Thursday, February 7, 2013

Valentine Day na Hukumu Ya Kuisherehekea









Brother Amry Jaribu (H/S MSATEKU)



                                                                                                         









Valentine Day (Siku Ya Wapendanao) Na Hukumu Ya Kuisherehekea

BismiLLaah wa AlhamduliLLaah was-Swalaatu was Salaamu ‘alaa Muhammad wa ‘alaa ‘Aalihi wa Aswhaabihil Kiraam, wa Ba’ad,
Allaah سبحانه وتعالى Ametuchagulia dini ya Kiislamu ambayo ndio dini ya haki na Hatokubali dini yoyote nyingine kama Anavyosema: 

((وَمَن يَبْتَغِ غَيْرَ الإِسْلاَمِ دِينًا فَلَن يُقْبَلَ مِنْهُ وَهُوَ فِي الآخِرَةِ مِنَ الْخَاسِرِينَ)
 
((Na anayetafuta dini isiyo kuwa Uislamu haitakubaliwa kwake. Naye Akhera atakuwa katika wenye kukhasirika)) [Al-'Imraan:85]
Na Mtume صلى الله عليه وآله وسلم ametuambia kuwa kutakua na makundi katika ummah wake ambao watawafuata maadui wa Allaah سبحانه وتعالى katika desturi na mila zao kama ifuatavyo:
((ستتبعون سنن من كان قبلكم شبراً بشبر وذراعاً بذراع حتى لو دخلوا جحر ضب لدخلتموه)) قالوا: أتراهم اليهود والنصارى؟ قال: ((فمن إذن؟)) البخاري ومسلم

((Mtafuata nyendo  za wale waliokuja  kabla yenu  hatua kwa hatua mpaka itafika hadi wakiingia katika shimo la kenge, na nyinyi mtaingia pia)) Wakasema (Maswahaba):  Ewe Mtume! Je, unamaanisha Mayahudi na Manaswara?  Akasema: ((Hivyo nani basi mwengine?)) Al-Bukhariy na Muslim

Maneno hayo aliyoyasema Mtume صلى الله عليه وآله وسلم  hakika yamesadikika kwani tunaona jinsi gani Waislamu siku hizi wanavyoigiza mila, desturi na tabia za makafiri na kuzisherehekea kama mfano siku hii inayoitwa ‘Valentine day’ (Siku ya Wapendanao). 
Na baya zaidi na la kusikitisha sana ni kwamba sherehe hizi zinaenezwa katika njia mbali mbali za mawasiliano kama kutumiana kadi, barua pepe (e-mail), salamu katika simu za mkono. Hakika fitna hii humfanya Muislamu aharibu ‘Aqiydah (Iymaan) yake kwa kudhani kuwa anafanya jambo la kawaida na hali ni jambo lisilo katika sheria ya dini yetu bali ni shirki kubwa na upotofu wa kufuata wanayoamini makafiri.
   

Historia Ya Sherehe Ya Siku Ya Valentine
Sherehe hii ya wapendanao ni sherehe ya wapagani  wa Kirumi wakati dini yao ya upagani ilikuwa ni dini iliyotapakaa kwa Warumi karne zaidi ya kumi na saba zilizopita.  Na fikra zao ilikuwa ni kuelezea hisia ya ‘mapenzi ya kiroho’
Kulikuwa na visasili (uongo) zilizohusishwa na sherehe hii ya upagani ya Warumi ambao umeendelea kutoka warithi wa Kikiristo. Miongoni mwa uongo huo ni kuamini kwao Warumi kuwa Romulus, aliyevumbua Rome, alinyonyeshwa siku moja na mbwa mwitu mwanamke, hivyo akampa nguvu na hikma. 
Warumi walikuwa wakisherehekea tukio hili katikati ya Februari kila mwaka kwa kufanya sherehe kubwa. Na mojawapo ya tambiko katika sherehe hii ni kuchinja mbwa au mbuzi. Vijana wawili wenye nguvu hujipaka damu ya mbwa au ya mbuzi katika miili yao, kisha huiosha damu hiyo kwa maziwa. Baada ya hapo, watu hufanya gwaride wakiwa vijana hawa wawilii wako mbele wakiongoza gwaride iliyokuwa ikitembea barabarani. Vijana hao wawili walikuwa wakichukua vipande vya ngozi ambavyo waliwapigia watu wanaowavuka. Wanawake wa kirumi walikuwa wakipokea mapigo hayo wakiamini kuwa yatawahifadhi na kutibu utasa.


Kuungamana Baina Mtakatifu Valentine (Saint Valentine) Na Sherehe Hii
Mtakatifu Valentine (Saint Valentine) ni jina waliopewa mashujaa wawili wakongwe waliokufa ambao ni wana wa kanisa la kikiristo. Inasemekena kwamba walikuwa ni wawili au mmoja tu. Huyo mmoja alikufa Rome kutokana na mateso ya kiongozi wa Kigothi aliyeitwa Claudius. Kanisa la Saint Valentine lilijengwa kwa ajili ya kudumisha kumbukumbu yake. 
Warumi walipoingia ukristo, wakaendelea kusherehekea sikukuu ya wapendanao (valentine day) lakini wakabadilisha kutoka fikra ya upagani ya ‘mapenzi ya kiroho’ (spiritual love) na kuleta fikra nyingine iliyojulikana kama ni ‘mapenzi ya mashujaa’ yaliyowakilishwa na Saint Valentine ambaye aliuliwa kwa ajili ya kutetea mapenzi na amani. Vile vile ikajulikana ni sikukuu ya wapenzi, na Saint Valentine alifanywa kuwa ni mlezi wa mapenzi ya mtakatifu. 
Miongoni mwa imani yao inayoambatana na sherehe hii ni kwamba majina ya wasichana waliofika umri wa kuolewa yaliandikwa katika vikaratasi vidogo vilivyokunjwa mviringo kisha vikawekwa katika chombo juu ya meza. Kisha wavulana waliotaka kuoa waliitwa na kila mmoja huchagua karatasi moja ikiwa na jina la msichana. Kisha hujiambatanisha naye huyo msichana aliyempata kutokana na kura hiyo aliyochagua kwa muda wa mwaka ili wajuane vizuri kisha tena hufunga ndoa, au kama hawakuelewana hurudia tena kufanya kura inapofika siku hiyo mwaka unaofatia.   
Vile vile imesemekana kwamba chanzo cha sikukuu hii, ni kwamba warumi walipokuwa wakristo baada ya ukristo kutapakaa, Mfalme wa Kirumi Claudius II alitoa hukumu katika karne ya tatu kwamba askari wasioe kwa sababu kuoa kwao kutawashughulisha na vita walivyokuwa wakipigana. Hukumu hiyo ilipingwa na Saint Valentine ambaye alianzisha kuozesha maaskari kwa siri. Alipokuja kujua mfalme, alimfunga jela na akamhukumu kuuliwa. Huko jela akapendana na mtoto wa mkuu wa jela, lakini ikawa ni siri kwani kutokana na sheria ya ukristo, mapadri na makasisi wameharamishwa kuoa au kupenda.
      
Hata hivyo alipewa heshima yake na wakristo kwa sababu ya kushikilia na kujikita imara katika ukristo wakati mfalme alipotaka kumsamehe kwa sharti aache ukristo na kuabudu miungu ya Kirumi ili awe msiri wake na awe mkwe wake. Lakini Saint Valentine alikataa ahadi hiyo na akapendelea ukristo, kwa hiyo akauliwa siku ya tarehe 14 Februari 270 CE. Ndio ikaitwa siku hii kwa jina la huyo mtakatifu (Valentine). 

Papa (Pope) naye akaifanya siku hiyo ya kufa Saint Valentine tarehe 14 Februari 270 CE kuwa ni sikukuu ya mapenzi. Na ni nani alikuwa Papa huyo? Ni Askofu mkuu wa kanisa la ‘universal church’, ambaye ni mrithi wa mtakatifu Peter.
Ndugu Waislamu tazameni vipi huyo askofu anavyohusika katika kuadhimisha sikukuu hii ambayo ni uzushi katika dini yao ya Kikiristo. Hii itukumbushe kauli ya Allaah سبحانه وتعالى
((اتَّخَذُواْ أَحْبَارَهُمْ وَرُهْبَانَهُمْ أَرْبَابًا مِّن دُونِ اللّهِ))
((Wamewafanya makuhani wao na wamonaki wao kuwa ni marabi badala ya Mwenyezi Mungu)) [At-Tawbah: 31]


Matendo Yanayotakiwa Kujiepusha Nayo Ambayo Yanayofanyika Katika Sikukuu Hii   
  1. Kuonyeshana bashasha na furaha kama ilivyo katika sikukuu zao nyingine.

  1. Kupeana mawaridi mekundu (Red Roses) ambayo ni alama ya kuelezea mapenzi, ‘mapenzi ya kiroho’ ya wapagani au ‘mapenzi’ ya Wakristo. Hivyo inajulikana kuwa ni ‘Sikukuu Ya Wapendanao’.

  1. Kupelekeana kadi. Na kadi nyingine zina picha za ‘mungu wa mapenzi wa kirumi’ ambaye ana mbawa mbili, akiwa amekamata upinde na mshale. Huyu ndio mungu wa mapenzi wa wapagani warumi. Shirk iliyoje hii ndugu Waislamu?

  1. Kubadilishana maneno ya mapenzi na matamanio katika kadi wanazopelekeana, yakiwa katika mfumo wa kimashairi, tenzi na sentensi fupi fupi. Kadi nyingine zina picha za kimzaha na maneno ya kuchekesha, na mara nyingi zina maneno ya kusema ‘Kuwa Valentine wangu’. Hii inaashiria maana ya kikiristo ya sikukuu hii baada ya kuwa asili yake ni kutokana na fikra za upagani.

  1. Katika nchi nyingi za kimagharibi, hufanyika sherehe siku hiyo ambayo kunakuweko kuchanganyika wanaume na wanawake, kuimba, na kucheza dansi. Na wengi wanapelekeana zawadi kama mawaridi, maboksi ya chokoleti kwa wake zao, marafiki na wanaowapenda.
Kutokana na maelezo yote hayo ya chanzo cha sikukuu hii, tunaona kwamba siku hiyo haina uhusiano wowote katika Uislamu, bali yana uhusiano na washirikina mapagani, hata wakristo katika dini yao nao pia ni uzushi, sasa itakuwaje sisi Waislamu tuwaigize kusherehekea?  
Basi ndugu Waislamu tutambue kuwa jambo hili ni ovu mno, haimpasi Muislamu kuharibu ‘Aqiydah (iymaan) yake kwani kuna hatari kubwa kushiriki katika sherehe hii nayo ni kuingia katika kumshirikisha Allaah سبحانه وتعالى, na kama tunavyojua kuwa Allaah سبحانه وتعالى Hamsamehe mtu anayefanya shirki pindi akifariki bila ya kutubu kama ilivyo katika aya ifuatayo: 
 ((إِنَّ اللّهَ لاَ يَغْفِرُ أَن يُشْرَكَ بِهِ وَيَغْفِرُ مَا دُونَ ذَلِكَ لِمَن يَشَاء وَمَن يُشْرِكْ بِاللّهِ فَقَدِ افْتَرَى إِثْمًا عَظِيمًا))
((Hakika Mwenyezi Mungu Hasamehe kushirikishwa, na Husamehe yaliyo duni ya hilo kwa Amtakaye. Na anayemshirikisha Mwenyezi Mungu basi hakika amezua dhambi kubwa)) [An-Nisaa: 48]



Hivyo ni kuharamishwa na Pepo na kupata makazi ya moto, tunajikinga na Allaah kwa hayo.
((إِنَّهُ مَن يُشْرِكْ بِاللّهِ فَقَدْ حَرَّمَ اللّهُ عَلَيهِ الْجَنَّةَ وَمَأْوَاهُ النَّارُ وَمَا لِلظَّالِمِينَ مِنْ أَنصَار)) 
((Kwani anayemshirikisha Mwenyezi Mungu, hakika Mwenyezi Mungu Atamharimishia Pepo, na mahala pake ni Motoni. Na waliodhulumu hawatakuwa na wa kuwanusuru)) [Al-Maaidah: 72]

Tunamuomba Allaah سبحانه وتعالى Atuepushe na kila aina ya shirk na Atuonyeshe yaliyo ya haki tuyafuate, na yaliyo ya batili tujiepushe nayo na Atuajaalie ni miongoni mwa wale wanaosikiliza kauli (nyingi) wakafuata zile zilizo njema.  Aamiyn

2 comments:

  1. Replies
    1. Tunashukuru Brother Seseme kwa kutupa moyo Allah atulipe wote.Amin

      Delete