MINBARI YA RAMADHAN RAMADHANIMINBARI YA RAMADHANI
Hii ni kutokana na mnasaba wa kuingia mwezi mtukufu wa Ramadhani. Minbari ya
Ramadhani itakuwa ikikuletea mawaidha yahusiyanayo na funga ya Ramadhani, ili
uweze kuijua funga na hatimaye uweze kufunga kama alivyoamrisha Mwenyezi Mungu
Mtukufu na kama alivyofunga Bwana Mtume
-Rehema na Amani zimshukie - ambaye ndiye kigezo chetu chema. Sambamba na
Minbari ya Ramadhani, BLOG yako ya MSATEKU itakuwa ikikuletea TUNDA LA
RAMADHANI. Kupitia tunda la Ramadhani utajifunza hadithi mbili tatu za Mtume
zihusianazo na funga tukufu ya Mwezi mtukufu wa Ramadhani. Hadithi hizi
zitakuwa zikifuatiwa na maelezo mafupi ili kuziweka wazi kwa wasomaji.
i) MINBARI YA RAMDHANI NA KHUTBA YA MTUME KATIKA KUUKARIBISHA
MWEZI MTUKUFU WA RAMADHANI :
Jueni na eleweni enyi ndugu zanguni Waislamu kwamba Mwenyezi Mungu Mtukufu
amejaalia mafanikio ya duniani ni ya muda mfupi, yenye kwisha na kuondoka, na
mafanikio ya akhera ndiyo yenye kusalia/kubakia milele. Haya mafanikio ya kudumu,
hayapatikani ila kwa kupitia barabara ngumu ya "TAQ-WA" kumcha
Mwenyezi Mungu na kumtii na kumfuata Bwana Mtume - Rehema na Amani zimshukie-.
Katika jumla ya nguzo kuu za Taqwa ni kuufunga huu mwezi mtukufu wa Ramadhani
ambao Allah ameujaalia kuwa ni REHMA kwa viumbe. Nao kama mjuavyo ndio mwezi
ambao imeteremshwa ndani yake Qur-ani Tukufu ikiwa ni muongozo kwa watu wote.
Muongozo uliosheheni hoja wazi za uongofu na upambanuzi baina ya haki na
batili. Ramadhani pia ni mwezi ambao hufunguliwa ndani yake milango ya pepo na
kufungwa milango ya moto. Ni kwa kuuzingatia umuhimu na nafasi ya mwezi wa
Ramadhani, ndipo Bwana Mtume akaitoa Khutba yake tukufu, khutba ya kihistoria,
khutba kongwe katika kuupokea na kuukaribisha mwezi mtukufu wa Ramadhani.
Imepokelewa na Salmaan Alfaarisy - Allah amuwie Radhi - amesema :
Alitukhutubia Mtume wa Mwenyezi Mungu - Rehema na Amani zimshukie - katika siku
ya mwisho ya mwezi wa Shaabani, akasema : "Enyi watu, umekufikieni mwezi
mtukufu wenye baraka. Ndani ya mwezi huu umo usiku wa LAYLATIL QADRI usiku
ambao ni bora kuliko miezi alfu moja. Mwenyezi Mungu amejaalia funga ya mwezi
huu kuwa ni FARADHI na kisimamo (cha ibada) cha usiku wake kuwa ni SUNNAH.
Atakayejikurubisha (kwa Mola wake) ndani ya mwezi huu kwa (kutenda) jambo
lolote la kheri, (malipo, jazaa yake) itakuwa ni kama
mtu aliyetekeleza fardhi katika miezi mingine. Na atakayetekeleza fardhi katika
mwezi huu, atakuwa ni kama mtu aliyetekeleza
fardhi sabini katika miezi mingine. Na mwezi huu ni mwezi wa SUBIRA, nao ni mwezi
ambao mwanzo wake ni REHEMA na katikati yake ni MAGHFIRA/MSAMAHA WA ALLAH na
mwisho wake ni KUACHWA HURU NA ADHABU YA MOTO. Yeyote atakayemfuturisha
mfungaji ndani ya mwezi huu, (ujira wa futari hiyo) utakuwa ni maghfira ya
madhambi yake (mfuturishaji) na kuachwa huru na adhabu ya moto na atapata ujira
kama aupatao mfungaji bila ya kupungua
chochote katika ujira/thawabu zake (mfungaji)". Tukasema : Ewe Mtume wa
Mwenyezi Mungu, sio sote tunaweza kupata (kitu) cha kumfuturisha huyo mfungaji.
(Mtume) akawajibu : "Mwenyezi Mungu humpa thawabu hizi yule
atakayemfuturisha mfungaji ndani ya mwezi huu kwa onjo/funda ya maziwa au
(kokwa ya) tende au funda ya maji. Na atakayemshibisha ndani ya mwezi huu
mfungaji, itakuwa ujira (wa shibe hiyo) ni maghufira ya madhambi yake
(mshibishaji) na Mola wake atamnywesha katika hodhi (birika) langu funda moja
ambayo hatopata kiu baada yake kabisa. Na atakuwa na ujira kama
aupatao mfungaji bila ya kupungua chochote katika ujira wake (mfungaji). Na
atakayempunguzia kazi mtumishi/mfanyakazi wake ndani ya mwezi huu, Mwenyezi
Mungu atamghufiria madhambi yake na kumuacha huru na adhabu ya moto. Basi
kithirisheni sana
ndani ya mwezi huu mambo manne. Mtamridhisha Mola wenu kwa kutenda mambo mawili
kati ya manne hayo; na mambo mawili hamjikwasii (hamna budi) nayo. Ama hayo
mambo mawili mtakayoridhisha nayo Mola wenu ni shahada (kushuhudia kwamba
hapana Mola apasaye kuabudiwa kwa haki ila ALLAH) na mumtake maghfira. Na ama
yale mambo mawili msiyojikwasia nayo ni mumuombe Mola wenu pepo na
mjilinde/mjikinge kwake na (adhabu) ya moto". Ibn Khuzaymah katika sahihi
yake.
MAELEZO : Ikiwa tunafuatana pamoja, tunaweza tukaigawa hadithi hii tukufu
ambayo ni khutba kongwe iliyo hai hadi leo na itaendelea kuwa hai mpaka mwisho
wa dunia. Khutba hii iliyotolewa na Khatibu mahiri, Bwana Mtume katika
kuukaribisha mwezi mtukufu wa Ramadhani, inagawanyika katika sehemu kuu tatu au
tuseme ina vipengele vikuu vitatu. Ukiizingatia hadithi utakuta mwanzo wa
khutba yake, Bwana Mtume - Rehema na Amani zimshukie - anawafahamisha maswahaba
na umma mzima juu ya utukufu, ubora, cheo na nafasi ya mwezi wa Ramadhani. Kuna
hekima/falsafa gani ndani ya maelezo haya ? Mtume anauelezea mwezi wa Ramadhani
ni mwezi wa namna gani ili muislamu aujue, kwani waswahili husema asiyekujua
hakuthamini. Akishaujua atauthamini na kuupa hadhi yake unayostahili.
Kuuthamini na kuupa heshima mwezi wa Ramdhani ni kuzidisha sana TWAA kwa Mwenyezi Mungu kwa kufanya
namna mbali mbali za ibada na mambo mengine ya kheri.
Sehemu ya pili ya hadithi, Bwana Mtume anataja fadhila/faida na ubora wa
mwezi wa mtukufu wa Ramadhani na kuwa ibada yeyote inayofanywa ndani ya mwezi
huu hailingani kithawabu/kiujira na ile ibada inayofanywa katika miezi mingine.
Kwa hiyo basi, Ramadhani ni ndio musimu wako wa ibada. Kadhalika Bwana Mtume
anatuelezea malipo na thawabu adhimu anazozipata mja mwenye kumfuturisha
nduguye muislamu katika mwezi huu wa Ramadhani. Hapa Bwana Mtume anaashiria
moyo wa ukarimu na upendo utakiwao waislamu wajipambe na kuwa nao. Kwani waislamu
wakipendana watakuwa ni wamoja na mshikamano, na wakishikamana watautawala
ulimwengu na hapatakuwa na nguvu ya kuwashinda, si magharibi wala mashariki.
Kisha ndipo Bwana Mtume akaikhitimisha khutuba yake kwa kutoa wito muhimu
kwa waislamu. Akawataka wakithithirishe sana
kumpwekesha Mola wao kwa kuleta kalima ya shahada na wamtake sana maghfira. Hali kadhalika akawataka
waislamu wakithirishe mno kumuomba Mola wao pepo na wamuombe awakinge na moto
wa jahanamu. Ili kuutekeleza wito huu ndipo
wanazuoni wetu wema -Allah awarehemu- wakatuwekea uradi uletwao msikitini ndani
ya mwezi wa Ramadhani. Chimbuko la uradi huu ni ile sehemu ya mwisho ya
hadithi. Uradi wenyewe ni huu :
ASH-HADU AN LAA ILAHA ILLA-LLAHU NASTAGHFIRULLAH, NAS-ALUKAL-JANNATA
WANA'UDHU BIKA MINAN-NAAR ALLAHUMMA INNAKA AFUWWUN, TUHIBBUL-AFWA FA'FU 'ANNAA
YAA KARIIM
Tunashuhudia kuwa hapana Mola apasaye kuabudiwa kwa haki ila Allah,
Tunakuomba maghfira (msamaha wa madhambi) Ewe Allah, Tunakuomba pepo na
tunajikinga kwako na moto, Ewe Allah, wewe mimi ni msamehevu na unapenda
msamaha, basi tusamehe Ewe KARIMU.
Haya shime ndugu zanguni waislamu, tukithirishe kuuleta uradi huu ndani ya
mwezi wa mavuno; mwezi mtukufu wa Ramadhani. Kwa kufanya hivyo tutakuwa
tumeuitikia wito wa Bwana Mtume kwa maslahi na faida yetu wenyewe.
TUNDA LA RAMADHANI :
Karibu ndugu yangu muislamu katika bustani ya Bwana Mtume -Rehema na Amani
zimshukie - uchume utakavyo na kula kiasi chako matunda matamu, mazuri
yasiyokwisha hamu; matunda ya Ramadhani. Ili
ufaidike na kunufaika na matunda haya unatakiwa uingie ndani ya bustani hii
tukufu kwa unyenyekevu, utulivu, adabu, heshima na usikivu.
TUNDA LA KWANZA - DUA YA KUFUTURU
Amepokea Ibn Majah kutokana na hadithi ya Abdillah Ibn Amri (amesema Mtume)
: YUNA MFUNGAJI WAKATI WA KUFUTURU KWAKE DUA ISIYOREJESHWA (yenye kujibiwa bila
ya kipingamizi)". Ni kwa sababu hiyo ndiyo Mtume alikuwa akisema (wakati
wa kufuturu) :
[ALLAHUMMA INNIY LAKA SWUMTU WA'ALAA RIZQIKA AFTWARTU FAGH-FIRLIY MAA
QADDAMTU WA MAA AKHARTU DHAHABAD-DHWAMAU WABTALLIT-'URUQU WATHABATAL AJRU
IN-SHAALLAHU TAALA]
Maana yake : "Ewe Mola wa haki ni kwa ajili yako tu nimefunga na
nimefuturu kwa riziki yako. Basi (nakuomba) unisamehe dhambi zangu
zilizotangulia na zijazo. Kiu kimeondoka na mishipa imelowana na ujira umethibiti
pindipo atakapo Mwenyezi Mungu Mtukufu"
Haya shime ndugu zanguni waislamu, tumuige Mtume wetu katika hili na
mengineyo ili tutengenekewe duniani na akhera. Usikubali kuipoteza fursa hii
adimu ya kukubaliwa duao, omba na Mola Karimu atakupa.
TUNDA LA PILI : FADHILA ZA KUHARAKIA KUFUTURU :
Imepokelewa hadithi kutoka kwa Abuu Hurayrah - Allah amuwie Radhi - amesema,
Amesema Mtume wa Mwenyezi Mungu - Rehema na Amani zimshukie- "AMESEMA
MWENYEZI MUNGU : HAKIKA WAJA WANGU WAPENDEZAO SANA KWANGU NI WALE WAHARIKIAO
KUFUTURU" Ahmad na Tirmidhi.
MAELEZO : Ni vema mtu akafanya haraka kufuturu, maadam ana
uhakika wa kutua/kuzama kwa jua. Ikiwa hana uhakika, basi ni vema akasubiri
adhana ili asije akafuturu kabla ya muda. Haya zingatia upendwe na Mola wako.
TUNDA LA TATU:Vipi Umsaidie Mwanao Afunge Mwezi Wa
Ramadhani?
Ndungu Zangu katika iman(mwanajumuiya)Siyamu
Ya Mtoto Ni Mas'uliya Ya Mama ,kabla ya Baba .. Nimas'uliya Kubwa Kwasababu
Mtoto Hajuwi Umuhimu Wa Siyamu Katika Umri wake..Mama Mtu Anashtuka Kuwa Mtoto
Wake Anamwambiya Kuwa Yeye Kafunga Lakini Hajuwi Kuwa Mwanawe Anakula.
Ndugu Zangu Kina Mama hata akina baba, Ukijuwa Kuwa Mtoto Wako Alikuwa Akila
Nahuku Akikuwambiya Kuwa Yeye Kafunga Fanya yafuatayo :
1: Ukishamjua Mtoto Anafunga jaribu Kumpa vijizawadi Kwa Kila Siku
Anayo Funga. Au muwahiidi zawadi katika sikukuu ya IDD,kwa mfano kumnunulia
nguo nzuri au viatu vizuri.
2: Usimfokee Na Kumwambia Kuwa Wewe Unasema Uwongo Unajidai
Umefunga Lakini Unakula Nyuma Yangu ...mwambiye Kwa Njiya
Nyengine Na Kumtolea Hadithi Za Watoto Walokuwa Wakisema
Uwongo Kwa Wazee Wao Na Natija Yake Bila Yeye Kuhisi
Unamkusudia Yeye.
3: Kumfundisha Mtoto Kufunga Kidogo Kidogo Kwa Mujibu wa Umri
Wake.
4: Kumsifu Mbele Ya Wenziwe Anapo Funga.
5: Hakikisha unawaunganisha a wanaofunga Katika Family kwa
Kufturu Pamoja Ili Ajuwe Kuwa Alokuwa Hawafungi wanafanya Makosa.
6: Usiweke Chakula Anachokipenda Mtoto Wako Mbele Yake
(sweets) Kabla Ya Iftar Akaja Akadhaifika.
7: Ahisi Mtoto Wako Katika Mwezi Mtukufu Wa Ramadhan Umuhimu
Wa Mwezi Wa
Ramadhani .. Kumchukuwa Katika Darsa Kukaa Naye
Nakusoma Quraan na Hadith ...