Alipokuja kujua mfalme, alimfunga jela na akamhukumu kuuliwa. Huko jela akapendana na mtoto wa mkuu wa jela, lakini ikawa ni siri kwani kutokana na sheria ya ukristo, mapadri na makasisi wameharamishwa kuoa au kupenda.
      
Hata hivyo alipewa heshima yake na wakristo kwa sababu ya kushikilia na kujikita imara katika ukristo wakati mfalme alipotaka kumsamehe kwa sharti aache ukristo na kuabudu miungu ya Kirumi ili awe msiri wake na awe mkwe wake. Lakini Saint Valentine alikataa ahadi hiyo na akapendelea ukristo, kwa hiyo akauliwa siku ya tarehe 14 Februari 270 CE. Ndio ikaitwa siku hii kwa jina la huyo mtakatifu (Valentine). 

Papa (Pope) naye akaifanya siku hiyo ya kufa Saint Valentine tarehe 14 Februari 270 CE kuwa ni sikukuu ya mapenzi. Na ni nani alikuwa Papa huyo? Ni Askofu mkuu wa kanisa la ‘universal church’, ambaye ni mrithi wa mtakatifu Peter.
Ndugu Waislamu tazameni vipi huyo askofu anavyohusika katika kuadhimisha sikukuu hii ambayo ni uzushi katika dini yao ya Kikiristo. Hii itukumbushe kauli ya Allaah سبحانه وتعالى
((اتَّخَذُواْ أَحْبَارَهُمْ وَرُهْبَانَهُمْ أَرْبَابًا مِّن دُونِ اللّهِ))
((Wamewafanya makuhani wao na wamonaki wao kuwa ni marabi badala ya Mwenyezi Mungu)) [At-Tawbah: 31]


Matendo Yanayotakiwa Kujiepusha Nayo Ambayo Yanayofanyika Katika Sikukuu Hii   
  1. Kuonyeshana bashasha na furaha kama ilivyo katika sikukuu zao nyingine.

  1. Kupeana mawaridi mekundu (Red Roses) ambayo ni alama ya kuelezea mapenzi, ‘mapenzi ya kiroho’ ya wapagani au ‘mapenzi’ ya Wakristo. Hivyo inajulikana kuwa ni ‘Sikukuu Ya Wapendanao’.

  1. Kupelekeana kadi. Na kadi nyingine zina picha za ‘mungu wa mapenzi wa kirumi’ ambaye ana mbawa mbili, akiwa amekamata upinde na mshale. Huyu ndio mungu wa mapenzi wa wapagani warumi. Shirk iliyoje hii ndugu Waislamu?

  1. Kubadilishana maneno ya mapenzi na matamanio katika kadi wanazopelekeana, yakiwa katika mfumo wa kimashairi, tenzi na sentensi fupi fupi. Kadi nyingine zina picha za kimzaha na maneno ya kuchekesha, na mara nyingi zina maneno ya kusema ‘Kuwa Valentine wangu’. Hii inaashiria maana ya kikiristo ya sikukuu hii baada ya kuwa asili yake ni kutokana na fikra za upagani.

  1. Katika nchi nyingi za kimagharibi, hufanyika sherehe siku hiyo ambayo kunakuweko kuchanganyika wanaume na wanawake, kuimba, na kucheza dansi. Na wengi wanapelekeana zawadi kama mawaridi, maboksi ya chokoleti kwa wake zao, marafiki na wanaowapenda.
Kutokana na maelezo yote hayo ya chanzo cha sikukuu hii, tunaona kwamba siku hiyo haina uhusiano wowote katika Uislamu, bali yana uhusiano na washirikina mapagani, hata wakristo katika dini yao nao pia ni uzushi, sasa itakuwaje sisi Waislamu tuwaigize kusherehekea?  
Basi ndugu Waislamu tutambue kuwa jambo hili ni ovu mno, haimpasi Muislamu kuharibu ‘Aqiydah (iymaan) yake kwani kuna hatari kubwa kushiriki katika sherehe hii nayo ni kuingia katika kumshirikisha Allaah سبحانه وتعالى, na kama tunavyojua kuwa Allaah سبحانه وتعالى Hamsamehe mtu anayefanya shirki pindi akifariki bila ya kutubu kama ilivyo katika aya ifuatayo: 
 ((إِنَّ اللّهَ لاَ يَغْفِرُ أَن يُشْرَكَ بِهِ وَيَغْفِرُ مَا دُونَ ذَلِكَ لِمَن يَشَاء وَمَن يُشْرِكْ بِاللّهِ فَقَدِ افْتَرَى إِثْمًا عَظِيمًا))
((Hakika Mwenyezi Mungu Hasamehe kushirikishwa, na Husamehe yaliyo duni ya hilo kwa Amtakaye. Na anayemshirikisha Mwenyezi Mungu basi hakika amezua dhambi kubwa)) [An-Nisaa: 48]



Hivyo ni kuharamishwa na Pepo na kupata makazi ya moto, tunajikinga na Allaah kwa hayo.
((إِنَّهُ مَن يُشْرِكْ بِاللّهِ فَقَدْ حَرَّمَ اللّهُ عَلَيهِ الْجَنَّةَ وَمَأْوَاهُ النَّارُ وَمَا لِلظَّالِمِينَ مِنْ أَنصَار)) 
((Kwani anayemshirikisha Mwenyezi Mungu, hakika Mwenyezi Mungu Atamharimishia Pepo, na mahala pake ni Motoni. Na waliodhulumu hawatakuwa na wa kuwanusuru)) [Al-Maaidah: 72]

Tunamuomba Allaah سبحانه وتعالى Atuepushe na kila aina ya shirk na Atuonyeshe yaliyo ya haki tuyafuate, na yaliyo ya batili tujiepushe nayo na Atuajaalie ni miongoni mwa wale wanaosikiliza kauli (nyingi) wakafuata zile zilizo njema.  Aamiyn